SHIRIKA la Maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC) limetoa msaada wa madawati 500 kwa kata ya Madimba wilaya ya Mtwara.
Msaada huo umefanya kata hiyo ifanikiwe kukamilisha agizo la Rais
John Magufuli kwa asilimia 100, hivyo kutokuwa na wanafunzi wanaokaa
chini.
Kata hiyo ya Madimba ndipo kwenye kiwanda cha kuchakata gesi,
inayosafirishwa kwa bomba la gesi mpaka jijini Dar es Salaam Mkurugenzi
wa TPDC, Dk James Mataragio alimkabidhi madawati hayo Mkuu wa Mkoa wa
Mtwara, Halima Dendego katika shule ya msingi Madimba na kushuhudiwa na
viongozi wa mkoa na wilaya.
Dk Mataragio alisema katika kuendelea kutekeleza dhana ya
uwajibikaji, TPDC imechangia madawati 500 kwa halmashauri ya Mtwara
Vijijini, lengo likiwa ni kumaliza tatizo la wanafunzi kukaa chini
wakiwa darasani.
Alisema kwa kutumia madawati hayo, utasaidia wanafunzi kupata elimu
bora na hatimaye kupata wataalamu watakaokuja kufanya kazi katika sekta
ya mafuta na gesi hapo baadaye.
Akizungumzia suala la madawati wilayani hapo, Mkuu wa Wilaya ya
Mtwara Vijijini, Fatma Ally, alisema baada ya msaada huo wa madawati,
kata ya Madimba imekamilisha agizo la Rais kwa asilimia 100 huku kata ya
Mkubiri ikibaki na uhaba wa madawati 14, ambayo atayanunua yeye na wao
kuwa wamekamilisha uhaba huo.
Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Mtwara
Vijijini, Denis Kitali alisema wilaya hiyo ina shule 67 za msingi na
sekondari huku kukiwa na upungufu wa madawati 5563 kutokana na mahitaji
ya madawati 13,155 na sasa wanayo madawati 7562.
Alisema kwa kushirikiana na wadau mbalimbali na kukarabati madawati
yaliyokuwa yakiharibika, watahakikisha wanakamilisha agizo la Rais
kutokuwa na mwanafunzi anayekaa chini.
Dendego alisema watahakikisha wanatekeleza agizo hilo la Rais kwa asilimia 100, ingawa bado kuna changamoto.
Lakini, aliwaagiza watendaji wake kuwa kabla yeye hajatumbuliwa, basi
atakuwa ameishawaondoa wao. Hivyo kwa kushirikiana, wameanzisha
programu mbalimbali zitakazowezesha kupata madawati katika shule zote
ikiwa ni pamoja na kuwaomba wadau mbalimbali kuwasaidia kufikia malengo.
CHANZO: HABARI LEO.
0 comments:
Post a Comment