Kampuni
ya Statoil Tanzania ina furaha kutangaza majina ya vijana watano
waliongia fainali za shindano la biashara la mashujaa wa kesho ambalo
lina dhumuni la kuhamasisha ujasiriamali kwa mikoa ya kusini mwa
Tanzania yaani Mtwara na Lindi.
Akitoa
taarifa hii meneja wa shindano hilo kutoka Statoil, Erick Mchome
amewataja washindi hao kuwa ni Razaki Kaondo, Edward Timamu and Sifael Nkiliye (walioshiriki kama timu moja), Saleh Rashid Kisunga, Azizi Doa, and Yunus Mtopa.
Shindano
la Mashujaa wa Kesho lilihusisha vijana wenye umri kati ya miaka 18 na
25 kutoka mikoa ya Mtwara na Lindi kuwasilisha mawazo yao ya biashara
ambayo baadae yalibadilishwa na kuwekwa kwenye andiko la biashara.
Mwaka
huu shindano hili lilivutia vijana zaidi ya 400 ambao waliwasilisha
mawazo ya biashara zao zinazolenga sekta mbalimbali za uchumi kama
kilimo, ufugaji, mawasiliano, na biashara nyingine ndogondogo. Vijana
waliruhusiwa kushiriki mmoja mmoja au hata kuunda vikundi vya watu
wawili mpaka watatu.
Mwazo
bora yaliyopatikana kati ya 400 yalikuwa 60 na wamiliki wa mawazo hayo
ambao ni zaidi ya vijana 80 kutoka Lindi na Mtwara walipewa mafunzo
maalum ya kuandaa andiko la biashara ambapo yalishindanishwa tena na
kupatikana vijana kumi bora waliopelekwa mbele ya majaji ambao wiki hii
walichagua maandiko matano bora kati ya kumi waliyopokea.
“Vijana
hawa watano watawasili jijini Dar es Salaam wiki ijayo ili kuja kutetea
maandiko yao ya biashara mbele ya jopo la majaji ambao mwisho wake
wataamua nani anafaa kuwa mshindi wa shindano letu,” alisema Bwana
Mchome.
Mshindi
wa shindano hili atatangazwa siku ya Ijumaa tarehe 15 Aprili jijini Dar
es Salaam katika hafla maalum iliyoandaliwa na Statoil ili kumpongeza
mshindi huyo na wenzake wanne ambao wamefanikiwa kuingia fainali.
Mshindi huyo atajinyakulia kitita cha dola za kimarekani 5,000 wakati
washindi wanne waliobakia watapata dola 1,500 kila mmoja. Washindi
wengine watano waliofanikiwa kuingia kumi bora watapata dola 1,000.
“Statoil
inaamini katika kuwawezesha vijana wenye vipaji katika maeneo yote
ambayo tunafanya shughuli zetu na kwa kufanya hivi tunachochea maendeleo
katika maeneo hayo ambayo nasi ni sehemu yake kwani tunafanya shughuli
zetu za uendelezaji wa nishati kama gesi na mafuta.,” amesema Meneja
Mkazi wa Statoil Tanzania, Øystein Michelsen.
0 comments:
Post a Comment