Mwandishi Wetu, Mtwara
SERIKALI imetangaza neema kwa wakazi wa Kitongoji cha Mchepa katika Kijiji cha Madimba, wilayani Mtwara ambalo litakuwa kitovu cha mradi wa uchimbaji wa gesi asilia, itakayokuwa suluhisho la matatizo ya umeme nchini.
Waziri wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo aliwaambia wananchi hao wakati wa uzinduzi wa mradi wa ujenzi wa bomba la kusafirishia gesi hiyo kuwa, wakazi wa Mchepa na Madimba, wataunganishiwa umeme bure.
“Tumeamua kwamba kila atakayehitaji umeme ataunganishiwa umeme huo bure, kwa hiyo kazi yenu ninyi, ni kuweka waya na vifaa vingine katika nyumba zetu halafu kazi ya kufikisha umeme kwenye nyumba zenu itakuwa ya Serikali, kwa hiyo jamani kazi kwenu,”alisema Profesa Muhongo.
Alisema Serikali pia imefanya mazungumzo na kampuni tatu za ujenzi wa bomba hilo, ili zianze kununua mazao ya wananchi wa eneo hilo zikiwemo mbogamboga na matunda, badala ya kuagiza mazao hayo kutoka Kenya na Afrika Kusini.
Profesa Muhongo alisema mipango iliyopo ni kuwezesha ujenzi wa viwanda vya usindikaji wa matunda na mbogamboga katika eneo la machimbo hayo ya gesi, ili kuwezesha bidhaa za wananchi wa eneo hilo kupata soko kwa urahisi zaidi kuliko ilivyo sasa.
“Pia tumeamua kwamba katika Chuo cha Veta cha Mtwara tutawasomesha vijana 50 bure kutoka Mtwara na katika ngazi ya taifa, tumeanza programu za kuwandaa wataalamu wa sekta ya gesi kwa kuanzisha mafunzo katika vyuo vyetu vya ndani na kuwapeleka wengine nje ya nchi,”alisema waziri huyo.
Kwa upande wake, Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati na Madini, Eliakimu Maswi alisema kupitia mradi wa ujenzi wa bomba hilo, Kitongoji cha Mchepa na Kijiji cha Madimba vitaboroshewa huduma za kijamii.
“Hapa tunasema kwamba lazima maisha yabadilike maana ndipo lilipo chimbuko la gesi, kwa hiyo huduma za elimu, afya na shughuli za michezo kwa kujenga viwanja vya michezo hiyo vitaboroshwa,”alisema
Waziri wa Nchi katika Ofisi ya Rais (Utawala Bora), George Mkuchika alisema lazima wananchi wa Mtwara wawe tayari kuupokea mradi huo kwa manufaa yao na nchi kwa jumla.
“Kuna baadhi ya watu hapa wanapita wanasema maneno ya uongo kwamba eti mradi huu utawanufaisha watu wengine kwa sababu gesi inapelekwa Dar es Salaam, sawa lakini huu ni mradi wa kitaifa, gesi ipo ya kutosha na hata ile inayozalishwa sasa watu wa Mtwara hawawezi kuitumia yote,”alisema Mkuchika.
Alisema kuanza kwa ujenzi wa mradi huo kuna maana kubwa ya kuwa sasa ni wakati wa wananchi wa mikoa ya Kusini, kupiga hatua za kimaendeleo”
Chanzo: Mwananchi
0 comments:
Post a Comment