Home » » BAVICHA YALAANI UKIUKWAJI HAKI ZA BINADAMU

BAVICHA YALAANI UKIUKWAJI HAKI ZA BINADAMU

Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399.
Mwenyekiti wa BAVICHA Taifa, Patrobass Katambi
BARAZA la Vijana la Chama cha Demokrasia na Maendeleo (BAVICHA), limelaani vikali kukithiri kwa muendelezo wa matukio ya ukiukwaji sheria na haki za binadamu unaofanywa na jeshi la polisi na serikali ya Chama Cha Mapinduzi (CCM).
Kauli hiyo, imetolewa jana na Mwenyekiti wa BAVICHA Taifa, Patrobass Katambi, wakati akitoa tamko kwa niaba ya Vijana na wadau wa amani, haki na usawa duniani kote.
Alisema CCM inatumia jeshi la Polisi kutekeleza malengo yake ya kisiasa ili kuua ushindani wa kisera.
Alisema kwa mjibu wa ibara ya 12 ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, inayosema kila binadamu wamezaliwa huru na wanayo haki sawa na wanapaswa kuheshimiwa, pia ibara ya 13 (3) inatoa ulinzi wa haki za kiraia, kimajukumu na matakwa ya mtu au jamii na 13 (4) inaagiza mtu yeyote kutobaguliwa na mtu au mamlaka yoyote.
“Tunaitaka Serikali itoe tamko na iwatangazie Watanzania na Umoja wa Mataifa kama ibara ya 3 (1),12, 13, 14, 18 na 21 za Katiba ya Jamhuri ya Muungano ya Mwaka 1977 hazitumiki na Serikali haizitambui mbali na viapo vya kuitii na kuilinda kwa viongozi wote akiwemo Rais Jakaya Kikwete.
“Pia serikali iwatamkie kwamba utii wa sheria bila shuruti utekelezwe na raia, vyama vya upinzani, wanaharakati wa haki za binadamu na wanahabari na siyo viongozi wa serikali, polisi na watawala,” alisema Katambi.
Aidha, alisema Serikali ya Tanzania itangaze kuwa haitambui na haifungwi na tamko la ulimwengu la haki za binadamu mwaka 1948 ya mkataba wa kimataifa unaopinga unyanyasaji na kutesa binadamu na mkataba wa haki za kisiasa na za kiraia 1966, pia na mkataba wa Afrika wa haki za binadamu na watu.
Alisema, Sheria ya vyama vya siasa ya Mwaka 1992 na Katiba ya Tanzania ya 1977, zinatoa haki ya maandamano ya amani kupinga ukiukwaji wowote wa haki, usawa, sheria, taratibu au kanuni msingi ya asili na kama inazitambua, iwachukulie hatua watendaji waliokiuka matakwa ya sheria.
Katika hatua hiyo, alisema endapo Serikali itapuuza malalamiko na madai dhidi ya unyama huo unaofanywa na jeshi la polisi kwa kushirikiana na chama tawala, hawatasita kuingia mtaani kupambana na kujichukulia sheria mkononi.

0 comments:

 
Supported by Tone Multimedia Company Limited
Copyright © 2012. Mtwara yetu - All Rights Reserved
Designed by Fredy Tony Njeje
Proudly powered by Blogs za Mikoa