Home » » Mgomo wa wafungwa watikisa Maregeza

Mgomo wa wafungwa watikisa Maregeza

Tishio la mgomo wa wafungwa 17 waliohukumiwa kifo na wa vifungo vya kati ya miaka mitano hadi 30 katika Gereza Kuu la Lilungu lililopo mkoani Mtwara, limelitikisa Jeshi la Magereza nchini na kuchukua hatua haraka kushughulikia malalamiko yao.
Aidha, wafungwa hao walikataa kuvichukua baadhi ya vitu vilivyopelekwa gerezani hapo na Mkuu wa Magereza Mkoa wa Mtwara, Mussa Kaswaka, wakidai ametumia fedha zake binafsi kuvinunua badala ya fedha za serikali.

Wafungwa hao walikuwa wakilalamikia kupewa chakula kibaya pamoja na kutumikishwa katika mashamba ya mkuu wa gereza hilo kinyume cha sheria.

Kutokana na hali hiyo, wafungwa hao walitangaza kuanza mgomo juzi ikiwa ni hatua ya kushinikiza uongozi wa gereza kuwatendea haki kama binadamu wengine kwa kuwapatia chakula kizuri.

Msemaji wa Jeshi la Magereza, George Muampashi, akizungumza na NIPASHE jana katika makao makuu ya jeshi hilo, jijini Dar es Salaam, alisema malalamiko ya wafungwa hao yamefanyiwa kazi kwa kuwapelelekea chakula.

Muampashi ambaye alitoa majibu hayo kwa mwanadishi baada ya kuwasiliana na Mkuu wa Magereza Mkoa wa Mtwara (RPO), Mussa Kaswaka, alisema wafungwa hao wamepelekewa maharage, sukari na redio kwa ajili ya kusikiliza.

Alisema kupelekwa kwa vyakula hivyo ambavyo ni moja ya mahitaji ya wafungwa hao kumefuatia uongozi wa juu wa jeshi hilo kumtuma RPO kwenda kuangalia hali ilivyo na kuzungumza na wafungwa hao.

Hata hivyo, taarifa ambazo NIPASHE ilizipata awali zilieleza kuwa Februari 6, mwaka huu baada ya gazeti hili kuripoti mpango wa wafungwa kugoma, Mkuu wa Magereza Mkoa wa Mtwara alifika katika gereza hilo akiwa amefuatana na Mkuu wa Gereza, Mohamed Nampenekela, ASP Magwiza, Inspekta Mnivato na Sajini Wadu.

Uchunguzi umebaini kuwa Mkuu huyo wa magereza alizungumza na wafungwa hao na kuwaeleza kuwa madai yao yote yapo ndani ya uwezo wa gereza.

Hata hivyo, mkuu wa gereza hilo, Nampenekela, alimweleza Mkuu wa Magereza Mkoa wa Mtwara kuwa hilo linawezekana, lakini haliwezi kuwa endelevu.

Maelezo hayo ya mkuu wa gereza yaliwatibua wafungwa hao ambao walisema wangeanza mgomo siku hiyo hiyo Februari 6 na kulalamika kuwa wanashangaa ni kwanini matatizo ya masuala ya chakula yapo katika gereza lao tu.

Taarifa zinaeleza kuwa baadaye mchana siku hiyo hiyo, Mkuu wa Magereza Mkoa wa Mtwara  alirejea katika gereza hilo kwa mara ya pili akiwa na ASP Kapinga, Asp Magwiza, Inspekta Mvinato na Ofisa Usalama wa gereza.

Mkuu huyo wa Magereza alifika katika gereza hilo na kuwapeleka wafungwa hao luninga (TV)  ya nchi 18, dawa za meno boksi tisa, mafuta ya kupaka boksi tisa, karanga kilo tano, maziwa ya NIDO ya gramu 900 makopo matano, sukari kilo tano na vyandarua tisa.

Hata hivyo, wafungwa hao walikubali kupkea vyandarua, TV na dawa za meno, lakini karanga, maziwa, sukari na mafuta ya kupaka walikataa kuvichukua wakidai kuwa alikuwa amevinunua kwa fedha zake.

Uchunguzi uliofanywa na NIPASHE awali ulibaini kuwa wafugwa hao wamekuwa wakilalamika kupewa chakula kibaya kwa miezi sita sasa tangu mwaka jana, lakini kila wanapomweleza Mkuu wa gereza anatoa sababu kuwa hajapewa fedha kutoka makao makuu.

Wafungwa hao walikuwa wanalalamika kuwa wanalishwa uji wa chumvi, ugali na kunde ambazo hazijaungwa kila siku wakati wanastahili kupewa uji wenye sukari, nyama, maziwa, matunda na mbogamboga kama ratiba ya chakula ya gereza hilo inavyoonyesha.

Aidha, wafungwa hao walikuwa wanalalamika kutumikishwa katika shamba la Mkuu wa gereza hilo, Mwamupenekela, lililopo eneo la Mikindani Mtwara na kusimamiwa na askari wawili wa Magereza, majina kwa sasa tunayasitiri.

Uchunguzi wa NIPASHE umegundua kuwa wafungwa hao na namba zao kwenye mabano ni Omar Mussa (104/2011), Said Ali Majije (93/ 201, Maulid Bakir (90/2003), Edward Robart Moringe (304/2008), Hussein Said Mtarela (93/ 2011) na Mustafa Maulid Rashid (140/2012).Wengine ni Bakari Bakari Ismail (89/2013),Abdul Alli Kura (303/2008), Juma Said Chamiunga (120/2013). Wote walihukumiwa adhabu ya kifo.

Waliohukumiwa vifungo vya kati ya mwaka mmoja hadi miaka 30 ni Rashid Mpungo (245/2010), Charles Ndandula (242/2009), Moses Mntigwa (590/2013), Hamis Jonad Nalieni (195/2012), Omar Mohamed Kungunu (191/2010), Omar Said Nambecha (5/2010), Seleman Khalfani (707/2013) na Abdul Ramadhani a.k.a Makaburi (128/2013).
 
CHANZO: NIPASHE

0 comments:

 
Supported by Tone Multimedia Company Limited
Copyright © 2012. Mtwara yetu - All Rights Reserved
Designed by Fredy Tony Njeje
Proudly powered by Blogs za Mikoa