Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399.
Mbunge wa Monduli, Edward Lowassa
Chama
cha Wananchi (CUF), kimeibuka na kumtetea aliyekuwa Mbunge wa Monduli,
Edward Lowassa (pichani juu), kwamba Chama Cha Mapinduzi (CCM),
kilimuonea kwa kukata jina katika ngazi ya Kamati ya Maadili na
kushindwa kulifikisha Kamati Kuu ya CCM (CC).
Lowassa alikatwa jina lake akiwa ni miongoni mwa wagombea 38 wa
urais kupitia CCM, lakini inadaiwa kwamba aliondolewa katika hatua za
awali kwenye Kamati ya Maadili.
Kadhalika, CUF kimesema kipo tayari kumpokea Lowassa ndani ya chama
hicho kwa kuwa ni msafi na hajawahi kufikishwa hata mahakamani kwa
ajili ya kushitakiwa kutokana na madai ya rushwa.
Kauli hiyo ilitolewa jana na Kaimu Mkurugenzi wa Habari na
Mawasiliano wa CUF, Abdul Kambaya, alipokuwa akizungumza katika kipindi
cha Pilikapilika za uchaguzi nchini kinachorushwa na kituo cha
Televisheni cha Star Tv.
Kambaya alirejea ripoti ya Kamati teule ya Bunge iliyoongozwa na
Dk. Harrison Mwakyembe mwaka 2008 kuchunguza kashfa ya Richmond ambayo
ilimng'oa Lowassa katika nafasi ya Waziri Mkuu.
Alisema katika kamati hiyo, Dk. Mwakyembe aliweka bayana kwamba
kila mtu aliyehusishwa ama kutajwa katika kashfa ya Richmond
angefikishwa mahakamani kujibu mashtaka.
Kambaya alisema mpaka sasa Lowassa hajawahi kufikishwa mahali
popote kushitakiwa na kwamba hatua hiyo inaoonyesha kwamba kiongozi huyo
hakuwa na kashfa yoyote.
Alisema lengo la CUF ni kuing'oa CCM na kwamba ukiona kuna mtu
mwenye uwezo mkubwa wa kuitikisa chama hicho na kukipasua wapo tayari
kumkaribisha ili washirikiane naye.
Alifafanua kuwa mtu ambaye siyo msafi hawezi kukaribishwa CUF na
kwamba Lowassa kama angekuwa mchafu angekuwa ameshitakiwa mahakamani
tangu alipojiuzuru mwaka 2008. Katika mjadala huo washirki walijadili
matumizi makubwa ya fedha yaliyojionyesha ndani ya CCM tangu mchakato wa
kuelekea Uchaguzi Mkuu ulipoanza.
Watu wengine waliojitokeza kumtetea Lowassa ni pamoja mwanachama
mwenye kadi namba nane ya CCM, Kingunge Ngombale Mwiru, ambaye alitamka
wazi kwamba kanuni na sheria ndani ya chama zilikiukwa.
Kingunge alisema haki haikutendeka kwa sababu Kamati ya Maadili kwa
mujibu wa kanuni na taratibu za CCM haina mamlaka ya kukata jina la
mgombea kwa sababu siyo kikao cha maamuzi. Wakati hayo yakisemwa, Katibu
wa Itikadi na Uenezi wa CCM, Nape Nnauye amewaonya watu wanaokisema
vibaya chama hicho na kwamba kitawachukulia hatua.
CHANZO:
NIPASHE
0 comments:
Post a Comment