Home » » PINDA AMEPOTOSHWA MRADI WA VIWANJA MTWARA-DC

PINDA AMEPOTOSHWA MRADI WA VIWANJA MTWARA-DC

MKUU wa Wilaya ya Mtwara, Bw. Wilman Ndile, amesema Waziri Mkuu, Bw. Mizengo Pinda, amepotoshwa kwenye mradi wa ugawaji viwanja katika Manispaa ya Mtwara.

Bw. Ndile aliyasema hayo juzi wakati akitoa taarifa ya utekelezaji wa Ilani ya CCM kwa mwaka 2010/15 kwenye kikao cha Halmashauri Kuu ya CCM wilayani humo.

Kikao hicho kilihudhuriwa na Katibu Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Bw. Abdulrahman Kinana ambapo Bw. Ndile alisema tayari mradi huo umekubaliwa na wananchi.

Alisema kutokana na umuhimu wa mradi huo, Halmashauri ya Mtwara ilikopa fedha sh. bilioni tatu ili kuwalipa fidia wananchi wenye mashamba na mazao lakini ameshangaa kuona baadhi ya viongozi wa TAMISEMI wamekataa mradi huo usiendelezwe.

"Katibu Mkuu, baadhi ya watendaji waliopo TAMISEMI, wamempotosha Waziri Mkuu kuhusu mradi wa viwanja lakini mradi huo, wananchi wameupokea na halmashauri imetenga fedha za kulipa fidia sh. bilioni tatu.

"Fedha hizi zitawezesha kupima viwanja 4,000 ambapo mradi huo ni mkubwa na utawawezesha wananchi wengi kuwa na makazi," alisema Bw. Ndile.

Akizungumza na Majira baada ya kumalizika kikao hicho, Bw. Ndile alisema kuna ugomvi wa wanasiasa ambao ni vigogo mkoani humo ndio uliosababisha mradi huo uonekane haufai lakini tayari jitihada zimefanyika na wananchi wamekubali kulipwa fidia.

"Mradi huu ni mkubwa lakini baadhi ya wanasiasa wanaupiga vita kwa sababu za kisiasa na kutolea mfano wa mradi uliokuwa Mkoa wa Lindi ambao ulikuwa na matatizo, kimsingi huwezi kufananisha mradi ule na huu wa Mtwara," alisema.

Chanzo:Majira

Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399.

0 comments:

 
Supported by Tone Multimedia Company Limited
Copyright © 2012. Mtwara yetu - All Rights Reserved
Designed by Fredy Tony Njeje
Proudly powered by Blogs za Mikoa