Home » » Mtwara watishia gesi kugeuka maji

Mtwara watishia gesi kugeuka maji







MUUNGANO wa vyama vya upinzani mkoani Mtwara, umepinga gesi asilia kwenda Dar es Salaam na kuwahimiza wananchi wa kusini hususani mikoa ya Lindi na Mtwara kuungana kupinga suala hilo.
Vyama vilivyoungana kupinga gesi asilia isiondolewe Mtwara, ni NCCR-Mageuzi, Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), UDP, TLP, ADC, APPT, SAU na DP.
Vyama hivyo vinafanya mikutano katika maeneo mbalimbali ili kuwaomba wananchi waungane nao kupinga gesi hiyo kuondoka kabla ya Wanamtwara hawajafaidika.
Makamu Mwenyekiti wa muungano huo, Uledi Abdallah, aliyasema hayo juzi kwenye mkutano wa hadhara uliofanywa katika Kata ya Madimba na Msimbati mkoani hapa.
“WanaMtwara lazima tuungane kwa pamoja gesi yetu isiondoke Mtwara, tusiogope na wala tusirudi nyuma tutetee haki yetu, kwani gesi ni mali yetu WanaMtwara…tuache mambo ya woga tusimame imara kutetea rasilimali yetu,” alisema Uledi ambaye pia ni Mwenyekiti wa NCCR -Mageuzi Jimbo la Mtwara Mjini.
Kwa upande wake, Mkuu wa Kaya ya Msimbati, Somoe Issa, alipinga gesi hiyo kupelekwa Dar es Salaam na kuongeza kuwa endapo wataendelea kung’ang’ania itageuka maji kwenye mabomba watakayotumia kusafirishia.
Alisema mara ya kwanza walipochimba gesi walishindwa kuendelea kutokana na mitambo kunasa kwenye shimo na kila walipojaribu kuitoa ilishindikana ndipo walipoenda kuwachukua mafundi kutoka Canada ambao nao walishindwa.
“Sasa kama mimi ndio niliowasaidia kunasua mitambo yao na wakaendelea na kazi zao ya uchimbaji wa gesi, basi nawaomba mimi kama mkuu wa kaya waachane mara moja na wazo la kuondoa gesi asilia Mtwara,” alisema.
Naye mkazi wa Msimbati, Juma Hassani, alisema kitendo cha serikali kutaka kuiondoa gesi hiyo si kitendo kizuri, kwani ni rasilimali pekee wanayoitegemea.
chanzo:daima

0 comments:

 
Supported by Tone Multimedia Company Limited
Copyright © 2012. Mtwara yetu - All Rights Reserved
Designed by Fredy Tony Njeje
Proudly powered by Blogs za Mikoa