Home » » SURUA YATIKISA SHULE

SURUA YATIKISA SHULE

Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399. 
Waziri wa Afya na Ustawi wa Jamii,Dk. Seif Rashid.
 
Wanafunzi 155 wa Shule ya Msingi Mkoma 1 katika kata  ya Mnekachi, wilayani Newala, Mtwara, wameshindwa kuhudhuria masomo kwa wiki moja sasa kutokana na mlipuko wa ugonjwa wa surua.  Mlipuko huo umesababisha hofu miongoni mwa walimu na wananchi kijijini hapo hasa baada ya mwalimu wa taaluma, Hamidu Mnyuko, naye  kuambukizwa ugonjwa huo.
Akizungumza na NIPASHE shuleni hapo, Mwalimu Mkuu wa shule hiyo, Awadhi Mkanapate, alisema mlipuko  huo ulitokea  shuleni hapo Agosti 14, mwaka huu.

“Huu mlipuko ni mkubwa na umeleta madhara makubwa hapa shuleni. Watoto wanakosa masomo... tangu alipogundulika mtoto wa kwanza kuwa na ugonjwa huu, maambukizi yamekuwa yanaongezeka siku hadi siku,”alisema Mkanapate.

Alisema  baada ya maambukizi hayo kuwa makubwa, uongozi wa ofisi ya Mganga Mkuu wa Wilaya ya Newala ulifika shuleni hapo na kuwaeleza kuwa watatoa chanjo kwa wanafunzi wote ili kuzuia maambukizi zaidi.

“Baada ya wataalumu wa afya kufika hapa, waliamua kutoa chanjo kwa shule nzima. Lakini jambo la ajabu mpaka sasa watoto waliopata chanjo hii ni wa darasa  la kwanza na la pili tu, hawa wengine hawajapatiwa chanjo ya aina yoyote ile kama walivyoahidi na hatujui tatizo ni nini,” alisema Mkanapate na kuongeza kuwa kutokana na hali mbaya iliyopo, viongozi kutoka mkoani walifika shuleni hapo na kushauri shule ifungwe kwa ajili ya kuzuia maambukizi.

Alibainisha kuwa watoto walioathirika zaidi na ugonjwa huo ni wa darasa la kwanza hadi la tatu.Mwalimu wa afya shuleni hapo, Mwanahamisi Madidi, aliiambia NIPASHE kuwa chanjo hizo zimetolewa kwa makundi huku baadhi yao wakipatiwa chanjo ya surua, Vitamini A, dawa ya macho na vidonge vya kutuliza maumivu (panadol).

“Kuna kundi lingine (la watoto) walipatiwa chanjo ya surua peke yake na kundi lingine wakapatiwa dawa ya macho na panadol peke yake. Dawa hazitoshi,” alisema.

Alisema mlipuko wa ugonjwa huo huenda ukawa umesababishwa na mazingira ya uchafu kutokana na shule hiyo kutokuwa na choo cha kudumu kwa muda mrefu.

“Jambo la ajabu ni kwamba mlipuko huu upo hapa shuleni tu, kwa wananchi wa hapa kijijini hakuna aliyepata ugonjwa huu na ndiyo maana nasema huenda tatizo la choo likawa ni tatizo mojawapo,” alisema Madidi.

Alifafanua kuwa kutokana na uhaba  wa dawa pamoja na chanjo, baadhi ya wazazi wanalazimika kuwapeleka watoto wao kupata huduma ya afya katika hospitali za watu binafsi.

Naye Leah Tarimo, mhudumu wa afya katika zahanati ya Mkoma 1, alisema kuwa upatikanaji wa chanjo na dawa ni tatizo kubwa na umesababisha watoto wengine wasichanjwe na maambukizi yanazidi kuongezeka.

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa kijiji hicho,  Athumani Nyambi, alisema kuwa kutokana na hali hiyo, serikali ya kijiji imezuia mikusanyiko ya watu ikiwamo katika vilabu vya pombe ili kuzuia kuenea kwa maambukizo zaidi kwa wananchi.

Ofisa Elimu wa Mkoa wa Mtwara, Hepson Kipenya, alisema kuwa hajapata taarifa zozote juu ya mlipuko huo, lakini alisema bwana afya akithibitisha kuwapo kwake, lazima shule ifungwe ili kuzuia maambukizi zaidi.

Kaimu Mganga Mkuu wa Hospitali ya Wilaya hiyo, Dk. James Kisusange, alisema kuwa sheria zinakataza kutoa chanjo kwa watoto wanaoumwa , hivyo wanalazimika  kusitisha zoezi  hilo mpaka hapo hali itakapotulia.

Akizungumzia madai ya upungufu wa dawa kwa wagonjwa, Dk. Kisusange alisema tatizo hilo lilikuwapo, lakini limefanyiwa kazi na tayari wameshapeleka dawa za kupunguza homa na dawa za macho ili kukabiliana na tatizo hilo.

Kuhusu taratibu za kufunga shule, Dk. Kisusange alisema kuwa bado wanasubiri majibu ya sampuli zilizopelekwa Dar es Salaam na kuwa, kama vipimo vitabainisha, shule hiyo itafungwa ili kuzuia maambukizi.

Shule ya Msingi Mkoma 1, ilianzishwa mwaka 1928 na ina jumla ya wanafunzi 988.

SURUA NI NINI?
Tovuti mojawapo ya serikali (http://www.tanzania.go.tz) inaeleza kuwa surua ni ugonjwa wa kuambukiza unaosababishwa na virusi vinavyosambaa kutoka kwa mtu mmoja kwenda kwa mwingine kutokana na majimaji yatokanayo na kukohoa au kupiga chafya.

Ugonjwa huu unaweza pia kumpata mtu mwingine anayegusa sehemu ya majimaji yenye virusi vya surua na kisha kupeleka mkono huo kinywani.Kwa hiyo, ikiwa kuna mtu mwenye virusi vya surua ndani ya nyumba, kuna uwezekano mkubwa wa kuambukizwa kwa watu wengine wote wanaoishi kwenye nyumba hiyo, na pia wageni wao. Hata hivyo, mtu aliyeambukizwa surua huwa hawezi kutambua hilo hadi baada ya wiki mbili tangu siku aliyoambukizwa.

VIFO
Wakati mwingine, ugonjwa wa surua husababisha vifo. Ripoti za Shirika la Afya Duniani (WHO) zinaonyesha kuwa mwaka 2012, kulikuwa na takribani vifo 122,000 vilivyotokana na ugonjwa huu duniani kote, hii ikiwa ni sawa na vifo 330 kila siku au vifo vya watu 14 kila baada ya saa moja.

Hata hivyo, kwa mujibu wa WHO, chanjo ya surua ilipunguza vifo kwa asilimia 78 duniani kote kati ya mwaka 2000 na 2012.

DALILI ZA SURUA
Watoto walioambukizwa surua huanza kuwa na mafua makali.Wanaweza pia kuumwa macho, joto la mwili kupanda na pia mabaka meupe mdomoni na kwenye koo, lakini yanayotoweka haraka. Vipele vidogo vyekundu huanza kuonekana siku chache baadaye, vikianzia nyuma ya masikio, kusambaa shingoni, usoni na mwishowe maeneo ya chini ya mwili na miguuni.

Vipele hivi huweza kubadilika na kuwa vyeusi, hudhurungi na kisha kutoweka.Ipo chanjo maalum kwa ajili ya kinga ya kuzuia ugonjwa wa surua. Hii hutolewa kwa watoto wenye umri wa miezi tisa na hugawiwa pamoja na matone ya Vitamin. Chanjo ya surua imekuwa ikitumika kwa zaidi ya miaka 40 sasa na imethibitika kuwa ni salama, inayozuia vyema maambukizi na pia ni nafuu.

Taarifa zaidi zinaeleza kuwa surua huwa haina dawa kwa sababu ni ugonjwa utokanao na virusi; na kwamba hata dawa za kuua bakteria haziwezi kutibu ingawa husaidia kukabili athari za surua kama maambukizi kwenye masikio na koo.

Njia mojawapo ya kusaidia wagonjwa wa surua ni kuwapumzisha, hasa kwenye chumba cha giza na pia kuwapa maji ya kutosha ili kuzuia ukosefu wa maji mwilini unaoweza kusababishwa na homa kali.

Dawa za kuzuia maumivu hutumika pia ili kuwapa unafuu wagonjwa. Mfumo wa kinga za mwili hupambana na virusi hivi na kuvitokomeza ndani ya wiki au siku 10. Wagonjwa wenye dalili mbaya zaidi hulazwa hospitalini.
SOURCE: NIPASHE

0 comments:

 
Supported by Tone Multimedia Company Limited
Copyright © 2012. Mtwara yetu - All Rights Reserved
Designed by Fredy Tony Njeje
Proudly powered by Blogs za Mikoa