WAKAZI wa Mtwara vijini mkoani hapa wahimizwa kuwapeleka shule watoto
wao ili waweze kunufaika na fursa zitokanazo na kuwapo kwa gesi mikoa
ya kusini, badala ya kulalamika kuwa hawapati ajira katika miradi
iliyopo.
Wito huo ulitolewa jana na Mbunge wa Jimbo la Mtwara Vijijini, Hawa
Ghasia alipokuwa akizungumza na wananchi katika mkutano wa hadhara wa
kuwashukuru kwa kumchagua kuwa mbunge katika uchaguzi uliofanyika kwenye
kijiji cha Hiyari.
Ghasia alisema kuwa ni vyema wananchi wakawapeleka shule watoto wao
ili wapate elimu itakayowawezesha kupata sifa za kuajiriwa katika miradi
mbalimbali inayotarajiwa kuanzishwa mkoani hapa kutokana na kuwepo kwa
fursa ya gesi ambapo wawekezaji wanatarajiwa kufungua viwanda na miradi
mingine.
“Ninawaomba ndugu zangu tuwasomeshe watoto wetu ili waweze kuwa na
sifa za kuajiriwa katika miradi ya gesi itakayoanzishwa baadaye,”
alisema Ghasia.
Kauli hiyo ilikuja baada ya wakazi wa kijiji cha Hiyari kilipo
kiwanda cha saruji cha Dangote kudai kuwa kumekuwa na ubaguzi wa kutoa
ajira kiwandani hapo ambapo wakazi wa kijiji hicho hawapewi nafasi hata
ya kupata kazi za ufagizi na kumwagilia bustani ambazo walisema
hazihitaji elimu ya juu.
Akisoma taarifa ya kijiji mbele ya mbunge huyo, mjumbe wa serikali ya
kijiji hicho, Luis Usale, alisema kuwa wakazi wa kijiji hicho mara
kadhaa wamekuwa wakiomba kazi kiwandani hapo na kukosa huku wakipewa
wanaotoka mbali na hapo.
HABARI LEO
0 comments:
Post a Comment