Home » » MCHEPUKO WAMPONZA MKAZI NEWALA

MCHEPUKO WAMPONZA MKAZI NEWALA

WATU wawili wamefariki dunia katika matukio mawili tofauti mkoani hapa, likiwemo tukio la mwanaume mmoja kucharangwa mapanga kwa madai ya kukutwa akifanya mapenzi na mke wa mtu.
Kwa mujibu wa Kamanda wa Polisi mkoani hapa, Augustine Ollomi, tukio hilo lilitokea Novemba 3 mwaka huu, Kijiji cha Mnyambe Wilaya ya Newala mkoani Mtwara, ambako Ali Marunda (34), mkazi wa kijiji hicho aliuawa kwa kukatwa panga kichwani na begani na Christopher Mtemela (60).
Kamanda Ollomi, alisema kuwa chanzo cha mauaji hayo ni marehemu kufumaniwa akifanya mapenzi na mke wa mtuhumiwa, ndipo alipoanza kumshambulia kwa mapanga na kusababisha kifo chake.
Aliongeza kuwa, baada ya mtuhumiwa kufanya mauaji hayo alichukua mwili wa marehemu na kuutupa barabarani.
Mtuhumiwa anashikiliwa na polisi kwa mahojiano zaidi na atafikishwa mahakamani baada ya uchunguzi kukamilika.
Katika tukio jingine, Fatuma Abdallah (30), alipoteza maisha baada ya kukatwa mapanga sehemu mbalimbili za mwili wake na mumewe, Abdallah Kantunda.
Kamanda Ollomi, alisema tukio hilo lilitokea Novemba 2 mwaka huu katika Kitongoji cha Rizika, Kijiji cha Kilombelo, Kata ya Mahurunga, Tarafa ya Kitaya Wilaya ya Mtwara.
Alisema kuwa siku ya tukio mtuhumiwa alimvizia mkewe alipokuwa akitokea kisimani kuchota maji na wenzake kisha kumjeruhi kwa kumkata na panga sehemu za kichwani, shingoni, mikononi na mdomoni, majeraha yaliyosababisha kifo chake.
Kamanda, alisema mtuhumiwa bado hajakamatwa na juhudi za kumsaka zinaendelea, kwani baada ya mauaji hayo mtuhumiwa alitoweka na kukimbilia kusikojulikana.
Chanzo:Tanzania Daima
Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399.

0 comments:

 
Supported by Tone Multimedia Company Limited
Copyright © 2012. Mtwara yetu - All Rights Reserved
Designed by Fredy Tony Njeje
Proudly powered by Blogs za Mikoa