Home » » Olimpiki Maalumu wachuana Mtwara

Olimpiki Maalumu wachuana Mtwara

Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399. 
WANAFUNZI wa shule maalumu kutoka wilaya za Masasi, Tandahimba, Nanyumbu, Newala, Mtwara Vijijini na Mtwara Manispaa mkoani hapa, jana walianza kushiriki mashindano ya Olimpiki Maalumu yatakayofanyika kwa siku mbili katika Uwanja ya Nangwanda Sijaona.
Akisoma risala kwa mgeni rasmi, mwanafunzi wa Shule ya Msingi Shangani, Fatuma Saidi, alimuomba kuwasha Mwenge wa Olimpiki Maalumu, ikiwa ni ishara ya kuwepo kwa michezo hiyo maalumu.
Alisema mwenge unaangazia vitendo vyote vya unyanyasaji na utengaji wa kundi la walemavu na kuonyesha kuwa, wana haki ya kupendwa, kuthaminiwa, kupata elimu bora, kuishi, kucheza na kupata mahitaji muhimu kama wanafunzi wengine wasio na ulemavu.
Mwanafunzi huyo alisema, michezo inawasaidia sana kujumuika na kushirikiana na jamii, kuwaimarisha miili, akili na ni tiba, kwani inawasaidia kufuata kanuni na taratibu katika jamii, kukuza ujasiri na uwezo wa kusimama mbele ya jamii na kujieleza.
“Pia naomba uendelezwe usemi usemao, ‘Walemavu Wakiwezeshwa Wanaweza,’” alisema.
Alisema kuwa Mkoa wa Mtwara umepata heshima kutokana na kutoa wanamichezo mahiri wa kuwakilisha taifa katika mashindano ya dunia mwaka 1996, wavulana wawili na wasichana wawili, ambao walishiriki kwenye riadha na kurudi na medali tisa.
Kwa upande wake, Ofisa Michezo wa Halmashauri ya Mji wa Masasi, Adolfina Hamisi, alisema kuwa lengo la michezo hiyo ya Olimpiki Maalumu katika mkoa na hata taifa ni kuiwezesha jamii kutambua umuhimu wa uwepo wa walemavu na ushirikishwaji kwa ujumla.
Mashindano hayo yanashirikisha mpira wa miguu na riadha huku washindi watauwakilisha mkoa ngazi ya taifa mjini Kibaha, Pwani.
Chanzo;Tanzania Daima

0 comments:

 
Supported by Tone Multimedia Company Limited
Copyright © 2012. Mtwara yetu - All Rights Reserved
Designed by Fredy Tony Njeje
Proudly powered by Blogs za Mikoa