Siku ya Alhamisi,
Disemba 27, 2012, mkoani Mtwara, lilijiri tukio ombalo, kwa watawala wetu,halikufikirika, halikutegemewa na katu halikutazamiwa. Wananchi wa eneo
hilo waliingia barabarani kudai manufaa ya gesi asilia iliyoko Msimbati, Mtwara
vijijini. kwa mujibu wa wana Mtwara gesi hiyo ilikuwa inasafirishwa Dar es Salaam
bila wao kubainishiwa watakavyonufaika .
Tukio hili lilileta
mshtuko wa volteji kubwa (high voltage shock) serikalini. Mkuu wa Mkoa huo
Kanali Joseph Simbakalile, alikuwa wa mwanzo kutoa kauli. Waandamaji na waratibu
(vyama vya upizani ) walipewa
lebo ya “wahaini na wapuuzi”. Kwa mujibu
wa Kiswahili sanifu, “uhaini ni tendo la
kusaliti nchi yako au / kufanya mipango
ya kupindua serikali halali iliyopo madarakani”. Na upuuzi ni jambo au tendo
lisilo la maana au la kijinga. Naye Waziri
wa Nishati na Madini Profesa Dr. Sospeter Muhongo akajitokeza :
naye akasema madai ya waandamanaji yanataka kuigawa nchi ( Tanzania ) vipande
vipande.
Rasilimali ya nchi ni
kwa manufaa ya nchi; hilo linaeleweka kwa kila mtu.Mifano aliyotoa ya katani
(mkonge)iliyolimwa Morogoro na Tanga kuwa iliwanufaisha watu wa Mtwara ina upogo.
Profesa angejua kuwa mkonge umelimwa Ubena zomozi (Pwani ) na huko kusini kulikuwa
na mashanba Mikindani, Kitunda, Mkwaya,
Ngurumahamba na Kikwetu . Uwanja wa ndege wa Lindi umezungukwa na shamba hilo
la Kikwetu. Kwa nini watu wa Mtwara
hawajasema maduhuli ya korosho yatumiwe huko kusini tu? Kauli za
viongozi wa serikali hazijagusa kiini au msingi wa madai ya watu wa Mtwara.
Watawala wametumia shoka mahali ambapo
ukucha ungestahiki.
“Uhaini na upuuzi” wa
wana Mtwara umesimama katika miguu ya historia. Kimantiki walichosema ni kuambia
serikali yao “mpaka hapa si zaidi” (this farther and no
further). Kuwaelewa watu hao hatuna budi kutalii mazingira
yaliyowasukuma kufanya walivyofanya. Wanakinyongo kilichorundikana kwa muda mrefu.
Hawakuwa bado wamepata mahali pakuegemea na
kuyatoa yaliyokuwa yanawakera na kuwasibu. Walatini wamesema “Veritatis vos liberabit “ ( ukweli
utatuweka huru); hivyo kuibua usuli na
mazingira ya ukweli kutaepusha kuwaelewa watu
hao kwa mtazamo hasi.
Kusini na buti la
Wadachi (Wajerumani)
Vita vya MajiMaji
(1905 – 1907 ) vya kupinga
utawala wa Wajerumani vilianzia
Nandete, wilayani Kilwa, mkoani
Lindi Mashamba ya pamba
yalihujumiwa , na harakati za wazalendo
hao zilienea maeneo yote ya
kusini ya mto Rufiji na kati ya Bahari ya Hindi na Ziwa Nyasa. Kipindi kifupi tu baada ya upinzani dhahiri kuanza askofu Cassian Spiss ( Mswisi – wananchi walimweka katika kundi la Wajerumani) aliuawa
akiwa njiani kuelekea Liwale .
Huko Nyangao ( Lindi) misheni ya Wajerumani ilishambuliwa na wapiganaji. Masista wawili wa Kijerumani waliuawa baada ya
kudhalilishwa na kuteswa na Waafrika.
Mwaka 1902 huko Kitangali (Newala) Mkulungwa (kiongozi ) Mkoto
aliwahamasisha wananchi wasilipe kodi kwa Wadachi. Wale ambao wangelipa
wangepata maradhi ya ndui. Ujumbe ulieleweka na wananchi wakaacha kulipa kodi. Wajerumani wakatuma kikosi maalumu cha askari kutoka
Lindi kumshughulikia kiongozi huyo. Alikamatwa na kunyongwa hadharani .
Kama tulivyosema
upinzani wa Wadachi ulikuwa umeenea sana kusini. Kwenye uwanda wa Makonde wananchi waliwaunga mkono wazalendo wenzao. Mwaka 1907 kikosi cha mamluki kilitumwa toka Lindi ( makao makuu ya
watawala katika sehemu hizo ) kwenda kuuzima uasi
Walipokuwa wanaelekea
kwenye lengo wananchi wakapata habari za ujio huo. Walipokuwa katika kijiji cha
Mtopwa (Newala) walivamiwa na wananchi. Askari wote waliuliwa wakazikwa pamoja .Mahali
hapo pako katikati ya kijiji cha Mtopwa. Tukio hilo lilikoleza hasira, ghadhabu
na ukatili wa Wajerumani.
Askari wengine
walipelekwa kumsaka kiongozi wa Mtopwa
aliyeitwa Mtumba bin Omari. Alikamatwa na kupelekwa Lindi ambako aliteswa na
hatimaye kunyongwa. Kaburi lake liko Lindi mjini sehemu iitwayo Mikumbi.
Hii ni sehemu ya
katalogi ya matukio ambayo yalichefua utawala wa Wajerumani kwa eneo la kusini.
Hivyo wakati sehemu nyingine za nchi zikisonga mbele kidogo huko kusini
waliwekwa kwenye kifukofuko (cocoon0.
Kusini chini ya
Waingereza
Baada ya Wajerumani kuangushwa
duniani pote katika Vita Vikuu vya Kwanza vya Dunia (1914 – 1918), Tanganyika,
iliyokuwa sehemu ya Dutch East Africa (nchi nyingine katika eneo hili zikiwa
Rwanda na Burundi) iliwekwa chini ya utawala wa Waingereza kama wadhamini. Nchi
haikuwa koloni kama ilivyokuwa Kenya, Nyasaland( Malawi) na Northern Rhodesia
(Zambia). Kwa maeneo ya kusini hali ilikuwa kama Wadachi waliwaambia cha
kuwafanyia wenyeji wa kusini. Hakuna kumbukumbu zinazoonyesha kwamba watawala
wapya walikuwa na mipango au azma ya kuendeleza eneo hilo katika fani mbali mbali. Yaliyotokea
yalilenga kunufaisha watawala.
Baada ya vita
Waingereza walikuwa wachovu kiuchumi hali ya huduma za kijamii ziliathirika na
vita. Kampuni iliyoitwa Overseas Food Corporation ilianzisha mradi mkubwa wa
kulima karanga Urambo (Tabora) Kongwa (Dodoma) na Nachingwea (Lindi). Ili
kuhudumia mashamba kwa ufanisi bandari ya Mtwara iliboreshwa. Wakati huo huo wakajenga
reli na bomba la mafuta toka bandarini Mtwara hadi Nachingwea. Reli ilikuwa
ienddelee hadi Mbamba bay pwani ya ziwa Nyasa.
Mnamo mwezi Oktoba
1961 lilifunguliwa tawi la reli la kilomita takribani 40, toka Chilungula hadi
Masasi. Miundombinu na shughuli za kilimo zilitoa ajira na maeneo yaliyopitiwa
na miundo msingi hiyo yalifunguka kwa maendeleo
Kwa sababu mbali mbali
mradi wa karanga Nachingwea ulifungwa. Mwaka mmoja baada ya Tanganyika kupata
Uhuru, sarikali ya Tanganyika huru ikaamini kuwa reli na bomba la mafuta
vilikuwa ni miradi isiyo na tija. (white elephant). Reli na bomba vikang’olewa.
Athari za hatua hiyo ni bayana .Kusini kulizidi kuzama kimaendeleo, taswira
iliyodumu kwa kipindi kirefu. Lakini kwa muda mfupi watawala (Waingereza) walimaizi kwamba eneo la kusini
lilikuwa na utajiri mwingi hivyo wakaita “Cinderella Province” Cinderella ikiwa na maana ya ‘mtu au
kitu ambacho uzuri au uwezo wake haujatambulikana”.
Jingine walilolifanya Waingereza ni kuangusha magogo na kupasua mbao huko Rondo Mnara (Lindi vijijini). Kampuni iliyoitwa Steel Brothers ilifanya kazi hiyo miaka ya 1950. Wakavuna ,
wakachuma na kuondoka . Wananchi
wakaachiwa visiki vya mipingo , mbambakofi,mivule nk. wakati huo huo walikumbatia umasikini.
Kusini baada ya uhuru.
Miaka michache ya kuelekea uhuru kulianzishwa mradi
mkubwa wa maji toka mto Ruvuma ,uliendeshwa
na kampuni ya Makonde Water Corporation.
Ilipangwa maji yaenezwe sehemu mbalimbali
huko kusini. Miaka michache baada ya kuasisiwa kwa vishindo mradi ulikufa. Wananchi hawakuelezwa sababu za mabadiliko hayo. Madhila , taabu na kero za kukosa maji hazikumilithika
.
Katihati ya miaka 1960
kulizuka mgogoro wa kiwanja katika mji mdogo wa Mahuta (wakati huo Newala , sazsa uko katika wilaya
ya Tandahimba ). Mfanyabiashara wa Kiasia
alipora eneo hilo ili ajenge kituo cha mafuta ya nishati. Wananchi wakachachamaa.
Uongozi wa mkoa na wilaya ukaingilia kati. Kwenye mkutano wa hadhara hapo Mahuta , kiongozi wa
wananchi alipigwa viboko kwa sababu za “kupinga hatua za maendeleo “ kama
walivyoita watawala. Kupinga uonevu
kunyanyaswa na kudharauliwa,
wananchi waliandika barua ngazi
za juu za taifa na kudai , moja , mkuu wa mkoa na yule wa wilaya wahamishwe
,mbili, wapendekeze majina ambayo yatatoa mkuu wa mkoa na yule wa wilaya ; na tatu kama maombi hayo
hayatakubalika watajitenga na kujiunga na Msumbiji ili wawe pamoja na FRELIMO
kutafuta ukombozi. Yaliyofuata ni historia.
Miaka mitatu baada ya uhuru wa Tanganyika , wana Msumbiji
kupitia FRELIMO walianzisha vita vya
ukombozi. Kutokana na mazingira ya
kijiografia ( kati ya nchi mbili ) eneo lote la kusini likawa “no go area” –
hapakuwa na shughuli zozote za maana za kimaendeleo zilizokuwa
zikifanyika . FRELIMO
wakafanikiwa kukunja jamvi ukoloni mwaka 1975. Ni dhahiri kwa miaka kumi
wengine walikuwa wamesonga mbele hapa nchini . Mategemeo na matumaini ya wengi
huko kusini ni kuwa serikali ingekuwa na
programu maalum “kufidia muda
uliopotea”. Wakati wa Vita kuu ya Pili vya dunia Yugoslavia ilipambana na
majeshi ya Adolf Hitler . Marshal Josef Tito akawaambia wapiganaji wale “ The wounded should not be left behind “
( majeruhi wasiachwe nyuma). Kimaendeleo
kusini ilijeruhiwa na kuachwa nyuma.
Barabara ya Dar es salaam – Lindi ni “mkunga” wa
matatizo ya kusini. Ahadi za serikali
kuijenga zimechukua kipindi kirefu kutekelezwa. Miaka ya 1970 – 80 kampuni moja ya Kitanzania na taasisi moja ya serikali waliteuliwa
kujenga barabara hiyo. Wakajenga
makambi Nangurukuru
(Kilwa).Hakuna ushahidi wa kazi iliyofanywa – tatizo la barabara likawa “
kichwa cha mwenda wazimu”. Mwaka 1977
wananchi wa kusini, wakiungwa mkono
na wa maeneo mengine, waliasisi mchango
maalum kwa ajili ya ujenzi wa barabara hiyo. Mwitikio wa wito huo
ulikuwa chanya. Ofisini ya Waziri Mkuu ikasitisha zoezi hilo kwa ahadi
kuwa serikali igejenga mradi huo. Imechukua miongo kadhaa kukamilika kazi hiyo.
Miaka ya 1960 – 70
wananchi wa kusini walihamasishwa kulima korosho kwa ajili ya
biashara. Matokeo yalikuwa ya kutia moyo. Mapori yalipisha mashamba ya mikorosho. Zao
likachangia umasikini. - Pembejeo bei juu na soko likawa halina
uhakika .
Kuna viwanda vya kubangua
korosho Masasi , Newala Lindi na
Mtwara lakini hakuna msimamo maalum wa Bodi ya Korosho na wanasiasa wa
kuuza nje zao lililoongezewa thamani. Bado wanakumbatia fikra hafidhina
zilizopitwa na wakati wa kuuza nje ya nchi korosho ambazo hazijabanguliwa.
Alama za nyakati na
Baba Kundambanda.
Walioandamana huko Mtwara
walikuwa wanadai haki waliyoikosa kwa
miaka mingi. Kilichoonekana
kama uhaini na upuuzi ni mbegu ya tunda ya mti wa ahadi zisizotekelezwa. Kwa wachunguzi wa mambo dalili zilianza
kujitokeza mapema mwaka 2012. Msanii mmoja wa huko kusini alitoa nyimbo zinazochambua
uadilifu wa polisi, EPA, sera nzuri za
Mwalimu Nyerere na wanasiasa wa
maeneo ya kusini wanavyo waona wananchi
kuwa ni mazuzu . Nyimba za msanii huyo, Baba kundambanda, anaimba kwa
lafudhi ya Kimakonde, moja ya lugha za
kusini na pia huingiza maneno ya lugha
hiyo kwa mfano anasema viongozi /
wanasiasa huwaambia wananchi kuwa koromeo
lilkipanda na kushuka maelezo yake ni
kuwa shetani anatwanga mtama ( Nandenga atwangi ntama pang’ulo ) . lakini
wananchi kwa kuwa si “ mavelu “ (mazuzu, wajinga ) hujibu “ kulambila” ( huo ni uongo ). Wimbo huu
una umarufu mkubwa na jijini Dar es salaam huchezwa na baadhi ya vituo vya
redio.
Nani hamwelewi nani ?
Maelezo ya Waziri Muhongo
kupitia vyombo vya habari hayajibu hoja ya msingi ya madai anayoyapuuza.
Yakichambuliwa kwa uyakinifu na mantiki ni kama kuhamisha magoli ili mabao
yasiingie kimiani. Takwimu anazotoa zipo
kando ya madai ya wananchi – tutanufaikaje? Kama ni zile ahadi za “yatakayofanywa
baadaye” ndiyo yanayewapa watu hao
nguvu ya
kutamka “ mpaka hapa si zaidi”
kwa sababu wamepitia mengi ya ahadi zisizotelekezwa. Msamiati wa vitisho hautapunguza ari ya wananchi kutoa maoni na madai.
Makala inahitimishwa kwa aina mbili za semi ambazo ni maarufu sana katika eneo hilo la nchi. Watu wakipeana
mikono kisha mkono mmoja ukaacha viganja na kuelekeza kwapani mtu huyo
ana lake jambo. Anayedai kuendelezwa hawi haini au mpuuzi – mkono unaelekea
kwapani. Mahusiano ya ukwe ni ya heshima kubwa sana katika jamii za Watanzania:
- usemi wa pili -kijana wa kiume alikuwa anavuka kijito kwa miguu na
mama mkwe: mama mkwe alikuda ili nguo zake zisirowe na kwa kufanya hivyo mapaja
yake yakaonekana. Katika usemi huu badala ya kijana weka neno wana Mtwara na
mama mkwe weka “viongozi wa serikali/ wanasiasa”. Nani kaonesha kisichostahiki?
Ronald M Munga
0 comments:
Post a Comment