Mbunge wa Mtwara Mjini (CCM), Hasnein Murji (kushoto) akiingia katika
chumba cha Mahakama ya Hakimu Mkazi Mkoa wa Mtwara jana kusomewa shtaka
la kufanya uchochezi. Picha na Haika Kimaro.Naibu
Waziri wa Nishati na Madini, Simba Chawene akizungumza jambo na Mbunge
wa Mtwara mjini, Hasnain Murji aliyekaa katika vikao vya mbunge mjini
mwaka huu.
MBUNGE wa Mtwara Mjini (CCM), Hasnain
Murji (46) amepandishwa kizimbani katika Mahakama ya Hakimu Mkazi mjini
hapa, mbele ya Hakimu Mkazi Mwandamizi Mfawidhi, Dynes Lyimo kujibu
mashitaka ya uchochezi yanayomkabili.
Mbunge huyo ambaye alikamatwa siku tatu
zilizopita jana alisomewa mashitaka na mwendesha mashitaka, Mwanasheria
wa Serikali, Kisheni Mtalemwa akisaid
iana na Zuberi Mkakatu, na kudai
kuwa Januari 19 maeneo ya Ligula mjini hapa alichochea watu kufanya
vurugu kinyume cha sheria.
Murji ambaye alirudishwa rumande baada
ya kukana mashitaka na kushindwa kutimiza masharti ya dhamana, anatetewa
na Wakili Chaula Msechu wa Kampuni ya uwakili ya C and M Advocates ya
Dar es Salaam.
Akisoma masharti ya dhamana, Hakimu
Lyimo alisema mshitakiwa alitakiwa kuwasilisha mahakamani hati ya
kusafiria, mdhamini mmoja mwenye mali isiyohamishika, yenye thamani
isiyopungua Sh milioni 20 na iwe imefanyiwa tathmini pia asifanye
mikutano yoyote ya hadhara bila kibali cha Kamanda wa Polisi wa Mkoa.
Baada ya Hakimu kusoma masharti ya
dhamana, mshitakiwa alijieleza, kwamba hati yake ya kusafiria iko Dar es
Salaam hivyo kuwa vigumu kwa kuiwasilisha mahakamani hapo kwa muda huo,
hali ambayo ilizua mabishano ya kisheria kati ya wakili wa Serikali na
wa upande wa utetezi.
Mwanasheria wa Serikali aliiambia
Mahakama, kwamba kwa kuwa kuwasilisha hati hiyo mahakamani ni moja kati
ya masharti ya dhamana, na kwa kuwa mshitakiwa alikiri kushindwa
kuiwasilisha jana, basi Mahakama ni vema ikazingatia masharti iliyoweka
na mshitakiwa apewe muda wa kutimiza masharti hayo.
“Mahakama yako imeweka masharti ambayo
yamesomwa mbele ya mshitakiwa, na kuwasilisha hati ya kusafiria ni moja
ya masharti yanayotakiwa kutimizwa, hivyo naiomba iyazingatie na
atakapoyatimiza basi haki yake hii ya msingi ya kupewa dhamana itolewe,”
alisema Kisheni.
Baada ya hoja ya upande wa Serikali,
Wakili Msechu aliiomba Mahakama impe dhamana mteja wake, ili awe nje
huku taratibu za kufuata hati hiyo Dar es Salaam zikifanyika, kwa kuwa
mshitakiwa ni kiongozi aliyechaguliwa na watu na alionesha ushirikiano
na Polisi hata pale alipotakiwa kuripoti kituo cha Polisi.
“Naiomba Mahakama yako impe dhamana
mteja wangu, kwa kuwa ni kiongozi wa kuchaguliwa na wananchi, ametimiza
masharti mengine, ni mwaminifu na hata alipojulishwa juu ya mashitaka
yake aliripoti mwenyewe Polisi na baada ya siku mbili au tatu
tutawasilisha hati hiyo hapa mahakamani,” alisema Chaula.
Baada ya hoja hizo, Hakimu Lyimo alitoa
msimamo wa kisheria juu ya suala hilo ambapo alisema kwa kuwa
kuwasilisha hati hiyo mahakamani ni sehemu ya masharti ya dhamana, hivyo
Mahakama iliona mshitakiwa hajatimiza masharti na hivyo kurudishwa
rumande hadi kesho Mahakama itakapopitia vielelezo vyake vya dhamana.
Kesi hiyo iliendelea sambamba na zingine
zinazohusu vurugu za Mei 22 na 23 ambapo watuhumiwa zaidi ya 90
walifikishwa hapo kujibu tuhuma za kuhusika na vurugu hizo.
Lakini kinyume na masharti ya dhamana ya
Murji washitakiwa wengine walitakiwa kuwa na mdhamini mmoja mwenye mali
zisizohamishika na kutambuliwa na watendaji wa mitaa katika maeneo
wanamoishi, masharti ambayo yalitimizwa na baadhi yao na walioshindwa
walirejeshwa rumande.
Viongozi wengine Wakati huohuo, viongozi
wanne wa vyama vya upinzani watafikishwa mahakamani hapo kwa mara ya
pili Juni 13, baada ya kufikishwa katika Mahakama hiyo Juni 4 kwa mara
ya kwanza wakikabiliwa na mashitaka matatu likiwamo la kula njama,
kufanya uchochezi na kuamsha hisia mbaya kwa wakazi wa Tanzania.
Viongozi hao ni Katani Ahmed Katani (33)
Mwenyekiti wa Vijana CUF na Saidi Kulaga (45) Katibu wa Wilaya ya
Mtwara CUF, Hassan Uledi (35) Mwenyekiti wa NCCR-Mageuzi wa Wilaya ya
Mtwara na Hamza Licheta (51) Katibu Mwenezi wa TLP wa Mkoa wa Mtwara,
wote wakazi wa Mtwara.
CHANZA HABARILEO
0 comments:
Post a Comment