RAIS JAKAYA KIWETE.PICHA YA MAKTABA KATIKA VURUGU ZA MTWARA ZILIZTOKEA HIVI KARIBUNI.
RAIS Jakaya Kiwete amesema serikali
itawakamata wanasiasa wanaochochea vurugu mkoani Mtwara kwa kisingizio
cha kuzuia gesi isitoke mkoani humo.
Rais alitoa kauli hiyo jana wakati
akizungumzia vurugu kubwa zilizotokea Mtwara jana wakati akihutubia
wananchi kwenye uzinduzi wa ujenzi wa barabara ya Dodoma - Iringa eneo
la Bahiroad. Barabara hiyo ya kilomita 70 ni kutoka Dodoma mpaka Fufu.
Asubuhi alizindua Iringa-Mgole. Alisema
kwamba gesi ya Mtwara ni rasilimali ya taifa na hakuna mtu anayeweza
kusema kwamba ni mali yake.
“Tukisema zabibu ni ya Dodoma au kahawa
ni ya Kilimanjaro tutakuwa tunatengeneza maajabu ya Mtwara… hatukubali…
nchi hii ni moja na rasilimali zitumike kwa watu wote,” alisema Rais
Kikwete.
Aidha alisema madai yanayotolewa na
wachochea vurugu kuhusu rasilimali hiyo ya gesi hayakubaliki na hayana
nafasi katika taifa la Tanzania. Rais alisisitiza katika hotuba yake
kwamba rasilimali za nchi ni mali ya watu wote na watu wacha
“Tutawakamata wanasiasa wote
wanaochochea vurugu bila kujali mapembe yao.” Alisema Rais Kikwete na
kuongeza kuwa Mtwara haijasahaulika katika matumizi ya rasilimali hiyo
ya taifa. Alisema kuna mipango ya kutumia gesi kujenga viwanda vya
mbolea na kutumia umeme kuunganisha gridi ya taifa kama ilivyo katika
gesi ya Songosongo.
Alisema fujo za awali zilipoibuka kwa
kisingizio cha kutotaka gesi itoke, Waziri Mkuu Mizengo Pinda alikwenda
mkoani humo na wakaelezana, na alidhani kwamba walikuwa wameelewana
lakini kumbe watu wenye chokochoko waliketi wakapanga mbinu wakisubiri
bajeti ikisomwa waingie mtaani na kufanya fujo.
Alisisitiza kwamba taifa halitakubali
kuacha kundi la watu wachache kuvuruga amani na kuwa serikali
itawakamata wao na viongozi wao na kuwafikisha mahakamani.
Hali ilivyo Mtwara Wakati Rais Kikwete
anatoa msimamo wake kuhusu ghasia hizo na hatua ambazo serikali yake
itachukua, imeripotiwa kwamba watu kadhaa wakiwemo askari polisi
wamekufa, huku nyumba, magari kuteketezwa na madaraja kubomolewa.
Hali hiyo tete iliyoukumba mji na hata
baadhi ya vijiji vya mkoa huo, ilisababisha pia Bunge kuahirisha kikao
chake cha jioni. Bunge jana jioni lilikuwa liendelee na mjadala wa
Bajeti ya Wizara ya Nishati na Madini iliyosomwa jana asubuhi.
Imedaiwa kwamba kiini cha vurugu hizo ni
uchochezi unaoendeshwa kuupinga mpango wa Serikali wa kujenga bomba la
gesi kutoka Mtwara kuja Dar es Salaam. Licha ya ujumbe wa Polisi Makao
Makuu kwenda mkoani humo jana, Serikali inatarajiwa leo kutoa tamko
bungeni, ikiwa ni pamoja na kuelezea hali halisi ya tukio hilo.
Waandishi wa habari Miongoni mwa
walioathirika na vurugu hizo ni Chama Cha Mapinduzi (CCM) ambacho
majengo yake sambamba na nyumba za viongozi wake wakiwemo madiwani
zimechomwa.
Vile vile baadhi ya waandishi wa vyombo
vya habari vya serikali na chama, wameathirika na vurugu hizo akiwemo
Mwakilishi wa Televisheni ya Taifa (TBC), Kassim Mikongoro ambaye nyumba
yake imechomwa.
Mwandishi wa gazeti hili, Hassan Simba
na wa gazeti la Uhuru, pia walilazimika kukimbia nyumba zao baada ya
kupewa taarifa kwamba kundi la wafanya vurugu walikuwa wakienda kuchoma
nyumba zao.
Taarifa kutoka mkoani humo, zinasema
kundi hilo lililokuwa likifanya vurugu, lilikuwa na silaha mbalimbali
ikiwemo mabomu yanayotumika kuvulia samaki na wengine wanadaiwa kwamba
walikuwa na magobori.
Katika eneo la Mikindani, ofisi zote za
serikali zilivamiwa na kuchomwa moto. Aidha Daraja la Mikindani
linatajwa kuwa limevunjwa kiasi kwamba ilikuwa vigumu kuingia wala
kutoka mjini Mtwara. Kundi hilo la watu liliendelea hadi eneo la
Shangani kwenye nyumba za viongozi.
Nyumba ya kupumzikia wageni inayoitwa
Shengena Lodge ilichomwa moto kwa kile kinachoelezwa kwamba iliwapokea
askari Polisi. Inadaiwa mmoja wa askari alichomwa mshale na watu hao.
Askari walifanya msako wa nyumba hadi
nyumba maeneo ya Magomeni na Mangowela. Katika maeneo mbalimbali ya mji,
milio ya risasi na mabomu ilitawala.
Matairi kila kona ya mji yalichomwa
barabarani huku polisi na zimamoto wakifanya kazi ya kuzima huku
ving’ora vikilia.
Vurugu hizo ziliathiri pia watoto shuleni ambao
walifungiwa huku walimu wakikimbia. Hakuna shughuli zozote zilizokuwa
zikifanyika zaidi ya watu kujifungia majumbani kwa hofu.
Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Mtwara,
Linus Sinzumwa hakupatikana mara moja kuelezea hali halisi ya vurugu
hizo kutokana na hali ilivyokuwa tete.
“Kuna wananchi eneo la Mdenga
wameonekana wakiwa na magobori. Baada ya kuvunja daraja la Mikindani,
walianza kuelekea Kijiji cha Mpapu kwa lengo la kubomoa daraja lingine,”
alisema mmoja wa watu walioshuhudia.
Baadhi ya watu waliozungumza na gazeti
hili, wamesema vurugu hizo ambazo zinadaiwa kufanywa na watu wanaopinga
gesi kusafirishwa kutoka mkoani Mtwara, zinapaswa zichunguzwe kwa kina
kubaini watu walio nyuma ya waandamanaji hao.
“Hapa utawaonea Polisi. Hizi ni vurugu
za kisiasa ambazo haziwezi kumalizwa na nguvu ya dola. Wanasiasa wenyewe
ndiyo wanapaswa kuzimaliza…wananchi hawawezi kujiunga bila kuwa na watu
nyuma yao,” alisema mmoja wa watu ambaye hakutaka jina lake litajwe.
Mmoja wa askari kutoka mkoani Mtwara
ambaye pia hakutaka jina lake liandikwe gazetini, alisema “wanasiasa
wanapaswa wabebe jukumu...unaweza ukalaumu polisi, lakini kama inaamua
kufanya kazi ipasavyo, hawa hawa wanasiasa ndiyo hao hao utawaona
wakiandamana kudai haki za binadamu.”
DCI atua Kwa mujibu wa tarifa kutoka
Makao Makuu ya Polisi, Kaimu Mkurugenzi wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai
(DCI), Issaya Mngulu ilimlazimu jana kwenda mkoani humo kwa ajili ya
kudhibiti vurugu hizo zilizodumu kwa zaidi ya saa sita.
Bunge laahirishwa Wakati hayo
yakiripotiwa kutokea Mtwara, kikao cha Bunge kilichotarajiwa kuendelea
jana jioni mjini Dodoma ili kujadili hotuba hiyo ya bajeti ya Wizara ya
Nishati na Madini kiliahirishwa na Spika wa Bunge Anne Makinda.
Mara baada ya kuingia kwenye ukumbi wa
Bunge, Spika wa Makinda aliwatangazia wabunge kwamba kikao hicho
kisingeweza kufanyika kutokana na vurugu zilizotokea mkoani Mtwara.
“Waheshimiwa wabunge hotuba hii ya
wizara ya nishati na madini ilipaswa kujadiliwa kwa siku mbili lakini
hata kabla ya nusu siku kufika, tulipata taarifa kwamba kungetokea
machafuko Mtwara.
Hivyo basi, naiagiza Serikali kulifuatilia suala hili
ili kesho itoe taarifa rasmi ya hali halisi ilivyo na muda huu, kamati
ya uongozi ya Bunge itakutana ili kujadili suala hilo, hivyo naahirisha
kikao hiki cha bunge hadi saa tatu asubuhi kesho.”
Magari yakwama Lindi Abiria zaidi ya 455
wamekwama katika kituo cha mabasi mjini Lindi mkoani humo kutokana na
vurugu hizo za Mtwara anaripoti Keneddy Kisula.
Dereva wa basi la abiria la Maning Nice
linalofanya safari zake kati ya Dar es Salaam, Lindi na Mtwara, Rashid
Ahmad alisema kwamba kuna wasi wasi wa usalama wa abiria, mali zao na
magari yao kuharibiwa.
Taarifa zilizopatikana mjini Lindi,
zilisema magari kadhaa yalichomwa moto. Inadaiwa katika Kijiji cha
Madangwa, gari ndogo aina ya Suzuki Vitara liliunguzwa kwa moto.
Licha ya wenye magari kugoma kuondoka
Lindi kwenda Mtwara, pia abiria waliridhia na kuamua kubaki mjini hapa
hadi wahakikishe usalama umeimarika.
Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Lindi,
George Mwakajinga alisema jeshi hilo liko tayari kuwasindikiza mpaka
mwisho wa safari yao. Alisema kwamba serikali iko tayari kutoa msaada wa
ulinzi kwa mabasi hayo yenye abiria yapatayo saba yaliyokwama.
Mabasi
hayo ni Maning Nice, Shilingi, Hamanju, No Rise, Buti la Zungu, Ng’itu
na Machinga.
HABARILEO.
0 comments:
Post a Comment