Home » » MAPATO YA GESI ASILIA TANZANIA KULIZWA

MAPATO YA GESI ASILIA TANZANIA KULIZWA

Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399.
Mbunge wa Kigoma Kaskazini,Zitto Kabwe
 
Takribani mwezi mmoja baada ya Kamati ya Bunge ya Uchumi, Viwanda na Biashara kuishauri Serikali kupitia upya mikataba ya gesi ili kubaini iwapo kweli inawanufaisha Watanzania na kama maslahi ya taifa yamezingatiwa, habari mpya zimeibuka kuwa  huenda Tanzania ikapoteza karibu Sh. trilioni 1.6 kila mwaka katika sekta ya gesi asilia.
Kiwango hicho kinaelezwa kuwa kitategemea viwango vya uzalishaji wa gesi asilia kitakachozalishwa nchini.

Uwezekano huo uliotolewa na Mbunge wa Kigoma Kaskazini, Zitto Kabwe, unashikamana na kauli ya Kamati ya Bunge ya  Uchumi, Viwanda na Biashara iliyowasilishwa na Mwenyekiti wake Luhaga Mpina bungeni Juni 4 mwaka huu.

Mpina alikuwa akiwasilisha maoni ya Kamati hiyo juu ya makadirio ya matumizi ya wizara ya Fedha kwa mwaka wa fedha wa 2014/15.

Kauli ya Zitto ya sasa ambaye alikuwa waziri kivuli wa fedha, inazidi kufunua hali ilivyokaa katika sekta ya gesi asilia kwa kuwa hadi sasa mikataba ya kugawana mapato haijakaa kuisaidia Tanzania kama ambavyo viongozi wengi wamekuwa wakieleza.

Ziito alisema kuwa uwazi unapaswa kuwa ndiyo mwongozo ili kufanikisha ndoto ya Tanzania ya kubadili utajiri wake wa maliasili kuwa na tija kwa wananchi wake.
Hivyo alihimiza kampeni ya kuweka wazi mikataba yote iliyo kwenye upande wa rasilimali ya gesi na mafuta, hali ambayo ni ya kawaida kwenye kampuni ndogo zinazotafuta kuongeza mitaji yao kupitia masoko ya hisa.

“Kwa kweli habari zilizotolewa kwenye kijitabu cha kampuni ya Swala kinaenda mbali ya kile kilichovuja toka kampuni ya Statoil/Exxon, ambapo kwa ufasaha kijitabu hicho kinajumuisha programu za kazi na malipo ya lazima kama yale ya ushuru wa mafunzo, kati ya mengi,” alisema.

Zitto alisema ni watu wachache wanaoweza kuelewa, lakini wakati taarifa za Mkataba wa Mgawanyo wa Mapato Yanayotokana na Uzalishaji wa Gesi Asilia (PSA),  kati ya Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC) na Kampuni ya Mafuta ya StatOil ya Norway zilipovuja kupitia mitandao ya habari ya kijamii, majadiliano yalizimwa.

Kwa mujibu wa Zitto, nyaraka iliyovuja siyo ya PSA haswa, lakini ni nyongeza kwa ile ya awali ya kitalu namba 2 na hasa ikichukuliwa kwamba uvumbuzi huo ni wa gesi asilia na si mafuta.

Makubaliano ya awali ya mkataba wa mgawanyo wa mapato yanayotokana na uzalishaji wa gesi asilia (PSA) yalifikiwa na kampuni hiyo ya Statoil mwaka 2007, wakati wizara ya Nishati na Madini ikiongozwa na Waziri Nazir Karamagi.

Zitto alisema kuwa makubaliano hayo ya awali kimsingi yalijikita kwenye mfano wa mkataba wa mgawanyo wa mapato yanayotokana na uzalishaji wa gesi asilia (PSA Model) wa mwaka 2004.

Alisema kuwa nyongeza iliyosainiwa na Statoil ilijikita kwenye nyongeza ya mfano wa mkataba iliyohitimishwa mwaka 2008, ikijumlisha masharti ya mkataba kwa ajili ya gesi.

Alisema kuwa nyongeza hiyo ilisainiwa Februari Mwaka 2012, wakati William Ngeleja akiwa waziri wa wizara hiyo.

Zitto alifafanua kuwa ni wazi masharti waliokubaliana yana manufaa zaidi kwa Statoil na Exxon kuliko kwa wananchi wa Tanzania.

Akiongelea tofauti zilizopo, Zitto alisema Kifungu cha 8.1 (i) kinaweka wajibu wa soko la ndani kinataka asilimia kumi ya uzalishaji uhifadhiwe kwa ajili ya soko la ndani.
CHANZO: NIPASHE

0 comments:

 
Supported by Tone Multimedia Company Limited
Copyright © 2012. Mtwara yetu - All Rights Reserved
Designed by Fredy Tony Njeje
Proudly powered by Blogs za Mikoa