MBUNGE wa Nanyumbu,
Dustan Mkapa (CCM), anatuhumiwa kujihusisha na biashara ya uvunaji
haramu wa mbao na magogo katika msitu wa hifadhi ya Mtambaswala uliopo
mkoani Mtwara. Aidha amedaiwa kuorodhesha majina ya uongo ya watu
wanaojihusisha na ujangili, ili kufanikisha nia yake ya kukwepa
operesheni ya safisha ujangili inayoendeshwa na Jeshi la Wananchi wa
Tanzania (JWTZ), kwa kushirikiana na askari wa wanyamapori.
Imedaiwa kuwa hatua ya mbunge huyo imesababisha wananchi wa jimbo lake, kuyakimbia makazi yao kutokana na kuhofia kukamatwa.
Hofu
hiyo imekuja kutokana na wanajeshi wanaoshiriki kwenye operesheni hiyo
kupiga, kujeruhi na kufikia hatua ya kuua watu wawili.
Wakizungumza
na RAI Jumatano kwa nyakati tofauti kwa masharti ya kutotajwa majina
kwa kuhofia kipigo kinachoendelea kutolewa jimboni humo, baadhi ya
wakazi wanaoishi kwenye jimbo hilo walisema kuwa wamehuzunishwa na
kitendo cha mbunge wao kuwahusisha na uharibifu wa misitu ya hifadhi.
Mmoja
wa wananchi hao, alisema taarifa kuhusu majina yaliyoorodheshwa na
mbunge huyo, zilitolewa na mmoja wa askari waliopo katika jimbo hilo.
“Tumeshindwa
kumwelewa mbunge wetu, anatambua kabisa kwamba yeye anajihusisha na
biashara hii ya kuvuna mbao na magogo kwenye hizo hifadhi kwa kuwatumia
baadhi ya vijana hapa vijijini, lakini anatusingizia sisi.
“Anapotugeuka
na kudai kuwa sisi ndio tunaohusika na biashara hiyo, tunashindwa
kumuelewa kwa sababu hili ni jambo ambalo limeleta madhara kwetu ambao
hatuhusiki,” alisema.
Akizungumza na RAI Jumatano, Diwani wa Kata
ya Napacho katika Jimbo la Nanyumbu, Mary Mtopa (CCM), alikiri uwepo wa
vipigo na vifo katika kata yake, ambavyo vimetokana na operesheni hiyo.
Akizungumzia
kuhusu taarifa za mbunge huyo kujihusisha na biashara hiyo, Mtopa
alisema hana uhakika kwa kuwa hiyo ni biashara ya siri ambayo huwezi
kumfahamu mhusika mara moja.
“Kusema kweli katika kata yangu hali
si shwari, wananchi wameyakimbia makazi yao kutokana na operesheni hiyo,
ni kweli nimesikia kuna majina wamepatiwa askari, lakini pia sijajua
wamepatiwa na nani kwa sababu hili ni suala la kiusalama zaidi.
“Kuna
mwananchi mmoja ambaye alikuwa mwalimu wa shule ya msingi, namfahamu
kwa jina moja la Guto, sasa ni marehemu, inasemekana wiki iliyopita
alichukuliwa nyumbani kwake usiku yeye na watoto wake wakapelekwa kwenye
kambi ya hao wanajeshi inayofahamika kwa jina la Mtema Upinde.
“Walipofika
huko kambini kwa mujibu wa maelezo ya watoto wake, wao walirudishwa,
lakini siku iliyofuata walipewa taarifa kuwa baba yao yupo hospitali,
kumbe alikuwa ameshafariki kwa kipigo alichopewa,” alisema.
Kwa upande wake, Mkuu wa Wilaya ya Nanyumbu, Festo Kiswaga, alisema hana taarifa hizo kwa sababu yuko nje ya eneo lake la kazi.
Alipoulizwa
Mkapa na RAI Jumatano kuhusu ukweli wa madai hayo, alikana kuhusika na
biashara hiyo na hata kuorodhesha majina ya watuhumiwa wa ujangili.
“Si
kweli kwamba najihusisha na biashara hiyo, hizo ni propaganda tu
zinaendeshwa ndani ya jimbo langu, kwanza nilikuwa naumwa hivyo sifahamu
nini kinachoendelea huko,” alisema.
Alipotafutwa Msemaji wa JWTZ,
Meja Erick Komba, kuzungumzia madai ya wanajeshi kupiga na kuua raia,
alisema kuwa hana taarifa hizo na hata hiyo operesheni ya kusaka
majangili haijui.
“Ninachofahamu ni kwamba wanafanya Operesheni Kimbunga na si ya ujangili, ngoja nifuatilie,” alisema.
Madai
ya Mkapa kuhusishwa na biashara hiyo yanawiana na yale yaliyowahi
kutolewa na Waziri wa Maliasili na Utalii, Khamis Kagasheki, kwamba wapo
baadhi ya viongozi wa Serikali wanaojihusisha na biashara hiyo haramu.
CHANZO DIRA
0 comments:
Post a Comment