Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399.
WAZIRI wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo, amewataka
Watanzania kujiandaa na uchumi wa gesi kwani mradi huo utakapokamilika
utaleta mageuzi makubwa nchini.
Kauli hiyo aliitoa mwishoni mwa wiki mkoani hapa, katika ziara yake
ya siku moja aliyoambatana na Balozi wa China nchini, Lu Youqing,
kutembelea na kukagua nyumba za wafanyakazi watakaofanya kazi kiwanda
cha kuchakata gesi kilichopo Kijiji cha Madimba pamoja na ukaguzi wa
mradi wa ujenzi wa bomba la gesi.
Profesa Muhongo alisema mradi huo unakwenda kama ulivyopangwa na
utakapokamilika, nchi itaingia kwenye uchumi wa gesi ambao utaondoa
umaskini nchini.
“Huu mradi utakapokamilika ndio utaleta mageuzi makubwa ya uchumi
nchini kwetu na tutaingia kwenye uchumi wa gesi, kwa sababu gesi ina
matumizi mengi na itatuhakikishia kupata umeme wa uhakika ambao ni
muhimu kwetu kwa ukuaji wa uchumi,” alisema.
Aliongeza kuwa lengo ifikapo mwaka 2025, Tanzania isiwe nchi masikini bali ya kipato cha kati.
“Kitakachotuwezesha kufika hapo ni huu mradi tunaojenga wa bomba la
gesi, kwa hiyo ndugu zangu wa Lindi, Mtwara, Pwani na Tanzania kwa
ujumla, tujitayarishe kwenye uchumi wa gesi tukiwa tumetulizana kabisa
kwa amani na kuaminiana,” alisema.
Katika ziara hiyo, Tanzania Daima ilikutana na kilio cha
muda mrefu cha malipo duni kutoka kwa baadhi ya vibarua wanaofanya kazi
mbalimbali katika kiwanda hicho cha kuchakata gesi asilia katika kijiji
cha Madima.
Wakizungumza kwa sharti la kuhifadhiwa majina yao, walisema kuwa
kiwango wanacholipwa ni kidogo kwa siku, ambacho ni sh 10,000 tofauti
na Wachina wanaopata sh 50,000.
“Tunafanya kazi ngumu sana kuanzia saa 12 asubuhi mpaka 12 jioni,
hatuna sikukuu wala Jumapili, lakini tunalipwa sh 10,000 kwa siku na
hiyo fedha unayolipwa kwa siku tunajitegemea kila kitu, ila Wachina
wanalipwa sh 50,000.
“Wakati sisi ndio tunafanya kazi ngumu, wao kazi yao ni kutusimamia
na kutuelekeza tu, lakini wanalipwa kiwango kikubwa, chakula wanaletewa
na maji safi ya kunywa ya kwenye chupa, ila sisi chakula
tunajitegemea, maji ya kunywa ni ya bomba tunawekewa kwenye matanki
ndio tunakunywa,” alisema mmoja wa vibarua hao.
Chanzo:Tanzania Daima
0 comments:
Post a Comment