Home » » Mzee Mkapa awaasa waandishi wa habari.

Mzee Mkapa awaasa waandishi wa habari.

Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399. 

Rais mstaafu, Benjamin Mkapa.
Rais mstaafu, Benjamin Mkapa, amewaasa waandishi wa habari nchini kuandika habari kwa usahihi na uadilifu ili kuepuka uchochezi na kulingiza taifa kwenye vurugu na machafuko na kurudisha nyuma maendeleo.
 
Mkapa alitoa onyo hilo juzi mjini hapa, wakati wa ufunguzi wa kituo cha redio ya kijamii ya Fadhila kilichopo Wilaya ya Masasi mkoani Mtwara.
 
Mkapa alisema waandishi wa habari wakiandika habari kwa usahihi, ukweli na kwa lugha inayoeleweka kwa jamii, watasaidia kuleta maendeleo nchini.
 
Alisema taaluma ya uandishi wa habari inayo fursa kubwa kuleta maendeleo ya kijamii na kisayansi.
 
Mkapa alisema maendeleo hayo hayawezi kuletwa kama waandishi wa habari wataandika habari zisizo za uhakika na usahihi unaoendana na maadili ya taaluma yao. 
 
“Andikeni habari za ukweli zenye lugha ambayo ni sahihi maana baadhi ya waandishi hasa katika redio za kijamii kwani bado hawatambui namna ya matumizi ya lugha katika kuandaa habari na hata kutamka matamshi hawatamki kwa usahihi unaotakiwa, ”alisema Mkapa.
 
Aliongeza kuwa baadhi ya waandishi wamekuwa wakikiuka maadili ya uandishi kwa kuandika habari za uchochezi dhidi ya watu ili kuchafua majina yao bila ya kufanya uchunguzi.
 
 Kwa upande mwingine, Mkapa alikipongeza kituo hicho kwa kurusha matangazo kwa usahihi kwa jamii iliyozungukwa na kwamba kwa sasa kinaweza kupata habari mbalimbali za wilaya ya Masasi na maeneo mengine ndani ya mkoa wa Mtwara na Lindi na taifa.
 
Naye Askofu wa Kanisa Katoliki Dayosisi ya Jimbo la Tunduru- Masasi, Castor Msemwa, alisema waandishi wa habari wanatakiwa kuwa na roho ya kumcha Mungu ili waweze kuandika habari katika mazingira ya amani na utulivu.
 
Msemwa alisema waandishi wanapaswa kuwa huru wakati wa kutimiza majukumu yao bila ya kuwekewa vizuizi katika kukusanya habari na pale wanapohabarisha umma kwa masilahi ya taifa.
CHANZO: NIPASHE

0 comments:

 
Supported by Tone Multimedia Company Limited
Copyright © 2012. Mtwara yetu - All Rights Reserved
Designed by Fredy Tony Njeje
Proudly powered by Blogs za Mikoa