Home » » Viongozi wa Dini Mikoa ya Lindi na Mtwara kuhudhuria mafunzo ya gesi asilia na mafuta nchini Thailand

Viongozi wa Dini Mikoa ya Lindi na Mtwara kuhudhuria mafunzo ya gesi asilia na mafuta nchini Thailand

Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399. 

Mkurugenzi wa Utawala na Rasilimali Watu Wizara ya Nishati, Bw.Mrimia Mchomvu (kushoto) akiongea na Viongozi wa Dini kutoka mikoa ya Lindi na Mtwara waliofika Makao Makuu ya Wizara ya Nishati na Madini, kabla ya kuanza ziara ya mafunzo ya gesi asilia na Mafuta nchini Thailand.Kushoto kwa Mkurugenzi wa Utawala na Rasilimali Watu ni Mkurugenzi Msaidizi, Idara ya Sera na Mipango katika Wizara ya Nishati na Madini, Bw. Maseke Mabiki.
Baadhi ya Viongozi wa Dini watakaohudhuria mafunzo kuhusu Gesi asilia na Mafuta wakimsikiliza Mkurugenzi wa Utawala na Rasilimali Watu katika Wizara ya Nishati na Madini, Bw. Mrimia Mchomvu (hayupo pichani). 

Na Teresia Mhagama

Jumla ya Viongozi 19 wa Dini kutoka Mikoa ya Lindi na Mtwara wanatarajia kwenda nchini Thailand kuanzia tarehe 26 Aprili mwaka huu kwa ajili ya ziara ya mafunzo katika masuala ya gesi asilia na mafuta.

Ziara hiyo inatokana na juhudi za serikali katika kuhakisha elimu kuhusu masuala ya gesi asilia na mafuta inatolewa kwa wananchi wa kada mbalimbali ili waweze kufahamu mchakato mzima wa upatikanaji wa gesi asilia na mafuta, faida zake katika nyanja za kiuchumi na kijamii, changamoto zake na namna nchi nyingine zinavyotumia rasilimali hiyo katika kukuza uchumi.

Akiwaaga viongozi hao kwa niaba ya Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati na Madini, Mkurugenzi wa Utawala na Rasilimali Watu katika Wizara hiyo, Bw. Mrimia Mchomvu amesema kuwa Wizara ya Nishati na Madini imeratibu mafunzo hayo ili kujenga uelewa kwa viongozi hao ambao nao wataitumia elimu hiyo katika kuwaelimisha wananchi kuhusu sekta ndogo ya gesi asilia nchini ili kujenga uelewa wa pamoja utakaowafanya wananchi kushiriki na kuwa na mtazamo chanya kuhusu miradi mbalimbali ya gesi asilia nchini.

Bw. Mrimia Mchomvu ameeleza kuwa Serikali imeamua kuwapeleka viongozi hao nchini Thailand kwa kuwa nchi hiyo imepiga hatua kubwa kimaendeleo kutokana na kujipanga vizuri katika kutumia gesi asilia katika masuala mbalimbali ya kiuchumi na kuhakikisha wananchi wanafaidika na uwepo wa gesi hiyo.

Naye mjumbe wa Halmashauri Kuu ya Taifa ya Baraza Kuu la Waislam Tanzania (BAKWATA), Sheikh Said Sinani akiongea kwa niaba ya viongozi hao wa dini wanaokwenda nchini Thailand, aliishukuru Serikali kwa kuona umuhimu wa kushirikisha viongozi wa dini katika masuala mbalimbali ya kitaifa.

Amesema kuwa viongozi hao wa dini watahudhuria mafunzo hayo kwa umakini mkubwa na baada ya kupata uelewa mpana kuhusu gesi asilia na mafuta kutoka nchi nyingine, watakuwa mabalozi katika kutoa elimu kwa waumini wao ili kujenga uelewa wa pamoja kuhusu sekta hiyo nchini.

Pamoja na kujifunza masuala ya gesi asilia na mafuta nchini Thailand, viongozi hao watapata fursa ya kutembelea eneo maalum la viwanda ambalo ukuaji wake umetokana na kuwepo kwa gesi asilia, Shirika la Umma linalojishughulisha na masuala ya Gesi na Mafuta, Mamlaka ya Uzalishaji Umeme, Mamlaka ya Usambazaji Umeme, mtambo wa kuzalisha umeme unaotokana na Tungamotaka (Biomass), mtambo wa umeme wa jua, na mtambo wa umeme wa Bayogesi.

Viongozi hao wa Dini kutoka mikoa ya Lindi na Mtwara wanatarajia kurejea nchini mnamo tarehe 07 Mei, 2014.

0 comments:

 
Supported by Tone Multimedia Company Limited
Copyright © 2012. Mtwara yetu - All Rights Reserved
Designed by Fredy Tony Njeje
Proudly powered by Blogs za Mikoa