VIONGOZI CHADEMA MTWARA WASHIKILIWA

Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399. 
CHAMA Cha Demokrasi na Maendeleo (Chadema), Wilaya ya Mtwara Mjini, jana walishindwa kuandamana baada ya Jeshi la Polisi mkoani hapa, kuwashikilia viongozi wa chama hicho kuanzia saa moja asubuhi hadi sita mchana.
Maandamano hayo yalitarajiwa kufanyika kuanzia maeneo ya Makanaledi kupitia Mnarani, barabara ya Zambia, Stendi Kuu, Madukani, Bima, Coco Beach hadi viwanja vya Mashujaa, ambako wangezungumza na wananchi, lakini yalidhibitiwa na polisi ambao walionekana wakirandaranda kila kona pamoja na magari ya JWTZ kuhakikisha hakuna maandamano hayo.
Viongozi walioshikikiwa na polisi ni pamoja na Mwenyekiti wa Chadema Wilaya ya Mtwara Mjini, Ibrahimu Mandoa, Mkufunzi Chadema Mkoa, Ismail Liuyo, Katibu Stanslaus Sumi na Katibu Mwenezi Hassani Mbangile.
Akizungumza na Waandishi wa Habari mara baada ya kutoka kituo cha Polisi Wilaya, Mwenyekiti huyo wa Wilaya, Ibrahimu Mandoa, alisema jana Chadema Wilaya walikusudia kufanya maandamano ya amani katika Manispaa ya Mtwara-Mikindani kupinga kuendelea kwa Bunge maalum la Katiba linaloendelea Dodoma.
Alisema kuwa, kimsingi kila mtu atakuwa anaelewa kuwa Rais Kikwete na vyama vya siasa ambavyo viko chini ya TCD, walikuwabaliana kwa pamoja kwamba hakuna uwezekano wa kuweza kupatikana Katiba mpya sasa hivi mpaka 2016 ndio zoezi la mchakato mzima liendelee.
Kwa upande wake, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mtwara, Augustine Ollomi, alithibitisha kukamatwa kwa viongozi hao na kuhojiwa kwa sababu ya kusambaza vipeperushi kwa wananchi.
Ollomi, alisema kuwa viongozi wa Chadema walitoa taarifa ya kufanya mkutano Septemba 21, lakini Mkuu wa Polisi wa Wilaya (OCD), Andrew Ndassa, aliwakatalia kwa sababu zilizotolewa zilikuwa kinyume, wao walitaka kufanya mkutano kupinga Bunge maalumu ambalo linaendelea Dodoma, na kwa ufahamu wake bunge hilo liko kisheria sio kama wanavyodai Chadema.
Alisema, juzi walipata vipeperushi ambavyo vilikuwa vimeandaliwa na viongozi Chadema mkoani hapa wakiwashawishi wananchi washiriki katika maandamano, hivyo ndio sababu ya kuwaita kwa ajili ya mahojiano.
Chanzo:Tanzania Daima

WAFANYABIASHARA WAIOMBA SERIKALI KUONGEZA KINA CHA MAJI

Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399. 
 
WAFANYABIASHARA wanaotumia kivuko cha Kilambo kilichopo wilaya ya Mtwara vijijini, mkoani Mtwara, wameiomba Serikali kuona umuhimu wa kuongeza kina cha maji katika kivuko hicho.
Wakizungumza na Tanzania Daima juzi  wafanyabiashara hao, walisema kuwa kivuko hicho kinategemea maji kutoka mto Ruvuma na Bahari ya Hindi hivyo yanapokupwa kivuko hicho kinashindwa kufanya kazi.
Alisema kivuko hicho kimekuwa kikitumiwa na wananchi wengi ambao wanafanya safari zao  kwenda Msumbiji ama Tanzania,  lakini wamekuwa wakikumbana na adha hiyo.
Mohamedi Mumbea, dereva wa gari kubwa ambaye ni Mtanzania na mfanyabiashara , alisema kuwa kutokana na kina cha maji kuwa kifupi inawalazimu kukaa kwa muda mrefu kusubiri maji.
Akizungumzia tatizo hilo, Mkuu wa Wilaya ya Mtwara, Wilman Ndile, alisema kuwa Serikali inatambua uwepo wa tatizo hilo na kuwa hivi sasa aina mpango wa kuchimba kina hicho.
Hata hivyo Ndile, alisema kuwa wawekezaji wa gesi katika mkoa huo wana mpango wa kujenga daraja katika eneo hilo ambalo linaunganisha nchi za Msumbiji na Tanzania.
Chanzo:Tanzania Daima 

WANAHABARI WAANZISHA SACCOS

Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399. 
 
KLABU ya waandishi wa habari mkoani hapa imekamilisha hatua muhimu katika kuanzisha chama cha kuweka na kukopa kwa wanahabari na wadau wao kitakachojulikana kama Mtwara Media Saccos.
Mwenyekiti wa klabu ya waandishi wa habari mkoani Mtwara MTPC, Hassan Simba, aliwaambia waandishi wa habari ofisini kwake jana kuwa hatua iliyofikiwa sasa ni ya uandikishaji wa wanachama baada ya kukamilisha kuipitia rasmu ya katiba ya chama hicho.
Simba, alisema kuwa rasimu ya katiba hiyo iliandaliwa na kamati maalumu iliyoundwa na kupitiwa na wadau wote na sasa imekamilika na kuweza kutumika kama katiba rasmi ya chama hicho.
“Hatua ya kwanza ilikuwa kuandika katiba ambayo ilizinduliwa na mkuu wa wilaya ya Mtwara Wilman Ndile katika mkutano wa wadau uliofanyika Januari mwaka huu…baada ya hapo ilipitiwa na wanahabari na wadau wao kisha ilirejeshwa kwa kamati ambayo imeipitia na sasa ipo tayari kwa kutumika,” alisema.
Mwenyekiti huyo alisema hadi sasa wadau wamejiandikisha na kujiunga na chama hicho chenye lengo la kuwajengea uwezo kiuchumi wanahabari mkoani humo ambao wengi wao ni wale ambao hawana sifa za kupata mikopo kutoka taasisi za fedha.
Mwenyekiti huyo alisema kuwa chama hicho kitakapokamilika kitakuwa mkombozi wa kiuchumi kwa wanahabari kwani kitatoa mikopo kwa masharti nafuu kwa wanachama wake.
Simba, alisema kuwa chama hicho kwa sasa kinaendeshwa chini ya uongozi wa juu wa MTPC kinatarajiwa kupata viongozi wake miezi mitatu ijayo ambapo kitafanya mkutano mkuu wa kwanza wa uchaguzi.
 Chanzo:Tanzania Daima

NYANGUMI WA TANI 30 AONEKANA MTWARA

Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399. 
Nyangumi wa tani 30 aonekana MtwaraWAKAZI wa Msangamkuu, Mtwara Mjini mkoani Mtwara na vitongoji vyake, jana walimiminika katika pwani ya Bahari ya Hindi kumshangaa samaki aina ya Nyangumi mwenye urefu wa futi 48 na tani zaidi ya 30.
Mbali na mshangao huo nyangumi huyo alikuwa kivutio kwa waliomwona huku ikielezwa kwamba mara ya mwisho samaki huyo alionekana zaidi ya miaka 25 iliyopita.
Akizungumza na Tanzania Daima, mvuvi wa samaki huyo Saidi Hassani ‘Ngassa’ alisema Septemba 3 akiwa katika shughuli zake alizivuta nyavu na kubaini kuna uzito usio wa kawaida uliosababisha chombo chake kuvutwa na samaki huyo.
“Baada ya kuona anaweza kuniletea shida nilimuacha samaki huyo akiwa kwenye nyavu nilirudi nyumbani kuwaita watu wengine ili wanisaidie kuvuta nyavu… lakini siku ya kwanza na ya pili ilishindikana hadi siku ya tatu tulimvuta mpaka pwani,” alisema Ngassa.
Ofisa Uvivu Manispaa ya Mtwara-Mikindani, Saidi Abdallah aliwataka wakazi wa Msangamkuu kutomla samaki huyo kwa kuwa ni sumu, badala yake watumie mafuta yake ambayo ni dawa ya misuli
 Chanzo;Tanzania Daima

ALIYELETA HOFU ABAINIKA HANA EBOLA

Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399. 
 
KIJANA Ally Selemeni (30), mkazi wa Mikindani, mkoani Mtwara aliyeleta hofu kwa wananchi waliokuwepo katika maeneo ya hospitali ya Rufaa ya Ligula kuwa ana dalili za ugonjwa wa Ebola, anaendelea vema na imebainika hana ugonjwa huo.
Akizungumza na waandishi wa habari jana katika hospitali hiyo, Selemani alisema kuwa alilazwa katika hospitali hiyo kutokana na kusumbuliwa na kifua kwa miezi miwili sasa.
Selemani aliyasema hayo kutokana na uvumi uliojitokeza mkoani humo kwamba ameathiriwa na ugonjwa wa ebola baada ya kutokwa na damu katika mwili wake kupitia puani na mdomoni kitendo kilichofanya wauguzi kumkimbia na kwenda kutafuta vifaa vya kujikinga na gonjwa huo.
“Watanzania wenzangu naomba wajue kuwa mimi sina ugonjwa wa ebola ila ni maneno ya watu tu baada ya kuona natoka damu katika mwili wangu wakajua nina huo ugonjwa,” alisema
Naye mdogo wa mgonjwa huyo, Sanjamin Abdallah (20) alisema kuwa kaka yake anasumbuliwa na kifua na sio kwamba ameathiriwa na ugonjwa wa ebola kama ilivyoelezwa na baadhi ya watu waliomuona.
Naye muuguzi aliyekuwepo zamu siku ya tukio, Mariam Mkanyama, alisema kuwa walipoona mgonjwa huyo anatokwa na damu puani na mdomoni walishitushwa na hali hiyo.
“Yaani tulipoona mgonjwa wa kifua anatoka damu puani na mdomoni tulipata na mshtuko mkubwa na tulikimbia kwenda kuchukua vifaa vya kujikinga zaidi kwa ajili ya kuchukua tahadhari ya ugonjwa huo,” alisema.
Alisema kuwa tukio hilo lilitokea Agosti 27 mwaka huu saa 4 asubuhi ikiwa ni siku ya tisa tangu mgonjwa huyu alazwe hospitalini hapo
Chanzo;Tanzania Daima

FAWOPA YAWAWEZESHA WAZAZI, WALEZI

Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399. 

SHIRIKA lisilo la Kiserikali la Faidika Wote Pamoja (Fawopa-Tanzania), la mkoani Mtwara, limeendesha mafunzo ya ujasiriamali kwa wazazi na walezi wa watoto wanaoishi katika mazingira hatarishi ili kuwawezesha kumudu kutunza familia zao.
Akizungumza na waandishi wa habari mara baada ya kumalizika kwa mafunzo hayo siku tatu, Katibu Mtendaji wa Fawopa-Tanzania, Baltazar Komba, alisema lengo kubwa baada ya mafunzo hayo kumalizika ni kuunda vikundi vya watu kumi kumi, ambao watapewa mkopo na  Fawopa kwa ufadhili wa Serikali ya Uholanzi chini ya usimamizi wa Shirika la Maendeleo la Uholanzi la Terre Des Hommes.
“Lengo la Mafunzo haya ni kuwajengea uwezo wazazi ama walezi wa watoto waliondolewa katika ajira na wale ambao walikuwepo katika dalili za kuajiriwa… ili kuweza kuwapa mbinu za ujasiriamali jinsi ya kujitambua, kubadirisha fikra, kuthubutu, kuanzisha biashara na kuzisimamia kikamilifu bila uoga wowote ili kuweza kupata fedha za kuhudumia familia zao bila matatizo yoyote,” alisema Komba na kuongeza:
Hivi vikundi vitakavyoundwa, watakuwa wanakutana na kuchangishana mwenye uwezo wa sh 500 ama 1,000… wanachangisha na wanaweka katika sanduku fedha zao na zikifikia sh 100,000 tutawakopesha laki tano na zikifikia laki mbili tutawakopesha shilingi milioni moja na riba yake ni asilimia 3 kwa miezi sita na mkopo huo utakuwa wa miezi mitatu hadi sita.
Aidha, Komba alisema wamefanya hivyo ili kuwasaidia watoto waendelee na masomo ambayo wamewadhamini, kwa sababu mtoto akitoka chuoni ama shule, nyumbani kama hakuna mahitaji ya muhimu ya msingi atarudi mtaani tena kuendelea na biashara yake ya kuajiriwa ama kujiajiri na kujikuta anaingia katika ajira ya mapema.
“Ni lazima tuwapatie mkopo hawa wazazi, ili mwisho wa siku waweze kuwasaidia watoto wao kuwanunulia mahitaji  muhimu madogo madogo akitoka chuoni ama shule ambako Fawopa tumewapeleka kusoma, akirudi nyumbani akute mahitaji yote muhimu ya kibinadamu,” alisema.
Nao baadhi ya washiriki wa mafunzo hayo, Sharifa Ismail, Mkazi wa Kata ya Reli na Salumu Ally, Mkazi wa Kata ya Vigaeni, waliishukuru Fawopa kwa kuwapa mafunzo hayo ya ujasiriamali.
“Ki ukweli tunawashukuru Fawopa kwa kutupatia haya mafunzo na wameahaidi kutupatia mikopo baada ya kumalizika kwa haya mafunzo, kinachotakiwa sasa ni sisi wenyewe wazazi ama walezi kujitahidi kwa moyo mmoja ili tuwe kitu kimoja tuweze kupata mikopo ambayo tutaweza kuwasaidia watoto wetu,” walisema na kuongeza. Hili Shirika la Fawopa ni watu wa kuigwa sana, yaani watawapeleka watoto wetu shule na chuo kuwasomesha na sisi leo tunasaidiwa mikopo lazima tuowanyeshe moyo wa dhadi kwao,” waliseama.
Chanzo;Tanzania Daima 
 
Supported by Tone Multimedia Company Limited
Copyright © 2012. Mtwara yetu - All Rights Reserved
Designed by Fredy Tony Njeje
Proudly powered by Blogs za Mikoa