KITUO cha Kanisa la Evangelist Assemblies of God Tanzania (EAGT)
cha Rahaleo Mtwara hakina majengo ya kuwalelea watoto yatima takriban
53 kituoni hapo.
Hayo yalibainishwa mwishoni mwa wiki na mkurugenzi wa kituo hicho
Caroline Mkwele wakati wafanyakazi wa Kampuni ya Simu za Mkononi ya
Vodacom Tanzania walipotembelea kituoni hapo kukabidhi msaada wa
chakula, fedha na vitu mbalimbali.
Alisema hali hiyo inasababisha baadhi ya watoto kulelewa na walezi majumbani.
“Changamoto tulizonazo ni nyingi lakini zaidi ni hili la kukosa kituo
rasmi kwa maana ya majengo ya kuwahifadhi watoto hawa kwa pamoja,
usipowaweka hawa watoto pamoja uwezekano wa kuwa na tabia tofauti ni
mkubwa.
“Hivyo kutokana na ukosefu wa kituo inatulazimu kukutana na watoto hawa kila siku ya Jumamosi,” alisema.
Meneja wa Vodacom Kanda ya Kusini Henry Tzamburakis alisema yatima
wanahitaji kupata elimu na mahitaji muhimu kama walivyo watu wengine.
“Napenda kutoa wito tusingojee mpaka kampuni ijikusanye ndio tuje
kutoa msaada, mtu yeyote anaweza kufanya hivi kwani haihitaji mpaka uwe
tajiri sana, ukiwa na chakula, nguo, chochote kile ambacho unaona
kitawafaa watoto hawa usisite kuwaletea,” alisema Tzamburakis wakati
akitoa msaada.
Boniface Seleman mmoja wa watoto yatima wanaolelewa katika kituo
hicho alisema: “Tunashukuru kwa msaada huu, nawaomba msife moyo
kutusaidia kwani bado tunahitaji sana na pia tunathamini kwa kile
mnachokifanya.”
Chanzo;Tanzania Daima
0 comments:
Post a Comment