Home » » ‘MFUMO STAKABADHI GHALANI HAULAZIMISHI KUKOPA’

‘MFUMO STAKABADHI GHALANI HAULAZIMISHI KUKOPA’

MKURUGENZI wa Bodi ya Korosho Tanzania (CBT), Mfaume Juma, amesema kuwa mfumo wa stakabadhi ghalani haumlazimishi mkulima kukopa fedha benki kabla ya kuuza korosho zake.
Kauli hiyo, aliitoa juzi katika mkutano na waandishi wa habari na kuongeza kwamba, kutokana na mahitaji mbalimbali yanayowakabili wakulima hususani wakisubiri kuuza korosho zao kupitia mfumo wa stakabadhi ya maghala, vyama vingi vya msingi vimekuwa vikikopa benki ili kuwalipa wakulima wake malipo ya awali.
Alisema kuwa, taratibu za benki ni kutoa kiasi cha asilimia katika bei mwongozo kama malipo ya wali kwa mkulima, kutegemeana na makubaliano wanayofanya na wateja wao ambao ni vyama vya msingi.
“Katika msimu wa 2013/2014 na 2014/2015, mabenki yalitoa asilimia 60 ya iliyokuwa bei mwongozo wa sh 1,000 kwa korosho daraja la kwanza na sh 8,000 kwa korosho za daraja la pili, kiasi hiki ni sawa na sh 600 kwa korosho daraja la kwanza na sh 480 kwa korosho za daraja la pili.
“Baada ya kukamilika kwa mauzo ya korosho, wakulima wanalipwa fedha zao zilizosalia ukiondoa gharama za uendeshaji ambazo zipo kwenye mkokotoo wa bei uliopitishwa na wakulima wenyewe katika mkutano wao mkuu wa wadau, hii inamaanisha kuwa malipo ya pili na bonasi yanategemea bei inayopatikana sokoni…Upo uwezekano wa wakulima kulipwa pesa zao zote kwa mkupuo mmoja endapo vyama vyao vya msingi havitakopa benki,” alisema.
Hata hivyo, Juma alieleza kwamba katika mfumo wa stakabadhi ghalani, hakuna mkulima anayekopwa korosho zake, bali yeye anakopeshwa kiasi cha fedha ili aweze kujikimu wakati akisubiri mauzo ya korosho zake.
Chanzo:Tanzania Daima
Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399.

0 comments:

 
Supported by Tone Multimedia Company Limited
Copyright © 2012. Mtwara yetu - All Rights Reserved
Designed by Fredy Tony Njeje
Proudly powered by Blogs za Mikoa