Home » » TANZANIA KUJIFUNZA MAFUTA NA GESI CANADA

TANZANIA KUJIFUNZA MAFUTA NA GESI CANADA

Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399. 

SERIKALI ya Tanzania inatarajia kutuma wataalam kwenda nchini Canada katika Kamisheni ya Mafuta na Gesi ya jimbo la British Columbia (BC Oil& Gas Commission) ili kupata uelewa zaidi katika masuala ya udhibiti wa mafuta na gesi nchini.

Hayo yalisemwa na Naibu Waziri wa Nishati na Madini anayeshughulikia Nishati, Charles Kitwanga wakati akizungumza na watendaji wa Kamisheni ya Mafuta na Gesi ya Jimbo la British Columbia katika Ofisi za kamisheni hiyo zilizo katika mji wa Victoria nchini Canada.

Akiongoza ujumbe wa Tanzania uliotembelea kamisheni hiyo ili kujifunza masuala ya udhibiti wa sekta ndogo ya gesi asilia na mafuta, Naibu Waziri alisema kuwa lengo la Serikali ya Tanzania ni kuhakikisha kuwa rasilimali zilizopo zinaendelezwa na faida yake kuonekana kwa wananchi hivyo wataalam watakwenda nchini Canada katika kamisheni hiyo ili kuongeza uelewa katika masuala ya udhibiti ambao kwa kiasi kikubwa unachangia katika kuhakikisha kuwa na maendeleo endelevu ya rasilimali zilizopo Tanzania.

“Mtazamo wa wananchi wengi ni kuwa makampuni ya kigeni yanakuja nchini Tanzania kuchukua rasilimali na kuondoka nazo bila wananchi hao kufaidika hivyo serikali inafanya kila jitihada ili faida za rasilimali zetu ziwafikie wananchi wote na moja ya vigezo vya jitihada hizo ni kuwa na mamlaka madhubuti za udhibiti zitakazo hakikisha makampuni ya nje na ndani ya nchi yanafanya kazi kwa kuzingatia kanuni na sheria zinazoongoza sekta husika,” alisema Kitwanga.

Naibu Waziri alieleza kuwa Tanzania ikiwa katika mchakato wa kutengeneza sheria na kanuni zitakazoongoza sekta ya gesi asilia na mafuta, inahitaji kupata maoni na uelewa zaidi kutoka katika nchi zilizopiga hatua katika uendelezaji wa rasilimali hizo ikiwemo jimbo la British Columbia ambalo limegundua gesi asilia kiasi cha zaidi ya futi za ujazo trilioni 2,900.

Naye Ofisa Mkuu wa Operesheni katika Kamisheni ya Gesi na Mafuta ya British Columbia, Mhandisi Ken Paulson alieleza kuwa kamisheni hiyo ambayo imeanzishwa zaidi ya miaka 15 iliyopita ina jukumu la kudhibiti shughuli zote za mafuta na gesi asilia ikihusisha, utafiti, uendelezaji na usafirishaji wa rasilimali hizo kwa njia ya bomba.

Mhandisi Paulson alieleza kuwa kamisheni hiyo pia ina jukumu la kukusanya takwimu za ki jiolojia zinazotumika katika shughuli za utafutaji wa gesi asilia na mafuta na kuzitangaza kwa njia ya tenda ili makampuni yanayohitaji kufanya shughuli za utafutaji mafuta na gesi katika jimbo hilo yanunue takwimu hizo kutoka kamisheni hiyo.

Kuhusu matumizi ya gesi asilia, Ofisa Mkuu wa Operesheni aliueleza ujumbe huo kutoka Tanzania kuwa asilimia 15 ya kiasi cha gesi kilichogunduliwa katika jimbo hilo kinatumika ndani ya jimbo la British Columbia kwa matumizi mbalimbali na kiasi kinachobaki kinasafirishwa kwenda bara la Amerika Kaskazini.

Kuhusu mfumo wa ugawanaji mapato (PSA) kati ya kampuni ya utafutaji na uchimbaji gesi asilia na mafuta, Mhandisi Paulson alieleza kuwa kampuni ikianza uzalishaji wa gesi au mafuta, serikali ya jimbo hilo hukusanya mrabaha wa asilimia 10 hadi 20 ya mapato.

Katika ziara hiyo ya mafunzo nchini Canada, Naibu Waziri wa Nishati na Madini ameambatana na Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini, Victor Mwambalaswa pamoja na baadhi ya wajumbe wa Kamati hiyo akiwemo, Murtaza Mangungu, Raya Ibrahim, Richard Ndasa, Deogratias Ntukamazina, Shafin Sumar na wataalam kutoka Wizara ya Nishati na Madini.

Chanzo:Majira

0 comments:

 
Supported by Tone Multimedia Company Limited
Copyright © 2012. Mtwara yetu - All Rights Reserved
Designed by Fredy Tony Njeje
Proudly powered by Blogs za Mikoa