Baadhi ya wananchi mkoani Mtwara wameulalamikia uongozi wa
manispaa na wilaya kushindwa kusimamia ujenzi wa barabara kiasi cha
kujengwa chini ya kiwango licha yakutakiwa kujengwa katika viwango vya
kimataifa.
Hali hiyo imekuja baada ya mkandarasi wa Kampuni
ya DB Shaprya anayejenga barabara ya Kunambi inayotoka soko kuu hadi
bandarini kuwa chini ya kiwango, hivyo kuanza kuharibika mapema sambamba
na mifereji kutokupitisha maji.
Ahmad Said mkazi wa Railway, alisema kuwa barabara
hiyo imejengwa kwa viwango hafifu hivyo kushindwa kuelewa viongozi
wanaohusika na utoaji wa tenda za kazi kwani wamekuwa wakitoa zabuni kwa
wakandarasi wenye kazi nyingi hivyo kushindwa kufanya kazi kwa kiwango
kinachotakiwa.
“Tunashindwa kuelewa viongozi wanaohusika na
utoaji wa tenda tulishangaa sana kuona kokoto zikimwagwa na makarai
badala ya magari kutokana na ukosefu wa vitendea kazi na haya ndiyo
matokeo yake barabara zinakuwa chini ya kiwango na zinazotumika ni pesa
zetu,” alisema Said.
Akizungumzia hali hiyo, Mwenyekiti wa Serikali za
Mtaa wa Serengeti, Zuhura Majdi alisema kuwa hali hiyo waliiona lakini
hakuwa na uwezo wa kuizungumzia na kwamba baada ya kuapishwa tatizo hilo
atalifikisha kwenye kata kuona ni kwa namna gani barabara inatengenezwa
kwa kiwango kinachostahili.
“Hili tatizo tuliliona na baada ya mvua kunyesha
ndiyo barabara inazidi kufumuka hivyo kwa kuwa tayari nimeapishwa
nitalibeba kwenda kata ili lifuatiliwe kuona nini kinafanyika kwa sababu
kama hivi mvua zimeanza kunyesha tayari sehemu zilizo karibu na
mifereji tayari zimefumuka,” alisema Majdi. Kwa upande wake, Meya wa
Manispaa hiyo, Suleiman Mtalika alipotafutwa juu ya hilo alitaka
atafutwe mkuu wa wilaya.
Chanzo:Mwananchi
Chanzo:Mwananchi
Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399.
0 comments:
Post a Comment