Home » » Kampuni ya ndege ya ATCL yarejesha safari za Mtwara

Kampuni ya ndege ya ATCL yarejesha safari za Mtwara



Na Mwandishi Wetu



………………………………………….


SHIRIKA la Ndege la Air Tanzania
(ATCL) litaanza tena safari zake kati ya Dar es Salaam na Mtwara,
kuanzia  Ijumaa tarehe 8 February 2013.



Akizungumza na waandishi wa habari
jijini Dar es Salaam jana, Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa ATCL, Kapteni
Milton Lazaro alisema kuwa shirika lake litatumia ndege aina ya Dash
8-300 ambayo inauwezo wa kubeba abiria 50.



“Sasa tumejipanga upya kurejesha
safari zetu kati ya  Dar es Salaam na Mtwara ambazo zinatarajiwa kuanza
Ijumaa, tarehe 8 mwezi huu wa Februari 2013. Urejeshwaji wa safari za
kwenda Mtwara, ni sehemu ya utekelezaji wa mpango wetu wa kuongeza
safari za kuenda mikoa mbali mbali ambayo tulikuwa hatuendi kwa sasa,”
alisema.



Kapteni Lazaro alibainisha kuwa
ratiba inaonyesha kuwa ATCL itaruka kwenda Mtwara katika siku za
Jumatatu, Jumatano, Ijumaa na Jumapili na kuongeza kuwa marekebisho ya
ratiba yataendelea kufanywa kulingana na mahitaji ya wateja. Alisema kuwa shirika lake litatoza nauli kuanzia shilingi 199,000 kwa tiketi ya kwenda na kurudi.  




“Abiria katika njia hii
watahitajika kulipia kuanzia shilingi laki moja na tisini na tisa elfu
kwa tiketi ya kwenda na kurudi. Abiria wanaweza kupiga simu namba
0782737730 ili wapate nafasi za usafiri. Vile vile abiria anaweza kupiga
simu kwa mawakala walio karibu yao,” alisema. 


Urejeshwaji wa safari za Mtwara
unakuja mwezi mmoja baada ya shirika hilo kurejesha safari za Kigoma
baada ya kumalizika kwa ukarabati wa uwanja wa Kigoma. 
“Napenda niwahakikishie abiria wetu  kuwa tutaendelea kutoa huduma bora kuliko zote kwa bei nafuu” alisema.



Aidha, Kapteni Lazaro alisema kuwa
shirika la ATCL lina mpango wa kuongeza ndege zaidi kabla ya mwishoni
mwa mwaka huu, na kubainisha kwamba wanategemea kuchukua ndege ambazo ni
kubwa zaidi na za kisasa zaidi.

0 comments:

 
Supported by Tone Multimedia Company Limited
Copyright © 2012. Mtwara yetu - All Rights Reserved
Designed by Fredy Tony Njeje
Proudly powered by Blogs za Mikoa