Home » » SEKTA BINAFSI WATAKA MAZINGIRA YA UWEKEZAJI MADINI,GESI YABORESHWE

SEKTA BINAFSI WATAKA MAZINGIRA YA UWEKEZAJI MADINI,GESI YABORESHWE

Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399. 
Katibu Mkuu Kiongozi, Balozi Ombeni Sefue
 
Wawekezaji kutoka sekta binafsi nchini, wameitaka serikali kuweka mazingira mazuri ya uwekezaji katika sekta za madini, gesi asilia na mafuta ili kuvutia wawekezaji wasiondoke nchini.
 
Aidha, wameitaka serikali kuwa makini katika utekelezaji wa sera na sheria ambazo baadhi yake zimeshafanyiwa marekebisho ili kuepuka na urasimu na vitendo vya rushwa.
 
Tahadhari hiyo ilitolewa jana na wawakilishi kutoka kampuni na sekta mbalimbali binafsi katika mkutano wa kutoa maoni kuhusu misingi 12 iliyopo kwenye Mkataba wa Taifa wa Maliasili nchini (TNRC).
 
Mchakato wa kupitia misingi hiyo iliyomo kwenye mkataba huo ambao unaeleza namna Watanzania na taifa kwa ujumla, wanavyoweza kunufaika na rasilimali zilizopo nchini zikiwamo gesi asilia, mafuta na madini, ulizinduliwa mwaka jana na Katibu Mkuu Kiongozi, Balozi Ombeni Sefue.
 
Wakitoa maoni yao katika mkutano huo uliofanyika jana jijini Dar es Salaam, chini ya uratibu wa Taasisi ya Uongozi nchini, walisema wawekezaji wanakimbia nchini kutokana na mazingira ya uwekezaji kutokuwa mazuri, zikiwamo sera na sheria zake.
 
Pia walihoji iwapo maoni yaliyotolewa kwa ajili ya  kuboresha eneo hilo, yatafanyiwa kazi kwa madai ya kwamba tayari mikataba imetolewa kwa wawekezaji na halmashauri.
 
Balyoruguru alihoji iwapo maoni yanayotolewa  kutoka makundi mbalimbali kuhusu namna wazawa watakavyoweza kunufaika na rasilimali hizo kwa madai ya kwamba tayari wawekezaji wameshaingia mkataba na serikali pamoja na halmashauri.
 
Naye Mkurugenzi mtendaji wa  Tan Discovery-Mineral Consultancy Company Limited, Rogers Sezinga, alisema, sekta zote za serikali zina sera na sheria za lakini hakuna mpango wa utekelezaji na kwamba serikali inapaswa kufanya maamuzi kwenye eneo hilo ili kuboresha mazingira ya uwekezaji na kuhakikisha wananchi wananufaika na rasilimali hizo.
 
“Idara za serikali zina mipango na sera nzuri za maendeleo lakini hakuna utekelezaji, kuna upotevu mkubwa katika uvunaji wa rasilimali za nchi,” alisema.
 
Kwa mujibu wa Sezinga, nusu ya wawekezaji wanaondoka nchini na kwenda nchi nyingine kwa madai kuwa serikali haina uwekezaji wa kutosha kwenye migodi na kutokana na hilo migodi mingi ya madini ipo mbioni  kufungwa kwa siku za usoni.
 
Naye Afisa Mtendaji Mkuu wa Taasisi ya Uongozi nchini, Prof. Joseph Semboja, wakati akitoa utangulizi katika mkutano huo, alisema, iwapo hakutakuwapo na usimamizi mzuri wa rasilimali hizo, itakuwa ni majuto kwa Watanzania bali zikisimamiwa vizuri, wananchi watakwenda kunufaika nazo.
 
Kwa upande wake mtafiti kiongozi kutoka Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Prof. Amon Mbelle, alizitaka sekta binafsi kutoa maoni ambayo yatasaidia kuimarisha mfumo bora wa utoaji maamuzi na kuangalia sababu zinazofanya kuwapo kwa mapengo zikiwamo taarifa za ukuaji wa uchumi usioendana na hali halisi ya maisha iliyopo.
 
Alitaka watoa maoni hao pia kuangalia mapengo mengine yakiwamo ya kuwa na matumizi makubwa yanayozidi mapato.
 
CHANZO: NIPASHE

0 comments:

 
Supported by Tone Multimedia Company Limited
Copyright © 2012. Mtwara yetu - All Rights Reserved
Designed by Fredy Tony Njeje
Proudly powered by Blogs za Mikoa