Home » » POLISI YASIKITISHWA NA VURUGU MASASI

POLISI YASIKITISHWA NA VURUGU MASASI

CHAMA Cha Mapinduzi (CCM) katika Halmashauri ya mji wa Masasi mkoani Mtwara kimeibuka na ushindi kwa kujinyakulia viti 945 sawa na asilimia 88 ya kura zote zilizopigwa katika uchaguzi wa wenyeviti wa serikali za mitaa, vijiji pamoja na vitongoji uliofanyika kote nchini jana.
Akitoa matokeo hayo, Kaimu Mkurugenzi wa Halmashauri ya Mji wa Masasi, Henry Kagogoro alisema vyama vingine vilivyoshiriki kwenye uchaguzi huo ni pamoja na Chadema iliyojinyakulia viti 71 sawa na asilimia 6.6, CUF viti 53 sawa na asilimia 4.9 NLD kiti kimoja asilimia 0.09 huku chama cha ACT Tanzania kikiambulia patupu.
Alisema kuwa uchaguzi huo ulifanyika na kumalizika kwa amani na utulivu licha ya kuwepo kwa dosari ndogo zilizojitokeza katika maeneo kadhaa ikiwemo katika kituo cha Kitunda kata ya Mkuti ambapo kundi la watu wasiofahamika walivamia kituo hicho na kukatakata kwa mapanga masanduku ya kupigia kura kabla ya kuhesabu kura.
Kagogoro alisema kutokana na vurugu hizo pamoja na dosari zingine, vituo vinne vitalazimika kurudia uchaguzi huo ikiwemo kituo hicho cha kitongoji cha Kitunda, kitongoji cha Chingale na Lisekese katika kata ya Temeke pamoja na kituo cha kijiji cha Makulani ambacho mgombea wa Chadema na CCM wamefungana kwa kupata kura sawa Chadema wakipata kura 154 na CCM 154.
Alisema katika kituo cha Chingale jina la mgombea wa CUF lilisahaulika kwenye orodha ya wagombea huku katika kituo cha Lisekese mgombea aliwekwa katika nafasi ya mwenyekiti wa kijiji badala ya mwenyekiti wa kitongoji.
Alisema matarajio yalikuwa ni kuandikisha wapiga kura 41,078 katika uchaguzi huo huku waliofanikiwa kuandikishwa ni 21,689 na kwamba waliopiga kura ni 12,258 ambapo wanaume ni 5,476 na wanawake ni 6,682 takwimu zinaonesha kuwa kuna mwamko wa wananchi kujitokeza katika upigaji kura.
Kagogoro alisema katika uchaguzi huo Halmashauri ya mji wa Masasi mkoani Mtwara ilikuwa na idadi ya mitaa 59, vitongoji 145, vijiji 31, kata 14 na tarafa mbili.
Katika uchaguzi huo uliovuta hisia za watu wengi, yapo baadhi ya maeneo ya kata ambazo vyama vya upinzani vimekuwa na nguvu, ikiwemo katika kata ya Mkuti ambayo Chama cha Wananchi (CUF) kimejinyakulia viti vitatu huku CCM wakiambulia viti viwili na kwa kata ya Nyasa, Chadema imeibuka kidedea dhidi ya CCM.

Chanzo:Habari Leo
Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399.

0 comments:

 
Supported by Tone Multimedia Company Limited
Copyright © 2012. Mtwara yetu - All Rights Reserved
Designed by Fredy Tony Njeje
Proudly powered by Blogs za Mikoa