Home » » MAAMBUKIZI YA UKIMWI YAPAA MASASI

MAAMBUKIZI YA UKIMWI YAPAA MASASI

MAAMBUKIZI ya virusi vya Ukimwi katika katika Halmashauri ya Mji wa Masasi , mkoani Mtwara yenye wakazi 102,696 yameongezeka kutoka asilimia 6.1 mwaka 2013 hadi kufikia asilimia 7.2 kwa mwaka 2014.
Ongezeko hilo linafanya mji huo kuwa miongoni mwa wilaya za mkoa huo ambazo kasi ya maambukizi ya virusi hivyo ni makubwa na kusababisha vifo vingi vya wazazi huku watoto wakibaki yatima.
Hayo yalibainishwa juzi na Ofisa Tawala wa Halmashauri ya Wilaya ya Masasi Jenifer Mapembe wakati akihutubia mamia ya wananchi kwenye kilele cha Maadhimisho ya Siku ya Ukimwi Duniani yaliyofanyika katika kijiji cha Mtakuja mjini Masasi.
Alisema licha ya kuwepo kwa jitihada kubwa za kuelimisha na kuhamasisha jamii zinazofanywa na Kamati ya Kudhibiti Ukimwi bado athari za ugonjwa huo kwa jamii ya Masasi zimekuwa kubwa na tishio kwa ustawi wa wakazi wa mji huo.
Alisema kuendelea kuwepo kwa watu ambao hawapendi kubadilika kitabia kuhusu athari za ugonjwa wa Ukimwi kwa jamii pamoja na kuwepo kwa matukio mbalimbali ya ngoma za asili na ngoma za vigodoro ndicho chanzo kikuu cha maambukizi ya ugonjwa wa Ukimwi kwa wakazi wa mji wa Masasi.
“Jamii inapaswa kubadilika ili kuzuia maambukizi mapya ya Ukimwi na endapo watu wataendelea kuwa na tabia ya ubishi basi mji wa Masasi uko kwenye uwezekano mkubwa wa kuendelea kuwa na idadi kubwa ya wananchi wanaoambukizwa ugonjwa huu,” alisema.
Kwa mujibu wa Ofisa Tawala huyo, Serikali ya Wilaya kwa ushirikiano na Kamati ya Ukimwi ya Wilaya pamoja na Idara ya Ustawi wa Jamii wamekuwa wakifanya jitihada kubwa ya kutoa elimu kwa wananchi ili watambue athari za Ukimwi.
Mratibu wa Ukimwi Halmashauri ya Mji wa Masasi Sada Mustapha alizitaja changamoto ambazo huchangia kuenea kwa kasi ugonjwa wa Ukimwi kuwa ni kutoshiriki kwenye mikutano ya elimu juu ya ugonjwa huo.

Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399. 
Chanzo;Habari Leo

0 comments:

 
Supported by Tone Multimedia Company Limited
Copyright © 2012. Mtwara yetu - All Rights Reserved
Designed by Fredy Tony Njeje
Proudly powered by Blogs za Mikoa