Home » » DC NDILLE ATAKA VYAMA VYA SIASA VISHIRIKISHWE UUZWAJI WA ARDHI

DC NDILLE ATAKA VYAMA VYA SIASA VISHIRIKISHWE UUZWAJI WA ARDHI

Na Faraji Feruzi, Mtwara

WATENDAJI wa serikali katika ngazi ya kata na vijiji katika Halmashauri ya Wilaya ya Mtwara Vijijini, mkoani Mtwara, wametakiwa kuwashirikisha viongozi mbalimbali wa vyama vya siasa ili kukomesha uuzaji holela wa ardhi katika halmashauri hiyo.

Ushauri huo umetolewa na Mkuu wa Wilaya hiyo, Williman Ndille, wakati akizungumza na wajumbe wa WDC katika Kata ya Naumbu, Kijiji cha Imekuwa.

DC Ndille pia alitumia ziara ya kujitambulisha na kutembelea miradi ya maendeleo ili kusikiliza kero za wananchi wa wilaya hiyo tangu kuteuliwa kwake.

Alisema kuna tabia ya wananchi kuuza maeneo yao kiholela kwa kisingizio cha ugumu wa maisha, hali inayosababisha ardhi nyingi katika vijiji mbalimbali kuangukia mikononi mwa wawekezaji feki ambao wanawarubuni viongozi wa vijiji pamoja na wananchi wa eneo husika kwa ahadi nyingi zisizotekelezeka.

DC Ndille alisema, popote pale watakapohitaji kuuzwa ardhi yenye ukubwa wa kuanzia hekari 250, ni budi kuwepo na ardhi ya kutosha ili kuepusha madhara pale eneo husika litakapouzwa.

Aidha alisema lazima kuwepo kwa makubaliano ya kutiliana saini na wanakijiji kwa kutumia mikutano mikuu ya vijiji, ikiwa ishara ya uuzwaji huo.

Mkuu huyo wa wilaya aliwataka viongozi hao kuhakikisha wanakuwa chanzo cha maisha bora kwa wale wanaowaongoza.

Wakichangia hoja mbalimbali katika kikao hicho, mmoja wa wajumbe, Hamisi Najuawali, aliwataka viongozi wa kata kutojiingiza katika suala la ruzuku ya pembejeo, ili kujiepusha na lawama.

Mjumbe mwingine, Omari Mengwa, aliitaka serikali kuhakikisha katika msimu ujao wa maandalizi ya zao la korosho, wanawashirikisha wakulima katika hatua yote ya utoaji maoni ya dawa zipi wanazozitaka na zile ambazo hawazitaki.

Katika hatua nyingine, Mengwa aliiomba serikali ya wilaya hiyo, kuwatafutia wakulima soko la mazao ya choroko, ufuta, mbaazi na mtama kutokana na ardhi ya kata ya Naumbu kukubalika kwa kilimo hicho, ili kutanua wigo wa mazao mbadala.

Katika hatua nyingine, ofisa ushirika wa halmashauri ya wilaya hiyo, Mohammed Lilanga, aliwasihi wakulima wa zao la korosho kujiunga na vyama vya ushirika ili waweze kupata fursa ya kupata elimu ya ushirika, upitishaji wa bei, mgawanyo wa maslahi, maamuzi ya pamoja na kuvijengea vyama hivyo uwezo.
Chanzo: Mtanzania

0 comments:

 
Supported by Tone Multimedia Company Limited
Copyright © 2012. Mtwara yetu - All Rights Reserved
Designed by Fredy Tony Njeje
Proudly powered by Blogs za Mikoa