Home » » Wadudu waharibifu washambulia mikorosho

Wadudu waharibifu washambulia mikorosho

Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399. 



 WANANCHI wa Wilaya ya Mkinga wamelelamikia wadudu waharibifu wa zao la mti wa mikorosho wanaohatarisha kutoweka kwa zao hilo siku za usoni kutokana na wataalamu kushindwa kuwapatia elimu na namna ya kukabiliana na kero hiyo iliyodumu kwa muda mrefu.

Wameiomba Halmashauri ya Wilaya ya Mkinga kutoa mafunzo kwa wananchi ili kufufua zao hilo kutokana na miti hiyo kukomaa na kushindwa kuzaa ipasavyo kwa sababu ya wadudu hao kuvamia zao hilo ambalo linategemewa kama biashara na kukuza uchumi wao.
Akizungumza na Nipashe jana, mkazi wa Kijiji cha Moa kata ya Moa, ambaye ni mkulima wa zao hilo, Nassoro Mbarouk, alisema ni vyema serikali ya wilaya na Halmashauri ya Mkinga ikaangalia namna ya kurudisha hadhi ya zao la kilimo cha korosho ili kuwaongezea vipato wananchi wa hali ya chini.
Alisema ni vyema halmashauri ikaangalia namna ya kudhibiti wadudu hao katika mashamba yao na kuwapatia mafunzo ili kukabiliana na changamoto ya kukosa mavuno katika vipindi vyote.
Alisema miti ya mikorosho imekomaa na kuzeeka hivyo serikali inapaswa kuunga mkono juhudi za wakulima hao ili kuangalia uwezekano wa kuwapatia mafunzo wakulima kwa lengo la kuondoa kero hiyo ikiwamo pembejeo na miche ya muda mfupi.
‘’Zao hili ambalo limetupa umaarufu mkubwa katika wilaya yetu limekufa na miti kuzeeka hivyo tunaomba maofisa ugani kuhakikisha wanatupatia elimu ili kurudisha hadhi ya sera ya taifa ya kilimo kwanza kwa vitendo,” alisema.
Aidha, alisema wananchi wengi wanakabiliwa na ugumu wa maisha kutokana na mazao mashambani kuvamiwa na wadudu hao hivyo kama serikali itaunga mkono juhudi za wakulima wanaweza kupiga hatua kimaendeleo na kurudisha historia ya zamani kwa mavuno ya zao la korosho ambalo lilikuwa likiongeza uchumi.
Alisema zao la korosho lilikuwa likiuzwa katika nchi jirani za Kenya, Uganda na Zambia na kukuza uchumi kutoka mtu mmoja hadi kufikia kaya na kuondokana na hali ya umasikini wakipato, lakini kwa sasa uchumi wa wilaya hiyo unasua sua kutokana na kilimo kutopewa kipaumbale na baadhi ya viongozi kukwamisha jitihada hizo za walala hoi.


Chanzo Gazeti la Nipashe
 

0 comments:

 
Supported by Tone Multimedia Company Limited
Copyright © 2012. Mtwara yetu - All Rights Reserved
Designed by Fredy Tony Njeje
Proudly powered by Blogs za Mikoa