Abdallah Bakari, Mtwara
WAKAZI wa Kijiji cha Msijute, Halmashauri ya Wilaya Mtwara, mkoani hapa wametaka katika Katiba ijayo, Rais aongezewe madaraka ili kumpa nguvu ya kufanya uamuzi.
Wakitoa maoni yao mbele ya Tume ya kukusanya maoni ya Katiba, wakazi hao bila kufafanua aina ya madaraka anayopaswa kuongezewa Rais, walisema hawaoni umuhimu wa kupunguza madaraka ya kiongozi huyo wa juu wa nchi.
Saidi Nawanda (62) na Selemani Likoko (68) kwa nyakati tofauti walisema mamlaka aliyonayo Rais kwa sasa hayatoshi hivyo ni muhimu aongezewe.
“Rais aongezewe madaraka, ili akisema jambo basi litekelezwe” alisema Nawanda bila ya kufafanua madaraka anayopaswa kuongezewa.
Maoni kama hayo pia yalitolewa na Likoko, ambaye alihoji iweje Rais apunguziwe madaraka badala ya kuongezewa.
“Rais aongezewe madaraka, na kamwe asipunguziwe” alisema Likoko.
Katika mkutano huo ulioendeshwa na mwenyekiti wa timu iliyopo hapa, Sengondo Mvungi, ulitanguliwa na maelezo ya umuhimu wa kutoa maoni ya Katiba yaliyotolewa na Mjumbe wa Tume hiyo, Kibibi Hassan ambaye aliwaambia ni wakati mwafaka kwao kutengeneza Katiba waitakayo.
“Tumieni fursa hii kutoa maoni yenu, jisikieni huru, utakachosema ndicho kitakachonukuliwa, baada ya hapa tutarudi kwenu tukiwa na rasimu ya Katiba, safari hiyo tutaiwasilisha kwenu kupitia mabaraza ya wilaya” alisema Hassan.
Aliongeza kuwa “Tutaipeleka kwenye Bunge maalumu la Katiba na baada ya hapo italetwa kwenu kwa ajili ya kupigia kura ya ndiyo na hapana, msiwe na wasiwasi, hii ni Katiba yenu.”
Chanzo: Mwananchi
0 comments:
Post a Comment