HI,
mambo vipi mdau, tumshukuru Mungu kwa kuwa bado tunaishi, kuna
waliopenda kuwa hai leo lakini hawapo, wamekwenda, wametangulia,
wameimaliza safari yao, tutafuata, wapumzike kwa amani. Shida na raha ni
sehemu ya maisha yetu, tuombeane heri tufanikiwe katika yote
tuliyopanga kuyafanya mwaka huu 2014, tuyafurahie maisha leo lakini
tujenge msingi bora kwa ajili ya kesho.
Nafurahi
kwa sababu tunawasiliana na tunapeana moyo kwa lugha yetu ya Kiswahili,
nafahamu kwamba kuwa Watanzania wanaojisikia fahari kujionesha kuwa
wanafahamu zaidi Kiingereza au lugha nyingine za nje kuliko lugha ya
taifa lao, wanajidhalilisha, na wamekubali kuwa watumwa!
Ni
watumwa kwa sababu fikra zao bado zimefungwa kwa minyonyoro ya ukoloni
wa fikra kiasi cha kusababisha waone kuwa hata lugha ya taifa lao si ya
maana na pia haifai hata kufundishia shule za msingi.
Inasikitisha
sana kumsikia Mtanzania anaunga mkono eti masomo yote shule za msingi
yafundishwe kwa Kiingereza. Kuna sababu zipi za msingi kufundisha masomo
yote shule ya msingi kwa lugha ya kigeni?
Kwa
nini tunaidharau lugha yetu ya Taifa? Hivi leo ukienda Japan,
Uingereza, China, Russia, Hispania, Ujerumani, Ureno wanatumia Kiswahili
kufundishia kwenye shule zao? Jibu ni rahisi tu, hawafanyi hivyo, na ni
kwa sababu wanathamini lugha zao, ni kipaumbele cha kwanza ndipo
nyingine zifuate. Lugha ni utambulisho wa wapi unatoka, ni bidhaa na
nyenzo muhimu katika mahusiano yetu na mataifa mengine, iweje leo
tukithamini Kiingereza kuliko lugha ya Taifa letu?
Utajitambulisha
wewe ni Mtanzania kwa kuzungumza Kiingereza? Utasemaje unaipenda
Tanzania wakati unakidharau Kiswahili? Unafiki! Yaani wakati watu
wanafikiria uwezekano wa kutumia Kiswahili kufundishia vyuo vikuu leo
kuna Watanzania wanapayuka kuunga mkono fikra za kinyonge na zisizo na
mashiko yoyote?
Kuthamini
lugha za nje kuliko Kiswahili ni utumwa wa kifikra, na si kweli na
kamwe haitakuwa hivyo, kwamba, eti usomi ni kufahamu zaidi Kiingereza.
Kuna Watanzania wanasema wanaipenda kwa moyo wote, lakini kwa matendo
yao ni wanafiki.
Kufahamu
Kiingereza si kigezo pekee cha kukufanya uwe msomi mzuri, na si wote
wanaofahamu lugha hiyo wanaweza kujenga hoja na kuzitetea, au wanaweza
kutetea maslahi ya jamii wanayotoka au nchi, tukatae kutawaliwa na
kujidhalilisha, tuache kuishi kwa mazoea, tuthamini vya kwetu zikiwemo
lugha zetu kwa sababu ni kielelezo cha utamaduni wetu.
Unaposema
upo huru zitathimini fikra zako, unahitaji fikra huru, huwezi
kuizungumzia Tanzania na usiitaje lugha ya Kiswahili kwa sababu ndiyo
lugha ya Taifa hili, na huwezi kumzungumzia Mtanzania na ukaacha kuitaja
lugha hiyo kwa sababu ndiyo lugha ya nchi yake, kama wewe unakithamini
Kiingereza kuliko Kiswahili, wewe ni mnafiki, uzalendo wako ni wa
mashaka na unajidhalilisha.
Chanzo;Habari leo
0 comments:
Post a Comment