Home » » NDEGE ZASITISHA SAFARI MTWARA KWA UBOVU WA UWANJA

NDEGE ZASITISHA SAFARI MTWARA KWA UBOVU WA UWANJA

Na Mwandishi wetu

Usafiri wa ndege kwa Mkoa wa Mtwara huenda ukawa kitendawili  kutokana na kile kinachodaiwa kuwepo kwa ubovu wa barabara ya kutua na kuruka  hali iliyoyalazimu baadhi ya makampuni ya ndege kusitisha safari zake mkoani hapa.

Hayo yamebainika baada ya siku chake Waziri wa Uchukuzi, Dk Harrison Mwakyembe, kufanya ziara yake ya ukaguzi wa uwanja wa ndege na bandari mkoani hapa.

Kampuni ya ndege ya Fly 540, iliyokuwa ikifanya safari zake mkoani hapa imesitisha huduma zake kuanzia Septemba 10, mwaka huu.

Akizungumza na NIPASHE jana ofisini kwake, Meneja tawi la Fly 540  Mtwara, Gilbert Mnanka, alisema kuwa tangu kuanza kwa huduma hiyo kampuni imekuwa ikipata hasara za matengenezo ya ndege hali iliyoilazimu kampuni hiyo kusitisha huduma zake.

Alisema kutokana na uwanja huo kuwa mbovu kwa muda mrefu sasa bila matengenezo imewalazimu kusitisha huduma zao mpaka hapo matengenezo ya uwanja huo utakapokamilika.

“Kwa Mtwara tumeanza kutoa huduma zetu mwezi Mei mwaka jana, lakini toka tuanze huduma hizi gharama za matengenezo ya ndege zimekuwa kubwa sana ikilinganishwa na huduma zetu, hivyo tumelazika kusitisha safari zetu kwa Mkoa huu mpaka hapo uwanja utakapokarabatiwa,” alisema.

“Sababu nyingine ni ukosefu wa taa za kuongozea ndege, hali hii imetugharimu sana, maana tumekuwa tukishindwa kufanya safari zetu usiku, lakini pia tumekuwa tukilazimika kuondoka Mtwara mapema kabla jua halijazama,” alifafanua Mnanka.

Akizumgumza na NIPASHE kwa njia ya simu Meneja uwanja wa ndege mkoani hapa, Mugasa Mlondo, alithibitisha kuwepo kwa taarifa hiyo.

“Hii taarifa ni kweli , kampuni ya Fly 540 wamesitisha safari zao toka  tarehe 10 ya mwezi huu,  lakini sio kweli kwamba uwanja wetu ni mbovu mbona ndege zingine zinakuja”? Alihoji. 

Mapema mwanzoni mwa mwezi huu, Mwakyembe alifika mkoani hapa kwa ajili ya kukagua uwanja wa ndege ambao ulikuwa ukifanyiwa ukarabati wa jengo la abiria (terminal 1) ambalo lilijengwa mwaka 1950, uliogharimu Sh. 173,652,018.10.

Katika taarifa iliyosomwa Septemba 2, mwaka huu Waziri Mwakyembe ilibainisha kuwepo kwa uchakavu wa tabaka la lami kwenye barabara ya kutua na kuruka yenye urefu wa mita 2,250  ambayo ilithibitisha kuwa mamlaka tayari imetenga fedha katika mwaka wa fedha 2012/2013 kwa ajili ya kukarabati sehemu zilizoharibika ili kuwezesha ndege kutua na kuruka kwa usalama.
Chanzo: Nipashe

0 comments:

 
Supported by Tone Multimedia Company Limited
Copyright © 2012. Mtwara yetu - All Rights Reserved
Designed by Fredy Tony Njeje
Proudly powered by Blogs za Mikoa