Home » » Takukuru yawapiga mkwara waandikishaji wa Daftari.

Takukuru yawapiga mkwara waandikishaji wa Daftari.

Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399. 

Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru)
Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) wilaya ya Masasi, mkoani Mtwara imesema kuwa itawachukulia hatua kali za kisheria wasimamizi wa vituo vya uandikishaji wa daftari la kudumu la wapigakura ikiwa watafanya upendeleo uandikishaji utakapoanza wilayani humo.
 
Onyo hilo lilitolewa jana wilayani hapa na Kamanda wa Taasisi hiyo, Nestory Gatahua, alipokuwa akizungumza na wasimamizi hao kwenye mafunzo ya uadikishaji wa uboreshaji wa daftari la kudumu la wapigakura kwa wasimamizi hao wa Halmashauri ya wilaya ya Masasi mjini hapa.
 
Alisema jukumu hilo ni la serikali, hivyo linapaswa kupewa umuhimu wake katika usimamizi na utekelezaji ili lifanyike kwa hali ya umakini wa hali ya juu na kufikia lengo la uandikishaji.
 
Gatahua alisema Takukuru itafuatilia kwa ukaribu uandikishaji katika kila kituo ili kuangalia mwenendo mzima wa uandikishaji utakapoanza wilayani humo na kwamba hatua kali zitachukuliwa  dhidi ya msimamizi yeyote atakayebainika kwa kosa la kupokea rushwa ama kutumia vibaya fomu za uandikishaji kwa maslahi yake binafsi.
 
“Msimamizi wa kituo anapaswa kutambua umuhimu wa zoezi hili… Taasisi yetu itafuatilia kwa karibu zoezi la uandikishaji kuanzia mwanzo hadi mwisho na iwapo msimamizi atabainika kitendo cha rushwa atawajibishwa kisheria,” alisema Gatahua.   
 
Alisema uandikishaji wa uboreshaji wa daftari la kudumu la wapigakura sio mchakato wa kisiasa, hivyo kama msimamizi yeyote atakuwa na itikadi ya vyama kwa kutoa upendeleo katika uandikishaji kwa kuangalia vyama vya siasa ni kinyume cha sheria, hivyo Takukuru inawajibika kumchukulia hatua msimamizi wa aina hiyo.
 
Kamanda huyo alisisitiza kuwa namba za simu za Taasisi hiyo alizotoa kwa wasimamizi hao wazifanyie kazi na kila msimamizi awe mlinzi wa mwenzake atakapomuona anakwenda kinyume cha kiapo cha utiifu kwa lengo la kuhakikisha jukumu hilo linatekelezwa kikamilifu.
 
Gatahua aliongeza kuwa wasimamizi hao wasitishwe na viongozi wa vyama vya siasa, badala yake wanatakiwa kufuata sheria na kanuni za mafunzo hayo waliyoyapata kutoka kwa wawezesheji hao kwani ulinzi wa kutosha upo, hivyo hawana sababu ya kuharibu kazi waliyopewa.
CHANZO: NIPASHE

0 comments:

 
Supported by Tone Multimedia Company Limited
Copyright © 2012. Mtwara yetu - All Rights Reserved
Designed by Fredy Tony Njeje
Proudly powered by Blogs za Mikoa