Home » » MIAKA 10 YA TSUNAMI, TANZANIA INAJIFUNZA NINI?

MIAKA 10 YA TSUNAMI, TANZANIA INAJIFUNZA NINI?

 http://www.mwananchi.co.tz/image/view/-/2573254/highRes/910632/-/maxw/600/-/wah201z/-/tunami.jpg
 Miaka 10 iliyopita sikukuu ya Krismasi iliwatumbukia nyongo watalii waliokuwa wakishereheka katika eneo la Banda Aceh, Indonesia baada ya wengi kupigwa na dhoruba ya Tsunami na kufariki dunia.
Tukio hilo lilitokea Desemba 26, 2004 na kusababisha takriban watu 220,000 kupoteza maisha katika janga hilo ambalo pia lilizikumbwa nchi jirani za India, Sri Lanka na Thailand.
Zaidi ya wananchi 170,000 walipoteza makazi, wengi wao katika mji wa Banda Aceh huku pia wakikosa huduma muhimu za kijamii.
Serikali ya Indonesia ilisema kuwa miaka michache baada ya Tsunami hiyo, mashirika zaidi ya 700 kutoka ndani na nje ya nchi yalitoa ushirikiano wa karibu kusaidia waathirika kwa gharama iliyofikia zaidi ya Dola za Marekani 7bilioni.
Miaka 10 baadaye; Desemba 26 mwaka huu maelfu ya wananchi wa Indonesia na watu kutoka nchi mbalimbali duniani, walikusanyika karibu na lango la makumbusho la Tsunami na kufanya ibada na maombi maalumu ya kuwakumbuka wote waliopoteza maisha.
Makamu wa Rais wa Indonesia, Jusuf Kalla aliongoza maadhimisho hayo na kutoa shukurani kwa wafanyakazi, watu kutoka mataifa mbalimbali duniani waliojitolea kusaidia waathirika wa Banda Aceh.
Maisha baada ya Tsunami
Ofisa wa Chama cha Msalaba Mwekundu, Tom Alcedo kutoka Marekani, anakumbuka namna walivyowasaidia waathirika kupata tena huduma muhimu za kijamii.
Anasema wafanyakazi karibu 1,000 wa mashirika mbalimbali yanayosaidia watoto, walilazimika kugawana watoto 1,300 waliokuwa wametengana na familia zao katika mji wa Banda Aceh.
Aidha, kila mmiliki wa nyumba iliyokumbwa na Tsunami au kupata ufa, alipatiwa fidia ya makazi ya muda. Hata hivyo, hakukuwa na ushahidi wa umiliki wa ardhi tena kwa waathirika katika mji huo kwani hata ofisi za Serikali zilisambaratishwa huku asilimia 30 ya watumishi wake wakipoteza uhai.
Changamoto nyingine ilijitokeza katika vifaa vya ujenzi kwani vilianza kupanda thamani, hatua iliyosababisha baadhi kuuzwa kwa magendo.
Kila mfanyabiashara alitumia nafasi hiyo kama sehemu ya kupata utajiri wa fedha nyingi wakati wa kujenga upya makazi na miundombinu ya biashara na viwanda

Funzo la Tsunami
Profesa Humprey Moshi kutoka idara ya uchumi, Chuo Kikuu cha Mzumbe anasema mataifa hayana budi kutambua kuwa majanga kama vile Tsunami hayatatabiriki na yanaweza kutokea muda wowote.
“Kinachohitajika kwa sasa ni suala la majanga kuingizwa kwenye mikakati kama sehemu ya mipango ya kiuchumi. Nchi zilizoendelea na Afrika waendelee kujenga msingi wa tahadhari za majanga kama hayo, itasaidia kwa miaka inayokuja,” anasema.
Mkurugenzi Mtendaji wa Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA) Dk Agnes Kijazi anasema, ni vigumu kwa Watanzania kujiandaa na majanga mithili ya Tsunami kutokana na changamoto ya kupata taarifa kwa haraka.
“Hakuna kipimo kinachoweza kuonyesha Tsunami italipuka siku tatu zijazo, hivyo inakuwa vigumu kutoa tahadhari ya kujiandaa kwa wananchi wanaokuwa kwenye mazingira ya kufikiwa na Tsunami hiyo,” anasema.
Anakiri hatari ya kutokea kwa Tsunami hiyo wakati wowote, akisema tahadhari inahitajika zaidi kwa Watanzania ikiwamo kufuatilia taarifa za mamlaka hiyo.
“Kasi ya Tsunami inapotokea katika nchi za Asia, ukanda wa Bahari ya Hindi hufika mpaka maeneo ya ukanda wetu hivyo ni hatari kwa usalama wa wananchi,” anasema na kuongeza:
“Mwaka 2004, Tsunami hiyo ilifika mpaka ukanda wa bahari yetu ya Hindi na watu kadhaa waliripotiwa kufariki. Ni muhimu kuwa na tahadhari kwa wote.’’
Hata hivyo, Kijazi anawatoa hofu Watanzania akisema katika historia ya mazingira ya nchi, Tsunami hiyo haijawahi kufika na badala yake imekuwa ikiishia katika ukanda wa Bahari ya Hindi.
Tahadhari nchi zinazopakana na bahari
Kituo cha tahadhari cha Tsunami ukanda wa Pacific (PTWC) kinasema, nchi zilizopo katika ukanda wa Bahari ya Hindi hazina budi kuchukua tahadhari.
Katika pwani ya Bahari ya Hindi barani Afrika, nchi zinazoshauriwa kuchukua tahadhari ni Tanzania, Somalia, Kenya, Msumbiji na Afrika Kusini.
Kituo cha tahadhari cha Indonesia kinasema matetemeko yenye ukubwa kama Tsunami, yana uwezo wa kuathiri eneo lote la ukanda wa pwani ya Bahari ya Hindi.
 Chanzo:Mwananchi
Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399.

0 comments:

 
Supported by Tone Multimedia Company Limited
Copyright © 2012. Mtwara yetu - All Rights Reserved
Designed by Fredy Tony Njeje
Proudly powered by Blogs za Mikoa