Home » » Majaliwa anusa harufu ya ufisadi Bandari Mtwara

Majaliwa anusa harufu ya ufisadi Bandari Mtwara

Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399. 
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa.
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa, amekutana na ufisadi katika utoaji wa zabuni wa ujenzi wa gati mpya tatu Bandari ya Mtwara.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa jana na Ofisi ya Waziri Mkuu kwa vyombo vya habari jana, ufisadi huo alikutana nao Jumamosi iliyopita wakati akiwa kwenye ziara bandarini hapo, akikagua eneo la ujenzi wa gati hizo.
 
Taarifa hiyo ilisema, Majaliwa alieleza ana taarifa kuhusu utolewaji wa zabuni hiyo na mzabuni ameshashinda lakini kuna madai kwamba watu wa manunuzi kupitia Mamlaka ya Udhibiti wa Manunuzi ya Umma (PPRA) ndiyo wanakwamisha zabuni hiyo.
 
Kutokana na hilo, Waziri Mkuu aliwataka wabunge wa mkoa wa Mtwara washirikiane kusimamia suala hilo ili ujenzi wake uweze kuanza mara moja na kuzalisha ajira kwa wananchi wa mkoa huo.
 
 “"Ujenzi ukikamilika siyo tu ajira zitaongezeka, bali hata meli nyingi zitaleta mizigo katika bandari hii na mapato ya mkoa yataongezeka,” ilisema taarifa hiyo ikimnukuu Waziri Mkuu na kuongeza:
 
“Natambua kwamba kuna mpango wa kujenga gati nne, ambazo moja kati ya hizo itajengwa na TPA (Mamlaka ya Bandari), lakini hizi tatu zilitangazwa na kupata mzabuni ambaye ni kampuni ya Hyundai kutoka Japan lakini imekuwa ikizungushwa bila sababu. Tutafuatilia kubaini tatizo liko wapi.” 
 
“Sasa hivi tuna uwezo wa kupaki meli moja tu, lakini gati hizi zikikamilika tutaweza kuwa na meli tatu kwa mpigo, cha msingi tusimamie maamuzi yetu kwamba lazima wafanyabiashara wa korosho watumie bandari hii kusafirisha mizigo yao na si kuipeleka kwingine.”
 
‘MAJIPU’ BODI YA KOROSHO
Waziri Majaliwa alisema kwenye Bodi ya Korosho nako kuna majipu yanahitaji kutumbuliwa. 
 
“RCC (Kamati ya Ushauri ya Mkoa) ilishakaa na kupitisha uamuzi kuwa mizigo yote ipitie Bandari ya Mtwara, lakini kuna watu ndani ya bodi hiyo wanatoa vibali vya kusafirisha mizigo kupitia Bandari ya Dar es Salaam,” alisema.
 
Alimtaka Mkuu wa Bandari ya Mtwara, Prosper Kimaro, awe makini na watu wa kitengo cha manunuzi katika bandari hiyo kwa sababu ni chanzo cha upotevu wa fedha za serikali kutokana na watu wachache.
 
"Hapa si kuna mtu alitaka kuiba Sh. milioni 300 kwa kufoji saini za wakubwa wake?” alihoji Waziri Mkuu swali ambalo lilijibiwa na Kimaro kwamba ni kweli lakini uongozi uliingilia kati kabla wizi huo haujakamilishwa.
 
FIDIA
Kuhusu fidia kwa wakazi wa vijiji vya Kisiwa na Mgao ambao wamekubali kuhama ili kupisha upanuzi wa bandari hiyo, taarifa hiyo ilisema Waziri Mkuu alisema tayari  Sh. bilioni 13.8 zimekwishatengwa na wizara na zitatolewa mwezi ujao.
 
Taarifa hiyo ilisema Majaliwa alimtaka mkuu wa mkoa huo akae na Kamati ya Ulinzi na Usalama ya Mkoa, ili kuweka mbinu za kuthibiti upenyo wa uingizaji wa mchele na sukari kwenye bandari bubu kwa lengo la kukwepa kodi.
 
Desemba 3, mwaka jana Waziri Mkuu alifanya ziara ya kushutukiza katika Bandari ya Dar es Salaam na kukuta makontena 2,431 yalitolewa bila kulipiwa ushuru, pamoja na Novemba 27, mwaka jana kubaini utoroshwaji wa makontena  349 ambayo hayakulipiwa kodi na kuisababishia serikali hasara ya Sh. bilioni 14.
 
Aidha, Februari 19, mwaka huu, kiongozi huyo alifanya ziara ya kushtukiza katika  Bandari ya Tanga na kukuta matishari tatu zikiwa chakavu, bila injini wakati serikali ilitoa fedha ya ununuzi wa matishari ya kisasa.
CHANZO: NIPASHE

0 comments:

 
Supported by Tone Multimedia Company Limited
Copyright © 2012. Mtwara yetu - All Rights Reserved
Designed by Fredy Tony Njeje
Proudly powered by Blogs za Mikoa