Home » » Watoto 1,300 Mikindani wanaishi kwenye mazingira hatarishi

Watoto 1,300 Mikindani wanaishi kwenye mazingira hatarishi

Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399. 
Watoto zaidi ya 1,300 katika Manispaa ya Mtwara –Mikindani wanaishi katika mazingira hatarishi  kutokana na wazazi au walezi wao kushindwa  kumudu  mahitaji yao.
Hali hiyo inasababisha  kuongezeka  kwa  watoto wa mitaani mjini hapo na endapo hatua za kupambana na tatizo hilo hazitachukuliwa mapema hatma ya maisha yao iko mashakani.

Katibu wa shirika lisilo la kiserikali Faidika Wote Pamoja (Fawopa) Baltazar Komba, alieleza jana wakati akifungua mafunzo ya  kuhudumia watoto wanaoishi katika mazingira hatarishi, (MVCC) kwa kata  za Mtonya, na Kisungule Mjini hapa.

Alisema  kufuatia ongezeko hilo shirika  limeanzisha mradi wa kuwatambua  watoto hao na kutoa mafunzo ya kuwezesha  kutafuta rasilimali  katika  maeneo yao kwa ajili ya kuwaendeleza kutoka kwenye  Kata zao badala ya kutegemea misaada ya  wafadhili.

"Tumeshuhudia wafadhili wengi wanakuja na kutoa misaada mbalimbali  kama sare za shule, daftari, viatu, na hata mabegi ya bei kubwa, lakini pindi wanapoondoka  watoto hawa wanashindwa kuendelea na masomo, "alisema.

Alieleza kuwa "lengo la mradi huu ni kuwapatia elimu viongozi wa kata pamoja na wanakamati ya kusaidia kushawishi jamii kuona umuhimu wa kumsaidia mtu asiyejiweza  kwa kutoa misaada mbalimbali hasa kwa  watoto walio na uhitaji wa kwenda shule,"alifafanua Komba.

Kwa upande wake mwezeshaji wa vikundi vya wanawake kusaidia watoto hao  Fatma Issa , alisema kupitia mafunzo hayo yameweza kuleta manufaa kwa wananwake ambao hawakuwa na uwezo wa kuhudumia watoto wao.

"Baada ya kupata mafunzo kama haya, wanawake waliamua  kuunda vikundi na kuanza kukopeshana  mwenye nacho akamkopesha asiyenacho kwa riba ya asilimia mbili na mafunzo haya yamewawezesha wanawake 123, ambao hapo awali hawakuwa na uwezo wa kuwapeleka watoto shule," alisema Issa.

Aidha  alifafanua kuwa, kupitia vikundi hivyo hivi  sasa watoto 255 wanakwenda shule, baada ya wanawake hao kuamua kuinuana kupitia mafunzo na kutoa elimu kwa wanakikundi wasiojua kusoma na kuandika.
 
CHANZO: NIPASHE

0 comments:

 
Supported by Tone Multimedia Company Limited
Copyright © 2012. Mtwara yetu - All Rights Reserved
Designed by Fredy Tony Njeje
Proudly powered by Blogs za Mikoa