Home » » MWANAFUNZI DARASA LA TATU AJINYONGA

MWANAFUNZI DARASA LA TATU AJINYONGA

Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399.

MWANAFUNZI wa darasa la tatu shule ya Msingi Mnomo, Kata ya Msangamkuu, Wilaya ya Mtwara Vijijini, Ahmadi Mtuna (10), amefariki dunia baada ya kujinyonga na kamba ya manira katika kenchi za nyumba aliyokuwa akiishi.
Tukio hilo, limetokea jana majira ya saa 5 asubuhi, eneo la Kilimani Kata ya Msangamkuu, ambako Ahmadi wakati akijinyonga familia yake ilikuwa nyumba ya jirani kwenye Maulidi.
Akizungumza na Tanzania Daima kwa njia ya simu, mama mkubwa wa Ahmadi, Sikujua Saidi, alisema jana asubuhi walikwenda na Ahmadi kuchoma korosho maeneo ya barabarani, baada ya kumaliza alimuaga kuwa anarudi nyumbani ndipo alipomruhusu.
Sikujua, alisema naye baada ya kurudi nyumbani alikuta mlango uko wazi, ndipo alipoingia ndani kufunga, lakini kabla ya kufanya hivyo alipotupa jicho juu alimuona Ahmadi ananing’inia, akamuita Ahmadi, Ahmadi lakini ikawa kimya, ndipo alipotoka nje kukimbia kwenda kuwaita majirani kwenye Maulidi ili waje wamwangalie na walipofika walikuta ameshapoteza maisha.
“Inaniuma sana, mwanangu tulikuwa wote muda huu tukichoma korosho dakika chache tu kaniaga naenda nyumbani, kumbe alikuwa ananiaga sitaweza kumuona tena hapa duniani… kikweli siamini kabisa na kilichotokea… Hapa alipojinyongea chini yake tumekuta nazi ambayo haijatolewa maganda, nadhani alikuwa anacheza baada ya nazi kuteleza ndipo aliponing’inia na kamba ikamkaba shingoni na umauti ukamkuta,” alisema Sikujua na kuongeza:
Wakati Ahmadi anajinyonga, Babu na Bibi yake walikwenda nyumba ya jirani kwenye Maulidi, kwa hiyo nyumbani hakukuwa na mtu, alikuwepo pekee yake na kamba aliyojinyongea ilikuwa inatumika kufungia mbuzi, sasa yeye nadhani alikuwa anajaribu kufunga kama anavyofungwa mbuzi…Tutaongea kila kitu lakini ukweli anao yeye marehemu alichokuwa anafanya, maana ni mtoto mdogo hana akili ya kujua hiki ninachofanya ni kitu kibaya, yeye akili yake anajua anacheza kumbe ni hatari.
Kwa upande wake, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mtwara, Augustine Ollomi, alipotafutwa kwa simu kuthibitisha, alikiri kutokea kwa tukio hilo na kuwa tayari maofisa wake wamekwishakwenda eneo la tukio na watakaporejea ofisini na kumpa taarifa, atatoa taarifa zaidi kwa vyombo vya habari.

0 comments:

 
Supported by Tone Multimedia Company Limited
Copyright © 2012. Mtwara yetu - All Rights Reserved
Designed by Fredy Tony Njeje
Proudly powered by Blogs za Mikoa