Home » » Kiwanda kipya cha cementi Mtwara chachu ya uchumi

Kiwanda kipya cha cementi Mtwara chachu ya uchumi


Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa Kituo cha Uwekezaji Tanzania (TIC), Bw. Raymond Mbilinyi (katikati) akionyeshwa mchoro wa ramani na mtaalamu wa udongo, Bw. John Olalokun (kushoto) wa kiwanda cha Simenti cha Dangote kinachotarajiwa kujengwa mkoani Mtwara. Bw. Mbilinyi alifanya ziara hiyo kuangalia maendeleo ya mradi huo mwishoni mwa wiki. Kulia ni meneja mkuu wa kiwanda hicho Bw. Dilip Musale.
Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa Kituo cha Uwekezaji Tanzania (TIC), Bw. Raymond Mbilinyi (kulia) akimsikiliza kwa makini mtaalamu wa udongo, Bw. John Olalokun wa kiwanda cha Simenti cha Dangote kinachotarajiwa kujengwa mkoani Mtwara katika ziara aliyoifanya kutembelea eneo hilo na kuangalia maendeleo ya utekelezaji wa ujenzi wa kiwanda hicho mwishoni mwa wiki. Ujenzi huo unafanywa na mwekezaji na tajiri maarufu raia wa Nigeria, Bw. Aliko Dangote.

Na Mwandishi wetu, Mtwara

Zaidi ya tani milioni mbili za saruji zinatarajiwa kuzalishwa nchini kwa mwaka mara baada ya kukamilika kwa ujenzi wa kiwanda cha kutengenezea simenti cha Dangote katika Mkoa wa Mtwara.

Pamoja na kiwango hicho cha simenti kuzalishwa, pia inatarajiwa kupatikana kwa ajira 400 za kudumu ujenzi huo utakapokamilika.

Uwekezaji huu unafanywa na tajiri maarufu raia wa Nigeria, Bw. Aliko Dangote ambaye ana vitega uchumi vikubwa katika nchi mbalimbali duniani.

Hayo yameelezwa na Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa Kituo cha Uwekezaji Tanzania (TIC), Bw. Raymond Mbilinyi alipofanya ziara katika eneo ambapo uwekezaji mkubwa wa ujenzi wa kiwanda cha saruji cha Dangote unatarajia kuanza Mkoani Mtwara.

“Kukamilika kwa mradi huu mkubwa katika mkoa wa Mtwara kutazalisha zaidi ya tani milioni mbili za saruji, lakini pia ajira za kudumu zaidi ya mia nne zitapatikana, hii itasaidia kukuza uchumi wa watu wa kusini na kuongeza pato la taifa kwa ujumla,” alisema Mbilinyi mwishoni mwa wiki iliyopita alipokuwa akiongea na waandishi wa habari mkoani humo.

Akielezea umuhimu wa ujenzi wa kiwanda hicho ambacho kinatarajia kukamilika baada ya miezi kumi na nane, Bw. Mbilinyi alisema uwekezaji wa aina hii si tu utaweza kuzalisha ajira nyingi kwa watanzania bali utaongeza kasi ya kuchochea uwekezaji zaidi katika mikoa ya kusini mwa Tanzania.

“Kwa takwimu tulizonazo, hadi kufikia mwaka 2011 tulikua na upungufu wa zaidi ya tani milioni moja za simenti, hivyo kiwanda hiki kitasaidia kuondoa upungufu huu,” alisema.

Alisisitiza kuwa mazingira mazuri yalijengwa na serikali pamoja na sekta binafsi ndio yaliyosaidia kumpata muwekezaji huyu mkubwa wa simenti katika Bara la Afrika kuja kuwekeza hapa Tanzania.

“Juhudi zetu zote kwa upande wa serikali na kwa upande wa sekta binafsi ndizo zilizosababisha muwekezaji huyu mkubwa kuja hapa kwetu hasa katika mkoa wa mtwara na kanda ya kusini kwa ujumla,” alisema na kuongeza kwamba serikali itaendelea kujenga mazingira bora ya kuvutia wawekezaji, si tu kwa viwanda vya simenti bali hata kwa viwanda vya aina nyingine.

Kwa upande wake Mkuu wa Mkoa wa Mtwara, kanali Mstaafu Joseph Simbakalia, alisema ujenzi wa kisasa siku zote unahitaji saruji hivyo uwekezaji huo umekua mkombozi kwa watu wa mikoa ya kusini na Tanzania kwa ujumla.

“Kukamilika kwa kiwanda hiki kutakuwa na faida kubwa sana kwa mkoa huu, hasa kiuchumi kutokana na mtwara kuwa na mafuta pamoja na gesi asilia ambayo inaweza kuongeza asilimia kubwa ya pato la Taifa na kuondoa umasikini katika nchi,” alisema Simbakalia.

Bwana Simbakalia aliongeza kuwa ni ukweli usiopingika kuwa Mkoa wake una ufursa nyingi sana za uwekezaji na miongoni mwao bado hazijafanyiwa uwekezaji unaotakiwa.

Naye mtaalamu wa masuala ya utafiti wa udongo kutoka katika kampuni ya simenti ya Dangote Bw. John Olalokun, amesema, wamefanya utafiti wa kutosha na kuona kuwa malighafi nyingi zinapatikana katika eneo husika na kuongeza kuwa hiyo ni faida kwao katika kuzalisha simenti kwa wingi mkoani humo.

Aliongeza kuwa kati ya walivyoangalia kufanya uwekezaji katika mkoa wa Mtwara ni kutokana na upungufu uliopo wa simenti katika mikoa ya kusini na hii imetokana na simenti nyingi kuelekezwa katika mikoa ya kaskazini mwa nchi.

0 comments:

 
Supported by Tone Multimedia Company Limited
Copyright © 2012. Mtwara yetu - All Rights Reserved
Designed by Fredy Tony Njeje
Proudly powered by Blogs za Mikoa