Home » » MAKALA MAALUM YA MAKALA YA MELI VITA‏

MAKALA MAALUM YA MAKALA YA MELI VITA‏

Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399. 



Hussein Makame-MAELEZO
USTAWI wa nchi yoyote duniani unategemea uwezo wa kulinda mipaka yake na rasilimali muhimu zilizopo ili kunufaika nazo na kuweza kupambana na maadui wake.
Katika kuhakikisha inatekeleza jukumu hilo kwa uhakika, Kamandi ya Jeshi la Wanamaji la Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ), hivi karibuni lilizindua meli vita 2.
Meli hizo zilizopewa majina ya P77 PNS Mwitongo na P78 PNS Msoga, zimepatikana kwa msaada wa Serikali ya Jamhuri ya Watu wa China.
Mkuu wa Jeshi la Wanamaji la JWTZ, Brigedia Generali Rogastian Laswai anasema kupatikana kwa meli hizo ni tamati ya wazo lililodumu kwa muda mrefu la wakuu waliopita wa kamandi hiyo waliobuni kutengeneza meli vita hizo.
Hata hivyo, Mkuu wa Majeshi Jenerali Davis Mwamunyange anasema meli hizo zimepatikana kupitia utekelezaji wa dhana ya Tanzania kuwa na jeshi dogo la kisasa linalotekeleza majukumu yake kwa ushupavu na weledi wa hali ya juu.
“Utekelezaji wa dhana hii ni pamoja na ununuzi wa zana na silaha mbalimbali za kivita, kuendeleza mafunzo ya kijeshi kulingana na wakati, na kuboresha huduma muhimu kama vile makazi ya wanajeshi” anasema Jenerali Mwamunyange.
Anasema kuwa meli hizi zitasaidia kwa kiasi kikubwa kulifanya jeshi hilo kutekeleza majukumu yake kwa ufanisi zaidi na kwa niaba ya Serikali ya Tanzania chini ya uongozi wa Rais Dkt. Jakaya Kikwete anaamini itahakikisha inaendelea kutekeza dhana hiyo.
Akizungumzia mchango wa China kwa jeshi hilo, Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa, Dkt. Hussein Mwinyi anasema Jeshi la Wanamaji limeanzishwa rasmi mnamo mwaka 1971 kutokana na msaada wa Serikali ya Jamhuri ya Watu wa China.
“Kwa kuanzia Serikali ya China ilitoa meli 13 na pia walitujengea vituo vya rada kwa ajili ya uchunguzi wa pwani.Kuanzia mwaka 1971 China imekuwa ni msaada mkubwa ikiwemo ujenzi wa karakana na terezo ya kuhudumia meli vita”anasema Waziri Dkt. Mwinyi.
 Anasema hadi leo Serikali ya Watu wa China imeendelea kuisaidia Tanzania kwa kuipatia meli vita hizo, wataalamu kwa ajili ya karakana na kutoa nafasi nyingi za mafunzo kwa maafisa na askari wa JWTZ.
Mbali na mchango huo, Waziri Dkt. Mwinyi anasema China imeianzishia Combania ya Marine Special Forces pamoja na vifaa vya mafunzo na kuendelea kuipatia walimu na wakufunzi kwa ajili ya shule ya Ubaharia iliyopo makao makuu ya Kamandi ya Navy.
Anabainisha kuwa hizo zimekuja muda muwafaka kutokana na mpango wa utafiti wa gesi na mafuta pamoja na kupambana na uharamia baharini ambao siku za karibuni umekuwa ni tishio kwa taifa.
Anaongeza kuwa kupatikana kwa meli hizo kumezidisha ari ya utendaji kazi kwa maafisa na askari wa kamandi ya Navy kwani sasa wamepata uwezo wa kulinda mipaka ya Tanzania ya bahari kwa ufanisi zaidi.
“Wizara ya Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa kwa niaba ya Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania na hususan Kamandi ya Navy, tunakushukuru na kukupongeza Amiri Jeshi Mkuu kwa kuimarisha jeshi letu kwani uzinduzi wa leo ni kielelezo kingine tena cha dhamira na jitihada madhubuti za kuliimarisha na kuliendeleza jeshi letu” anasema.
Anaongeza kuwa hadi sasa jeshi hilo limefanikiwa kupunguza uharamia na uvuvi haramu, limewezesha maafisa na askari wa JWTZ kushiriki kwenye operesheni mbalimbali na kuiletea sifa nzuri na heshima Tanzania.
Akizungumza kabla ya kuzindua meli hizo, Rais Jakaya Kikwete ameishakuru Jamhuri ya Watu wa China kwa kuiwezesha Tanzania kupata meli hizo.
“Ni ukweli usiofichika kuwa katika kuendeleza jeshi letu hili hatuna mshirika anayefanana na Jamhuri ya Watu wa China.Wametusaidia kwa mengi na ushirikino wetu sasa umekuwepo tangu Jeshi hili limeanza miaka 51 iliyopita mpaka leo hawajachoka” anasema Rais Kikwete.
“Kwa kweli hatuna maneno mazuri ya kuwashukuru zaidi ya kusema ahsanteni sana.Tunatoa shukrani maalum kwa kampuni ya Polytechonologies kwa ushirikiano wao.Hii ni moja ya kampuni ya China tunayoshirikiana nayo katika kupata silaha za jeshi letu”.
Anasema kupatikana kwa meli hizo kunaandika historia mpya katika Jeshi la Wanamaji kwani Kamandi ya Navy ya JWTZ imekuwa ikipata msaada mbalimbali kutoka Jeshi la Ukombozi la China hadi sasa ingawa zipo nchi nyingine zinazoisaidia Tanzania.
“Waswahili wanasema usione vyaelea vimeundwa, haya yote ni matunda ya udugu na urafiki baina ya nchi zetu ulioanzishwa na viongozi  waasisi wa mataifa haya Rais Mao Zedong kwa upande wa China na mwalimu Julias Nyerere kwa upande wa Tanzania.”
“Lakini pia viongozi waliowafuatia viongozi hao wa China na Tanzanaia nao pia wameendelea kudumisha na kuendeleza uhusiano huo, hayo ndio yametufikisha hapa tulipo.”
Rais Kikwete ameahidi kwamba ataendelea kuuenzi na kuudumisha uhusiano huo wenye tija kubwa kwa nchi zote mbili.
Balozi wa China nchini Tanzania, LU Youqing anasema historia ya maendeleo ya nchi nyingine duniani inaonesha kwamba ili kukabiliana na  matatizo ya ulinzi na usalama wa ndani na nje ya nchi ni lazima uwe na jeshi lenye uwezo mkubwa wa kiulinzi.
Anasema ushirikiano wa majeshi kati ya Tanzania na China ni sehemu muhimu sana kwa nchi husika kwani umekuwa nguzo kubwa ya maendeleo ya nchi hizo.
 “Kwa kweli tunajisikia furaha sana kwa hilo na tunatoa pongezi zetu za dhati kwani hii inaonesha kwamba urafiki na uhusiano kati ya China na Tanzania umepata maendeleo makubwa sana” anasema Balozi Youqing.
“Nikiwa Balozi wa China nchini Tanzania mimi binafsi nimeshuhudia  ushirikiano mkubwa wa urafiki mkubwa na udugu wa dhati na China na hii inaashiria kwa Wizara za Ulinzi ya Taifa la China na Tanzania zimefanikiwa kuanzisha uhusiano mzuri” anaongeza.
Anasema wanaamini ushirikiano wa Jeshi la China na Tanzania utaendelea kukua, Wizara ya Ulinzi ya China na Jeshi la China litaendeleo kuunga mkono ujenzi na maendeleo ya Wizara ya Ulinzi ya Tanzania na Jeshi la Tanzania”
“Meli vita hizi mbili zinaweza kutoa mchango wa usalama na maendeleo ya Tanzania na hatimaye jeshi la wanamaji liwe na nguvu zaidi.Udumu milele ushirikiano na urafiki kati ya China na Tanzania.”
Rais Kikwete anabainisha kuwa meli hizo ndio meli kubwa kuliko zote ambazo Jeshi la Wanamaji linazo na kwamba zina uwezo wa kwenda kwa kasi kubwa zaidi na kubeba silaha zenye nguvu zaidi.
“Moja ya kilio chetu cha muda mrefu ni uwezo mdogo wa meli zetu na lengo letu ilikuwa ni kulipa uwezo jeshi letu kwa kupata meli kubwa zenye uwezo wa kulinda mipaka yetu na rasilimali zetu kwenye maji makubwa” anasema Rais Kikwete.
Baada ya kupata meli hizo Rais Kikwete anasema “Kwa hiyo sasa tuna uwezo wa kulinda mipaka yetu ya bahari na mpaka wetu ni mrefu una kilomita 1000 kutoka kule Moa mpaka unafika Msimbati ni maili 850 ambazo ni sawa na kilomita 1000”
Anaongeza kuwa “Kwa hiyo huwezi ukaulinda kwa viboti vidogo vidogo lazima uwe na meli kubwa kama hizi mbili na kuweza kujenga uwezo wa kutosha.Kwa hiyo ndugu zetu wa China tunachoahidi ni kwamba tutaendelea kushirikiana nanyi”
Anabainisha kuwa kabla ya kupata meli hizo Tanzania imekuwa ikishirikiana na Kenya, Msumbiji na hata Afrika Kusini ili kulinda mipaka na rasilimali zake.
Hivyo anasema sasa ana uhakika mpaka wa bahari wa Tanzania utakuwa unalindwa kwa uhakika na rasilimali zake zitakuwa zinalindwa kwa uhakika.
Naye Waziri Dkt. Mwinyi anasema meli hizo pia zitaongezea uwezo wa JWTZ kutekeleza majukumu yake mbalimbali katika eneo la bahari ikiwa ni pamoja na kupambana na maharamia.
 “Pia meli hizi zitasaidia kutoa msaada kwa mamlaka za kiraia wakati wa majanga, kusaidia kudhibiti uvuvi haramu pamoja na kutekeleza shughuli nyingine mbalimbali kwa mahitajio ya kitaifa na kimataifa”, anasema Dkt. Mwinyi na kuongeza kuwa:
Hata hivyo, pamoja na kupata meli hizo Rais Dkt. Kitwete anasema kuna mpango mwingine wa kupata meli vita nyingine kubwa zaidi ya hizo.
“Kwa muda mrefu tumekuwa tuna kazi ya kutafuta meli zenye uwezo huo lakini nataka kuwaambia kwamba tuna mpango tayari wa kupata meli nyingine na baada ya muda si mrefu tunachozughulikia tu ni upatikanaji wa fedha.Tukishakamilisha taratibu za kupata fedha kuna meli nyingine zitakuja bora zaidi, kubwa zaidi na zenye uwezo mkubwa zaidi”
 “Ni ghali lakini lazima tuzichukue.Kwani kulinda uhuru ni kazi rahisi?Maana ukisema ni gharama kupata vifaa hivyo hasara yake ndio hii, tunaibiwa samaki wetu, tuna gesi asili, kule ipo siku watu wanaweza kwenda wakabomoa platform zile wakatuibia rasilimali, hivyo lazima tujenge uwezo wa kuhakikisha kwamba tuna uwezo wa kulinda mipaka yetu”.
Kama hiyo haitoshi anasema kuwa huo ni mwanzo wa kufanya mambo makubwa kwa ajili ya Jeshi la Wanamaji kwani mipango imekamilika ya kupata vyanzo vya fedha na anaamini kabla hajaondoka madarakani anaweza kukukamilisha hilo.
Hivyo analitaka JWTZ na kuwamuru maafisa na askari katika meli vita hizo kutekeleza majukumu yao kwa uhakika na uhodari wa hali ya juu kwa kuzingatia na kufuata amri na maelekezo yaliyopo.
Pia wafuate maelekezo yatakayotolewa na viongozi wao kwa mujibu wa katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Sheria ya Ulinzi wa Taifa na kanuni za majeshi ya Ulinzi.
Kwa mujibu wa JWTZ, meli hizo mbili zina mizinga kisasa mikubwa miwili na mizinga ya msaada sita kwa kila meli na baadhi ya mizinga hiyo inapiga  kwa kutumia nguvu ya umeme na vifaa maalum vya kutafutia shabaha vinavyoitwa GF 90.
Silaha za meli hizo husaidia katika mashambulizi ya boti ndogo za maharamia ambazo zinaweza kuwa zinakaribia meli hiyo au kwa chombo kingine tunachokwenda kutoa msaada baharini.
Mizinga hiyo yenye uwezo mkubwa ina uwezo wa kupiga shabaha ya baharini kwa umbali wa kilometa 9, shabaha ya angani umbali wa kilometa 7.
Hivyo hiyo meli hii ina uwezo wa kufanya mapigano ya angani, baharini na hata nchi kavu na zinaweza kusafiri kutoka bandari ya Dar es Salaam hadi kwenye Economic Exclusive Zone ya Tanzania na ikaongeza umbali wa mita 150 nautical miles.
Aidha zinaweza kwenda na kurudi eneo hilo kwa muda wa siku saba baharini bila kuongeza mafuta, maji wala oil na kuwa na chakula cha kutosha.
  
 

0 comments:

 
Supported by Tone Multimedia Company Limited
Copyright © 2012. Mtwara yetu - All Rights Reserved
Designed by Fredy Tony Njeje
Proudly powered by Blogs za Mikoa