Home » » SERIKALI YAPIGA MARUFUKU UPIGAJI RAMLI

SERIKALI YAPIGA MARUFUKU UPIGAJI RAMLI

Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Mathias Chikawe.
Serikali imepiga marufuku waganga wa jadi maarufu kama wapiga ramli, kutokana na kuwa chanzo cha mauaji watu wenye ulemavu wa ngozi (albino) yaliyoibuka kwa kasi nchini hivi karibuni.

Waganga hao wametajwa kuhusika moja kwa moja kutumia njia hiyo kufanya udanganyifu kwa wanasiasa wanaogombea ngazi tofauti za kisiasa pamoja na watu wanaotaka kupata utajiri wa haraka.

Akizungumza jana jijini Dar es Salaam, Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Mathias Chikawe, alisema Jeshi la Polisi na Chama cha Maalbino Tanzania (TAS), wameunda kikosi kazi kwa ajili ya kufanya operesheni ya ukaguzi kuwabaini waganga ambao watakiuka agizo hilo.

Alibainisha kuwa ili operesheni hiyo iweze kutekelezeka, wizara itashirikiana na Wizara ya Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi), ili kuwabaini waganga hao katika mitaa, Kata, Tarafa, Wilaya na mikoa.

“Kuna wimbi kubwa la waganga wapiga ramli ambao wanawadanganya watu wataweza kupata ubunge, udiwani na utajiri kwa njia ya kuwateka, kuwaua albino, hii si kweli, hakuna utajiri wa haraka haraka wa bila kufanya kazi ni udanganyifu na uhalifu,” alisema Chikawe.

Alisema, operesheni hiyo ya kikosi hicho, kitaanza kufanya kazi wiki mbili zijazo katika mikoa mitano sugu inayoongoza kwa matukio ya mauaji ya albino, ambayo ni Mwanza, Simiyu, Geita, Tabora, Shinyanga na kisha Mara, Kagera na Rukwa.

Pia Waziri Chikawe alisema kikosi hicho kitashughulikia kesi ambazo zilifutwa awali kutokana na kukosekana na ushahidi wa matukio hayo ili kuweza kuzirudisha mahakamani kusikilizwa tena.

Alisema operesheni hiyo itakayokuwa na watu wanne kutoka TAS na wawili kutoka Jeshi la Polisi, na kusema kesi zote zitatolewa uamuzi kwa kushirikiana na Mahakama pamoja na ofisi ya Mkurugenzi wa Mashtaka wa (DPP).

Mwenyekiti wa TAS, Ernest Kimaya, aliipongeza serikali kwa kuanzisha operesheni hiyo, alisema kilio cha muda mrefu cha maalbino kimesikilizwa huku akivitaka vyombo vya habari, wananchi kutoa ushirikiano ili kuhakikisha taarifa za vitendo hivyo zinafikishwa katika vyombo vya usalama.

Hivi karibuni mtoto Pendo Emmanuel (4) wa Kijiji cha Ndami, Wilaya ya Kwimba, mkoani Mwanza, usiku wa saa nne aliibwa na watu wasiofahamika walivamia nyumbani kwa wazazi wa mtoto huyo na kutoweka naye kusikojulikana.

Waziri Chikawe alisema kuwa watu 15 tayari wamekamatwa kwa ajili ya kuhojiwa kuhusiana na tukio hilo.

Takwimu za kuanzia mwaka 2006 zinaonyesha kuwa albino 74 wameshauawa nchini huku 56 wakinusurika kifo, kati yao 11 wamepata ulemavu mwingine wa kudumu.
CHANZO: NIPASHE
Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399.

0 comments:

 
Supported by Tone Multimedia Company Limited
Copyright © 2012. Mtwara yetu - All Rights Reserved
Designed by Fredy Tony Njeje
Proudly powered by Blogs za Mikoa