Home » » Ghasia: Pelekeni watoto shule

Ghasia: Pelekeni watoto shule


WAKAZI wa Mtwara vijini mkoani hapa wahimizwa kuwapeleka shule watoto wao ili waweze kunufaika na fursa zitokanazo na kuwapo kwa gesi mikoa ya kusini, badala ya kulalamika kuwa hawapati ajira katika miradi iliyopo.
Wito huo ulitolewa jana na Mbunge wa Jimbo la Mtwara Vijijini, Hawa Ghasia alipokuwa akizungumza na wananchi katika mkutano wa hadhara wa kuwashukuru kwa kumchagua kuwa mbunge katika uchaguzi uliofanyika kwenye kijiji cha Hiyari.
Ghasia alisema kuwa ni vyema wananchi wakawapeleka shule watoto wao ili wapate elimu itakayowawezesha kupata sifa za kuajiriwa katika miradi mbalimbali inayotarajiwa kuanzishwa mkoani hapa kutokana na kuwepo kwa fursa ya gesi ambapo wawekezaji wanatarajiwa kufungua viwanda na miradi mingine.
“Ninawaomba ndugu zangu tuwasomeshe watoto wetu ili waweze kuwa na sifa za kuajiriwa katika miradi ya gesi itakayoanzishwa baadaye,” alisema Ghasia.
Kauli hiyo ilikuja baada ya wakazi wa kijiji cha Hiyari kilipo kiwanda cha saruji cha Dangote kudai kuwa kumekuwa na ubaguzi wa kutoa ajira kiwandani hapo ambapo wakazi wa kijiji hicho hawapewi nafasi hata ya kupata kazi za ufagizi na kumwagilia bustani ambazo walisema hazihitaji elimu ya juu.
Akisoma taarifa ya kijiji mbele ya mbunge huyo, mjumbe wa serikali ya kijiji hicho, Luis Usale, alisema kuwa wakazi wa kijiji hicho mara kadhaa wamekuwa wakiomba kazi kiwandani hapo na kukosa huku wakipewa wanaotoka mbali na hapo.

HABARI LEO

0 comments:

 
Supported by Tone Multimedia Company Limited
Copyright © 2012. Mtwara yetu - All Rights Reserved
Designed by Fredy Tony Njeje
Proudly powered by Blogs za Mikoa