KAMATI YA FEDHA TANDAHIMBA YARIDHISHWA NA MIRADI YA MAENDELEO

Agosti 5, 2024

Kamati ya Fedha, Utawala na Mipango Halmashauri ya Wilaya ya Tandahimba imekagua Miradi ya Maendeleo inayotekelezwa katika Halmashauri hiyo ikiwemo Elimu na Afya na kupongeza utekelezaji wa Miradi hasa Shule ya Msingi Malamba inayojengwa kupitia Mfuko wa Elimu.

Akizungumza wakati wa Ziara hiyo Makamu Mwenyekiti wa Halmashauri Rehema Liute amesema ubora wa Miradi waliyotembelea inaridhisha huku akisisitiza kasi iongezeke pasipo kuathiri ubora wake.

Kamati hiyo imetembelea Miradi yenye thamani ya Tsh. Milioni 298 ikiwemo Shule ya Msingi Malamba ,
Ujenzi wa matundu 23 ya Vyoo Shule ya Msingi  Mkombozi na Ujenzi wa Zahanati ya Kijiji Cha mitondi B .

#kaziiendeleešŸ”„

 

MRADI WA CHUMBA CHA KOMPYUTA WAZINDURIWA LUAGALA SEKONDARI.

Mwenyekiti wa Mfuko wa Elimu Wilaya ya Tandahimba Mshamu Bakiri amezindua Mradi wa  Chumba Cha Kompyuta Shule ya Sekondari Luagala  Kwa ajili ya wanafunzi wa Shule hiyo kuweza kujifunza Masomo yao pamoja na kuwa na Ujuzi wa TEHAMA.

Mradi wenye Gharama ya Tsh.Milioni 70 ukijumuisha Chumba Cha kompyuta, Meza na Kompyuta 25 umefadhiliwa na Taasisi ya CAMARA EDUCATION TANZANIA ambayo imelenga kurahisisha ufundishaji na  ujifunzaji, kuongeza Ujuzi wa matumizi ya Kompyuta na TEHAMA na hatimaye kuzalisha wataalamu wenye Ujuzi wa TEHAMA hapo baadae.

Mwakilishi wa Mkuu wa Wilaya ya Tandahimba Francis Mkuti amewaasa Wanafunzi akisema
" Mkiitumia Vizuri ufaulu utaongezeka na tunawadai matokeo,hatutarajii kupata Sifuri kwa kuwa Mazingira yameboreshwa"

Kwa Upande wake Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri hiyo DCI.Mariam Mwanzalima amewashukuru wafadhili hao kuwa sehemu ya kuboresha Miundombinu ya Sekta ya Elimu akisisitiza Wanafunzi kutumia Kompyuta hizo kwa matumizi yaliyokusudiwa.

Katika Uzinduzi huo Viongozi mbalimbali wamehudhuria akiwemo Mwakilishi wa Mkuu wa Wilaya, baadhi ya Madiwani na  Wajumbe wa Bodi ya Mfuko wa Elimu .

#kaziiendelee

 


WILAYA YA SIHA YAFIKA TANDAHIMBA KUJIFUNZA MFUMO WA STAKABADHI GHALANI NA MFUKO WA ELIMU.

Agosti 1, 2024

Wataalamu na Baraza la Madiwani Halmashauri ya Wilaya ya Siha kutoka Mkoani Kilimanjaro wamefika Halmashauri ya Wilaya ya Tandahimba Kwa ajili ya kujifunza namna bora ya ukusanyaji wa Mapato  kupitia Mfumo wa Stakabadhi ghalani sambamba na Mfuko wa Elimu ambapo vyote hivyo vinatekelezwa kwa ufanisi katika Wilaya ya Tandahimba.

Awali akizungumza katika Kikao Cha ndani Mkuu wa Wilaya ya Siha Mhe.Dkt.Christopher Timbuka  amesema wameona ni vema kuja kujifunza Tandahimba Kwa kuwa ni Wilaya inayofanya vizuri kwa ukusanyaji wa Mapato kupitia Mfumo wa Stakabadhi ghalani .

Katika kipindi Cha Mwaka wa Fedha 2023/2024 Halmashauri ya Wilaya ya Tandahimba imekusanya Mapato kiasi Cha Tsh.Bilioni 6.7 sawa na 120.98% ya Makisio ya Bajeti ambayo ilikuwa Tsh. Bilioni 5.5.
 
Kaziiendelee

 

KATA YA DINYECHA YAOMBA VIJIJI VIWILI KUPEWA HADHI YA MITAA


Ikiwa ni mkutano wa mwisho wa Baraza la Madiwani kwa mwaka wa fedha 2023/2024 kupokea  na kujadili taarifa za Maendeleo za kata kwa robo ya nne, Leo tarehe 30/07/2024 Kata ya Dinyecha imewasilisha ombi la vijiji viwili Chikwaya na Kibaoni kupewa hadhi ya mitaa. Kwa sasa kata ya Dinyecha Ina Vijiji viwili, Mitaa mitatu na Vitongoji 11.

Mkurugenzi wa Halmashauri ya Mji Nanyamba, Eng. Mshamu A. Munde aliahidi kutuma timu ya wataalamu kuangalia ikiwa vijiji hivyo vina sifa ya kuwa mitaa kabla ya kupeleka ombi hilo ngazi za juu kwaajili ya mchakato zaidi.

Akitoa maoni kuhusu taarifa za maendeleo za kata zilizowasilishwa Mbunge wa Jimbo la Nanyamba, Mhe. Abdallah Dadi Chikota aliwataka wajumbe kuonesha miradi ya maendeleo zinazotekelezwa katika kata zao bila kujali chanzo cha fedha au taasisi wezeshi.

“Mfano kata ya Kitaya kuna mradi mkubwa wa maji utakaotoa maji kijiji cha Maembejuu kwenda Mchanje mpaka kijiji cha Maembechini ambao tayari umefikia 80% lakini kwenye taarifa haijaoneshwa. Hata kule kata ya Nyundo kuna ujenzi wa Zahanati na kijiji cha Niyumba pamoja na ujenzi wa shule fedha za BOOST taarifa haijaainisha hayo.”Alisema Mhe. Chikota

Katika hatua nyingine Mkurugenzi amewataka watendaji wa kata kuhakikisha makusanyo katika kata zako hayashuki 80% kwa ustawi mzuri wa Halmashauri.
 

HALMASHAURI YA MJI NANYAMBA KUJENGA SHULE KUBWA YA UFUNDI.

Halmashauri ya Mji Nanyamba inatarajia kutekeleza mradi wa ujenzi wa shule ya ufundi stadi itakayojengwa katika mtaa wa Nanyamba B Kata ya Nanyamba kwa ufadhili wa SEQUIP.

Taarifa kamati ya Fedha, Utawala na Mipango iliyowasilishwa Leo tarehe 31/07/2024 katika Baraza la Madiwani ilieleza kuwa tayari Kamati ya Maendeleo ya Kata ya Nanyamba (WDC) imefanikiwa kulipa fidia na kutwaa eneo lenye ukubwa ekari 10 kwa gharama ya shilingi 20,000,000 (Milioni ishirini) inayotokana na michango ya shilingi ishirini iliyokatwa kwa wakulima wa korosho.

“Itakuwa ni shule kubwa ambayo itakuwa na mabweni, karakana, maabara na itakusanya wanafunzi wa Halmashauri yote. Mwanafunzi akihitimu pale kutakuwa na cheti cha taaluma pamoja na cheti cha ufundi.” Alieleza Mhe. Abdallah Dadi Chikota, Mbunge wa Jimbo la Nanyamba.

Katika hatua nyingine madiwani wamepiga kura za kumchagua Makamu Mwenyekiti wa Halmashauri, ambapo Mhe. Maliki Hamis Majali, Diwani wa kata ya Kiromba amepigiwa kura za Ndio kuendelea na nafasi yake hiyo.

Aidha, Mhe. Jamal Abdallah Kapende, Mwenyekiti wa Halmashauri ya Mji Nanyamba ametangaza kamati mpya za kudumu zitakazoanza kazi kwa mwaka wa fedha 2024/2025.

 

" TANDAHIMBA TUKO VIZURI UTEKELEZAJI WA AFUA ZA LISHE" MKUTI.

Julai 29, 2024

Mwakilishi wa Mkuu wa Wilaya ya Tandahimba Francis Mkuti ameongoza Kikao Cha Robo ya Nne Cha kijadili Utekelezaji wa Viashiria vya  Mkataba wa Lishe na kuwapongeza Viongozi hasa Watendaji wa Kata kwa kusimamia vyema na kuhakikisha Jamii inakuwa na lishe Bora na kuimarisha Afya zao.

Awali akitoa taarifa ya robo ya Nne(Aprili-Juni 2023/ 2024) Afisa Lishe Wilaya ya Tandahimba Asha Selemani amesema Shule za Sekondari na Msingi zote  Wilaya ya Tandahimba zinapata Chakula walau Mlo mmoja kwa siku , na wamefanikiwa kudhibiti utapiamlo kwa 100% kwa  watoto wenye Umri Chini ya miaka mitano sambamba na kufanikiwa kuelimisha jamii ulaji Bora wa Mlo kamili.

Aidha, Mkuti amewasisitiza watendaji wa Kata kuendelea na kasi hiyo na zaidi kwa kutoa Elimu kwa Jamii juu ya umuhimu wa kuzingatia lishe Bora .

Katika Robo ya Nne Kata ya Mihambwe imeongoza kwa 95.54%  utekelezaji wa Mkataba wa afua za Lishe kati ya Kata 32 za Wilaya ya Tandahimba.

#kaziiendeleešŸ”„

 

KATIBU MKUU DKT NCHIMBI AZURU KABURI LA MKAPA, CCM YATOA MILIONI 10 KUBORESHA MAJENGO YA SHULE LUPASO .


Katibu Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi Balozi Dkt. Emmanuel John Nchimbi ametembelea kaburi la aliyekuwa Rais wa Awamu ya 3, hayati Benjamin William Mkapa katika Kijiji cha Lupaso mkoani Mtwara, leo Julai 28, 2024, kuhani familia na kuzungumza na wananchi wa Lupaso.

Balozi Nchimbi amesema “naomba nikiri kuwa mimi ni mwanafunzi wa hayati na nimekuwa Mwenyekiti wa Umoja wa Vijana Taifa (UVCCM), katika kipindi chake. Ndiye alinilipia ada ya kusoma chuo kikuu na alikuwa mfuatiliaji sana na alitulea vizuri. Sio sisi tu, bali Watanzania wote aliwalea pia. Alikuwa mzalendo kwa nchi, alifanya mabadiliko makubwa kwa nchi yake na kwa Chama chake, lakini yote CCM chini ya Dkt Samia tutaendelea kuyaenzi yale yote aliyoyoacha hayati Benjamin Mkapa. Pamoja hayo nimeambiwa kero za hapa na tumezichukua. CCM inatoa shilingi milioni 10 kuanza kukarabati shule ya hapa Lupaso.”

Katika ziara hii Dk Nchimbi ameambatana na Katibu wa NEC-Itikadi, Uenezi na Mafunzo Ndg. Amosi Makalla, Katibu wa NEC-Organaizesheni Ndg. Issa Ussi Haji (Gavu) pamoja na Katibu wa NEC- Siasa na Uhusiano wa Kimataifa Ndg. Rabia Abdallah Hamid.














 
Supported by Tone Multimedia Company Limited
Copyright © 2012. Mtwara yetu - All Rights Reserved
Designed by Fredy Tony Njeje
Proudly powered by Blogs za Mikoa