Home » » WAZIRI AKIPA MASHARTI KIWANDA

WAZIRI AKIPA MASHARTI KIWANDA

Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399. 
 

WAZIRI wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais, Dkt. Binilith Mahende, ametoa miezi minne kwa kiwanda cha M.M Integrated Steel Mills Ltd kiwe kimefunga mitambo ya kutibu majitaka yanayozalishwa na kiwanda chao.

Waziri Dkt. Mahenge alitangaza hatua hiyo wakati akiwa kwenye ukaguzi kwenye kiwada hicho kilichopo jijini Dar es Salaam, ikiwa ni mfululizo wa ukaguzi anaoendelea kuufanya kwenye viwanda mbalimbali jijini humo.

Hatua hiyo imekuja baada ya Baraza la Taifa la Hifadhi ya Mazingira (NEMC), kupokea malalamiko kutoka kwa wanafunzi wa Chuo cha Kodi kilicho jirani na kiwanda hicho kuwa wanaathirika na majitaka ya kiwanda hicho.

Mbali na kupewa sharti la kufunga mitambo hiyo, Waziri Dkt. Mahenge aliutaka uongozi wa kiwanda hicho kuwasilisha Mpango wa Kuhifadhi Mazingira wa kiwanda hicho baada ya miezi mitatu ambao kuwepo kwake kunatiliwa shaka.

Hatua hiyo ilitokana na kiwanda hicho kushindwa kumridhisha waziri juu ya wapi wanaupeleka mchanganyiko wa mabaki ya madini mbalimbali yanayotumiwa na kiwanda hicho baada ya kuwepo kwa taarifa kuwa hutumika kinyume na taratibu.

Mbali na hayo, Waziri Dkt. Mahenge alitoa miezi mitatu wawasilishe ripoti ya ukaguzi wa mazingira kinyume cha hapo watatozwa faini na NEMC kwa mujibu wa sheria, kwani hawaruhusiwi kuendesha kiwanda katika hali hiyo.

Akizungumza kwa niaba ya uongozi wa kiwanda hicho Mkurugenzi wa Miradi ya kiwanda hicho, Lawrence Manyama, alisema watatekeleza maagizo hayo ingawa alidai kwa sasa wameacha kugawa mchanganyiko wa madini kwenye viwanda.

Katika kiwanda cha BIDCO Oil & Soap Ltd, Waziri huyo alitoa muda wa miezi 6 kwa kiwanda hicho kuacha kutumia magogo ya miti kama vyanzo vya nishati kwani matumizi hayo yanachangia kuharibu mazingira.

Alisema gharama za kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi yanayochangiwa na matumizi ya chanzo hicho ni kubwa sana kwa Serikali lakini pia kwa karne ya sasa kiwanda hicho kinatakiwa kuacha kutumia chanzo hicho.

Hata hivyo, mmoja wa wafanyakazi wa kiwanda hicho, Elias Nchwari, aliponea chupuchupu kuwekwa ndani na Mwanasheria wa NEMC, Manchare Heche,baada ya kumjibu vibaya Waziri Dkt. Mahenge wakati akiwasili kwenye kiwanda hicho.

Katika hatua nyingine Dkt. Mahenge alikipongeza kiwanda cha Coca Cola Kwanza kwa kupiga hatua kubwa ya mabadiliko ya matumizi ya nishati na katika kuhifadhi mazingira kwa kutumia mitambo ya kisasa kutibu majitaka.

Hata hivyo, aliutaka uongozi wa kiwanda hicho uwe mabalozi kwa viwanda vingine ambavyo havizingatii kuhifadhi mazingira katika uzalishaji wao, hivyo kuwa chanzo kikubwa cha kuchafua mazingira.

Naye Meneja Mkazi wa Uzalishaji wa kiwanda hicho, Luois Coetzee alisema pamoja na gharama kubwa waliyotumia katika nishati na mitambo ya kutakatisha majitaka, lengo lao kubwa ni kuhakikisha wanafanya mambo kwa usahihi wake.

Mtaalamu wa mitambo ya kutakatisha majitaka, Emiliana Kweka alisema wanalazimika kutumia mbinu mbalimbali kuhakikisha kuwa maji yanayotoka kwenye kiwanda hicho yanakuwa salama kwa mazingira na viumbehai.

 Chanzo:Majira

0 comments:

 
Supported by Tone Multimedia Company Limited
Copyright © 2012. Mtwara yetu - All Rights Reserved
Designed by Fredy Tony Njeje
Proudly powered by Blogs za Mikoa