Home » » 'WATANZANIA WAJIANDAE UCHUMI WA GESI'

'WATANZANIA WAJIANDAE UCHUMI WA GESI'

Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399. 
 
WAZIRI wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo, amewataka Watanzania kujiandaa na uchumi wa gesi kwani mradi huo utakapokamilika utaleta mageuzi makubwa nchini.
Kauli hiyo aliitoa mwishoni mwa wiki mkoani hapa, katika ziara yake ya siku moja aliyoambatana na Balozi wa China nchini, Lu Youqing, kutembelea na kukagua nyumba za wafanyakazi watakaofanya kazi kiwanda cha kuchakata gesi kilichopo Kijiji cha Madimba pamoja na ukaguzi wa mradi wa ujenzi wa bomba la gesi.
Profesa Muhongo alisema mradi huo unakwenda kama ulivyopangwa na utakapokamilika, nchi itaingia kwenye uchumi wa gesi ambao utaondoa umaskini nchini.
“Huu mradi utakapokamilika ndio utaleta mageuzi makubwa ya uchumi nchini kwetu na tutaingia kwenye uchumi wa gesi, kwa sababu gesi ina matumizi mengi na itatuhakikishia kupata umeme wa uhakika ambao ni muhimu kwetu kwa ukuaji wa uchumi,” alisema.
Aliongeza kuwa lengo ifikapo mwaka 2025, Tanzania isiwe nchi masikini bali ya kipato cha kati.
“Kitakachotuwezesha kufika hapo ni huu mradi tunaojenga wa bomba la gesi, kwa hiyo ndugu zangu wa Lindi, Mtwara, Pwani na Tanzania kwa ujumla, tujitayarishe kwenye uchumi wa gesi tukiwa tumetulizana kabisa kwa amani na kuaminiana,” alisema.
Katika ziara hiyo, Tanzania Daima ilikutana na kilio cha muda mrefu cha malipo duni kutoka kwa baadhi ya vibarua wanaofanya kazi mbalimbali katika kiwanda hicho cha kuchakata gesi asilia katika kijiji cha Madima.
Wakizungumza kwa sharti la kuhifadhiwa majina yao, walisema kuwa kiwango wanacholipwa ni kidogo kwa siku, ambacho ni sh 10,000 tofauti na Wachina wanaopata sh 50,000.
“Tunafanya kazi ngumu sana kuanzia saa 12 asubuhi mpaka 12 jioni, hatuna sikukuu wala Jumapili, lakini tunalipwa sh 10,000 kwa siku na hiyo fedha unayolipwa kwa siku tunajitegemea kila kitu, ila Wachina wanalipwa sh 50,000.
“Wakati sisi ndio tunafanya kazi ngumu, wao kazi yao ni kutusimamia na kutuelekeza tu, lakini wanalipwa kiwango kikubwa, chakula wanaletewa na maji safi ya kunywa ya kwenye chupa, ila sisi chakula tunajitegemea, maji ya kunywa ni ya bomba tunawekewa kwenye matanki ndio tunakunywa,” alisema  mmoja wa vibarua hao.
Chanzo:Tanzania Daima

0 comments:

 
Supported by Tone Multimedia Company Limited
Copyright © 2012. Mtwara yetu - All Rights Reserved
Designed by Fredy Tony Njeje
Proudly powered by Blogs za Mikoa