KITUO cha Uwekezaji nchini (TIC) kimesema kitaendelea kushirikiana na
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Mtwara, ili kuendelea kuhamasisha na kuvutia
wawekezaji wa ndani na nje ya nchi katika mkoa huo wenye fursa nyingi.
Mkurugenzi Mtendaji wa kituo hicho, Juliet Kairuki, alieleza hayo
waandishi wa habari wakati wa ziara yake mkoani hapa mwishoni mwa wiki,
kwamba ni katika kuimarisha mahusiano hayo ya kikazi kati ya pande hizo
mbili maendeleo yatakapopatikana.
Katika ziara hiyo, mkurugenzi huyo alikutana na Mkuu wa Mkoa wa
Mtwara, Kanali mstaafu, Joseph Simbakalia na maofisa wengine na pia
kujionea shughuli za uwekezaji zinazoendelea kufanyika.
“Mazungumzo yetu yamekuwa ya manufaa, panahitajika ushirikiano mkubwa
kati yetu ili kuzidi kukuza uwekezaji katika mkoa huu,” alisema.
Alisema mazingira hayo ya ushirikiano yakizidi kujengwa, yatasaidia
shughuli za kukuza uwekezaji na kufikia malengo yanayohitajika.
Kairuki alisema panahitajika kuwajengea uwezo maofisa wa Ofisi ya
Mkuu wa Mkoa, ili nao washiriki kikamilifu katika kufikia malengo ya
uwekezaji.
Alisema pia ofisi yake itaendelea kushirikiana na taasisi nyingine za
serikali na sekta binafsi, ili lengo katika mkoa huo litimie.
Alifafanua mkoa huo una fursa nyingi za uwekezaji zikiwemo za utalii,
uzalishaji kwenye viwanda na biashara na kuwa muhimu ardhi iandaliwe
kwa ajili ya wawekezaji wanaoenda kuwekeza.
Alisema bandari nzuri mkoani hapa na pia maeneo yaliyotengwa na
serikali kwa ajili ya uwekezaji ni moja ya sababu kubwa zinazovutia
wawekezaji katika sekta mbalimbali.
“Serikali ikiendelea kutenga maeneo kama hayo itasaidia sana katika
uwekezaji,” alisema Kairuki na kuongeza kituo chake kwa sasa kinaandaa
hati za ardhi na kuweka miundombinu ya msingi katika maeneo hayo, ili
kurahisisha na kuvutia wawezekezaji zaidi.
Alisema kufanikisha kwa jambo hilo kunategemea zaidi ushirikiano na
taasisi nyingine za serikali ili kutatua tatizo la ardhi ambalo wakati
mwingine linakuwa ni kikwazo kikubwa katika uwekezaji.
Katika ziara hiyo, alitoa ripoti ya hali ya uwekezaji kwa mkuu wa
mkoa ili aweze kuwa na ufahamu wa wawekezaji wanaokuja kuwekeza katika
mkoa wake, hasa wale waliopitia katika kituo chake na kujisajili.
Sambamba na hilo, pia alikagua hati za ardhi zinazotolewa na kituo
chake kwa wawekezaji waliowekeza mkoani hapa kwenye miradi mbalimbali.
Alisema alifanya hivyo sababu wawekezaji wengine hawafuati sheria
sawasawa na hawatoi ripoti zao, hivyo kituo chake hakiwezi kufahamu
wanaendelea vipi bila ya kutembelea miradi hiyo na aliahidi kuendelea
kufanya hivyo
Chanzo;Tanzania Daima
0 comments:
Post a Comment