Home » » JAMII YATAKIWA KUTAMBUA MCHANGO WA WALEMAVU

JAMII YATAKIWA KUTAMBUA MCHANGO WA WALEMAVU

Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399. 
JAMII imetakiwa kutambua, pia kuthamini mchango unaotolewa na watu wenye ulemavu kwani watu hao wana uwezo mkubwa  katika kuchangia pato la familia na taifa.
Ushauri huo ulitolewa na Agnes Machenje, kwenye warsha  ya pamoja kuhusu mchango wa sekta ya habari katika kushughulikia watu wenye ulemavu, ambayo iliwashirikisha waandishi wa habari kutoka Shirika la habari Radio Valo ya nchini Finland na waandishi wa habari kutoka Shirika la habari na mawasiliano ya Jamii (Mtukwao Community Media) kutoka Mtwara pamoja na watu wenye ulemavu.
Machenje, alisema jamii bado hawajaitikia wito wa elimu juu ya watu wenye ulemavu hususani kwa watoto walemavu ambao hawapati haki yao ya msingi ukizingatia elimu.
“Jamii inatakiwa itambue na kufahamu juu ya elimu kwa watoto wao ambao ni walemavu kwani wamekuwa wakikosa elimu na kukosa haki yao ya msingi ukizingatia elimu kwao ni duni kutokana na kumuona mlemavu kama mtu ambae ni mzigo hawezi kufanya kitu chochote…Kinachotakiwa sasa watoto hao wapelekwe shule ili wakapate elimu ndio haki yao ya msingi na ya kikatiba.
“Wazazi ama Walezi walio wengi wao watoto  wao wenye ulemavu wanafungiwa majumbani wakiogopa aibu kuonekana nje na mtu mwingine kwamba yeye amezaa mtoto mlemavu yaani wanasema unaleta mkosi ndani ya familia kwa sababu mtu ukizaa mtoto mlemavu ina maana ni mkosi kwa jamii inayokuzunguka,” alisema Machenje.
Aliongeza kuwa, jamii bado haijapata mwamko wa elimu kujua mlemavu anaweza kufanya kitu kikubwa cha maana  ambacho mtu mwingine ambaye aliye na viungo vyake vilivyotimia angeweza kukifanya.
“Kinachotakiwa sasa jamii iondokane na mtazamo hasi wakimuona mlemavu wasimbague washirikiane naye kwani anaweza akatoa mawazo mazuri sana ambayo yanaweza kuinua jamii na taifa kwa ujumla…Kwa hiyo wajue kwamba mlemavu akiwezeshwa anaweza na asipowezeshwa itakuwa kikwazo lakini walemavu wana vipaji vya aina nyingi na anaweza kufanya kitu kizuri zaidi.
 Chanzo:Tanzania Daima

0 comments:

 
Supported by Tone Multimedia Company Limited
Copyright © 2012. Mtwara yetu - All Rights Reserved
Designed by Fredy Tony Njeje
Proudly powered by Blogs za Mikoa